Shirika la Rafiki Social Development
Organization – SDO la mkoani Shinyanga leo Jumanne Agosti 15,2017
limezindua Mradi wa ulinzi wa mtoto, haki za watoto na utawala
utakaotekelezwa kwa kipindi cha miaka miwili katika kata 30 kwenye
halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga,Shinyanga Vijijini na Kahama Mji.
Uzinduzi wa mradi huo umefanyika katika
ukumbi wa Ibanza Hotel Mjini Shinyanga ambapo mgeni rasmi alikuwa mkuu
wa wilaya ya Shinyanga,Josephine Matiro.
Akizungumza wakati wa kuzindua mradi
huo,Matiro alilitaka shirika hil0 kushirikiana na wadau mbalimbali
wakiwemo viongozi wa jadi la sungusungu,serikali,viongozi wa dini,kimila
na wananchi.
“Niwapongeze sana Rafiki SDO kwa kupata
mradi huu muhimu kwa ajili ya ulinzi wa watoto,sote tunatambua kuwa
vitendo vya ukatili wa watoto vimekithiri katika jamii,serikali pekee
haiwezi kumaliza vitendo hivi,lazima tushirikiane ili watoto wetu wawe
salama”,alisema Matiro.
“Natamani kusikia mashirika yanajitokeza
kuanzisha miradi kwa ajili ya kupambana na vitendo vya ulawiti
wanavyofanyiwa watoto wetu,taarifa nilizo nazo ni kwamba baadhi ya
watoto wa kiume waliopo katika shule za msingi wanafanyiwa mchezo mbaya
wa kulawitiwa,tena wanafanyiwa na watu wazima,hili halikubaliki lazima
tushirikiane kumaliza tatizo hili”,aliongeza Matiro.
“Naomba mashirika yanayojihusisha na
masuala ya watoto yajitokeze na kuanzisha miradi ya kusaidia watoto
wanaolawitiwa,tunapaswa kuwalinda watoto hawa,kinachotakiwa ni
ushirikiano japo changamoto katika kesi za ukatili ni wazazi na walezi
kumaliza kesi kienyeji”,alisema Matiro.
Katika hatua nyingine aliwataka wazazi
na walezi kutoa ushirikiano katika vyombo vya dola pale panapotokea
watoto wamefanyiwa vitendo vya kikatili na kunyimwa haki zao.
Akizungumza wakati wa uzinduzi
huo,Mkurugenzi wa Shirika la RAFIKI SDO,Gelard Ng’ong’a alisema mradi
huo unatekelezwa na Shirika la Rafiki SDO kwa kushirikiana na shirika la
kimataifa la kuhudumia watoto “Save The Children International” kwa
hisani ya shirika la Maendeleo la nchini Sweeden – SIDA.
Ng’ong’a Mradi huo unalenga kumlinda
mtoto na kuhakikisha watoto wanapata haki zao pamoja na kuwajengea uwezo
wa kupaza sauti zao ili kuhoji haki hizo kutoka kwa wazazi, viongozi na
wadau wengine wanaohusika.
“Kupitia mradi huu,tunaamini vitendo vya
ukiukwaji wa haki za watoto vilivyokithiri mkoani Shinyanga vitapungua
kwa asilimia 20% katika kata 30 za Manispaa ya Shinyanga, Shinyanga
vijijini na Mji wa Kahama ifikapo mwezi wa Novemba mwaka 2018”,alisema
Ng’ong’a.
Aidha alisema mradi huo utasaidia
kuongeza utumiaji wa mifumo rasmi kama vile ofisi za ustawi wa jamii,
dawati la jinsia na watoto pamoja na vituo vya huduma viliyowekwa na
serikali na wadau wengine katika kumlinda mtoto na haki zake.
“Tunatarajia pia ongezeko la ushiriki wa
watoto katika kutoa maamuzi, kuhoji na kudai haki zao kutoka kwa wazazi
na wadau wengine wanaopaswa kuwahudumia watoto”,aliongeza Ng’ong’a.
Kwa upande wake Meneja Mradi wa ulinzi
wa mtoto, haki za watoto na utawala kutoka shirika la Rafiki SDO,Shangwe
Kimath alisema ili kufanikisha mradi huo ipasavyo wamejipanga kutoa
mafunzo na kuongeza uelewa wa ulinzi wa mtoto kwa jamii, kuhamasisha
ushirikishwaji wa mtoto na uragbishi na ushawishi.
“Pamoja na mambo mengine tumeandaa
kampeni za kuhusisha wanaume katika malezi na makuzi ya watoto na
kuwajengea uwezo viongozi na watendaji wa serekali za mitaa, wazazi,
waalimu na kamati za ulinzi wa mtoto juu ya ulinzi wa mtoto na utawala
wa haki za watoto”,alieleza Kimath.
Naye Meneja wa Shirika la Save The
Children mkoa wa Shinyanga,Benety Malima alisema mradi huo unatekelezwa
katika mikoa mitatu nchini Tanzania,ambayo ni Shinyanga,Dar es salaam na
Songwe.
“Tunaishukuru serikali kwa kuendelea
kushirikiana nasi katika utekelezaji wa miradi mbalimbali,tunampongeza
mkuu wa wilaya Josephine Matiro kwa ushirikiano wa kutosha ambao amekuwa
akitupatia,suala la ulinzi wa motto linahitaji ushirikiano wa wadau
wote”,aliongeza Malima.
Mradi huo utatekelezwa katika
halmashauri ya manispaa ya Shinyanga kwenye kata ya Ngokolo, Ndembezi ,
Masekelo Ndala, Kambarage, Ibinzamata Chamaguha, Chibe, Lubaga na Old
Shinyanga na katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga ni kwenye kata ya
Salawe, Lyamidati, Mwenge, Mwantini, Tinde, Didia, Solwa, Iselamagazi
Lyabusalu na Lyabukande.
Kwa upande wa halmashauri ya Mji wa
Kahama mradi utatekelezwa kwenye kata ya Mwendakulima, Nyihogo,
Kagongwa, Nyasubi, Majengo, Kahama mjini, Mhongolo Zungomela, Nyandekwa
na Busoka.
ANGALIA PICHA ZA MATUKIO WAKATI UZINDUZI WA MRADI HUO
Wa kwanza kushoto ni Afisa Ustawi wa
jamii Manispaa ya Shinyanga John Nhabi,akifuatiwa na Mkuu wa wilaya ya
Shinyanga Josephine Matiro,Mkurugenzi wa Shirika la RAFIKI SDO,Gelard
Ng’ong’a na Meneja wa Shirika la Save The Children mkoa wa
Shinyanga,Benety Malima (wa kwanza kulia) wakiwa katika ukumbi wa Ibanza
Hotel Mjini Shinyanga wakati wa uzinduzi wa mradi wa ulinzi wa mtoto,
haki za watoto na utawala
Mkuu
wa wilaya ya Shinyanga,Josephine Matiro akizungumza wakati wa uzinduzi
wa Mradi wa ulinzi wa mtoto, haki za watoto na utawala utakaotekelezwa
na Shirika la Rafiki SDO kwa kushirikiana na shirika la kimataifa la
kuhudumia watoto “Save The Children International” kwa hisani ya shirika
la Maendeleo la nchini Sweeden – SIDA.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Josephine Matiro akizungumza ukumbini.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Josephine Matiro akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akizungumza ukumbini.
Wadau wakiwa ukumbini wakati wa uzinduzi wa mradi huo.
Wadau mbalimbali wa masuala ya watoto
kutoka kata 30 za halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Vijijini,Manispaa
ya Shinyanga na Kahama Mji ambako mradi huo utatakelezwa
wakifuatilia kilichokuwa kinaendelea ukumbini.
Mkurugenzi wa Shirika la RAFIKI
SDO,Gelard Ng’ong’a akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mradi wa ulinzi wa
mtoto, haki za watoto na utawala.
Mkurugenzi wa Shirika la RAFIKI
SDO,Gelard Ng’ong’a akieleza namna mradi huo utakavyosaidia kupunguza
vitendo vya kikatili dhidi ya watoto.
Mkurugenzi wa Shirika la RAFIKI
SDO,Gelard Ng’ong’a akizungumza ukumbini ambapo alisema ili kufanikisha
mradi huo pia panahitajika bajeti kutoka serikalini kwa ajili ya watoto.
Wadau wakifuatilia kilichokuwa kinaendelea ukumbini.
Meneja wa Shirika la Save The Children
mkoa wa Shinyanga,Benety Malima akieleza namna wanavyoshirikiana na
serikali katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika jamii.
Wadau wakiwa ukumbini.
No comments:
Post a Comment