Na Nassir Bakari, Dar es salaam
Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), kupitia Idara yake ya Vyuo na Vyuo vya Elimu ya Juu, umemkingia kifua Mwenyekiti wa CCM Rais Dk. John Magufuli ukisema kwamba hafanyi uteuzi kwa njia za kibaguzi bali anafanya hivyo kwa kuzingatia weledi na uwezo wa anayemteua.
UVCCM imesema, hayo leo jijini Dar es Salaam, na kupinga vikali kauli iliyotolewa hivi karibuni na Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu, kwamba Rais Dk. Magufuli amekuwa akifanya uteuzi kwa kuzingatia ubaguzi wa ukanda, ukabila, dini na jinisa.
Akifungua Kikao cha kazi cha Viongozi wa Vyuo na Vyuo vikuu mkoa wa Dar es Salaam, Kaimu Katibu Mkuu Idara ya Vyuo na Vyuo Vikuu- UVCCM, Daniel Zenda alisema, UVCCM kupitia Idaya yake, inapinga na kulaani vikali kauli hizo za Tundu Lissu kwa sababu ni kauli za hatarai kwa kuwa zina lengo la uchochezi, kudhalilisha na kugawa Wananchi kwa misingi ya kibaguzi.
"Ndugu Watanzania kauli hii ya Tundu Lissu ni yenye lengo la kuchonganisha, kudhalilisha na kuwagawa wananchi, Sisi Vjana wa Vyuo na vyuo Vikuu, tunalaani kwa nguvu zetu zetu kauli hii. Kwa mfano ukitazama uteuzi wa Mkuu wa Majeshi nchini anatoka Bara, lakini hupo chini ya Waziri wa Ulinzi Dk. HusseinMwinyi ambaye anatoka Zanzibar", sasa hapo ubaguzi unakujaje", alisema na kuhoji.
Alisema, kimsingi katika kufanya uteuzi, Rais anazingatia haki yake ya kikatiba ambayo inampa mamlaka ya kuteua na kutengua kwa kadri anavyoona inafaa. "ibara ya 36 kifungu cha pili ambayo kinasema Rais atakuwa na madaraka ya kuteua watu wa kushika nafasi za madaraka ya viongozi wanaowajibika kuweka sera za idara za taasisi za Serikali na watendaji wakuu wanaowajibika kusimamia utekelezaji wa sera za idara hizo", alifafanua.
"Mnajua siasa ni kama dawa, dawa huwa inaisha muda wake, sasa huyu Tundu Lissu naye amekwisha muda wake kisiasa, ndiyo maana inafika wakati anazungumza maneno ya kipuuzi katika jamii, nawaomba ndugu Watanzania wenzangu tuyapuuze maneno yake, hayana maana, Ndugu Wananchi wa Singida Mashariki tunawaomba 2020 msifanye makosa tena tuleteeni anayefaa kuliko huyu Tundu Lissu", alisema Zenda.
Alisema, kuisha kisiasa kwa Tundu Lisu na upinzani kwa jumla, kunatokana na uchapakazi ulioonyeshwa na uongozi wa awamu ya tano, chini ya Rais Dk. Magufuli. " Hawa kina Tundu Lisu kwa sasa hawana hoja, ndiyo maana sasa wanatapatapa kujaribu kutafuta pa kushika.
"Sisi kama vijana wasomi tunaiunga mkono Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk. Magufuli kwa mambo yote inayoyafanya, Watanzania wenyewe tumekuwa ni mashahidi wazuri wa hayo mambo, tunaomba Mungu ampe afya njema ili aendelee kututumikia Watanzania" alisema Zenda.
No comments:
Post a Comment