Monday, July 24, 2017

UVCCM YALAANI UKIUKWAJI AGIZO LA RAIS WILAYANI UKEREWE

Na Wazo Huru Blog, Ukerewe-Mwanza

Umoja Wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa umelaani vikali ukiukwaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli unaofanywa na Baadhi ya Viongozi wa Serikali wa Wilaya kwa kuwatoza wananchi tozo mbalimbali ambazo zimezuiliwa.

Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa Ndg Shaka Hamdu Shaka Leo Julai 23, 2017 Wilayani Ukerewe Mkoani Mwanza Wakati wa ziara ya siku moja alipokuwa akizungumza na Vijana wa Jumuiya ya Chama hicho (UVCCM) pamoja na  wanachama wa chama cha Mapinduzi (CCM) kijijini Kitanga, Kata ya Kakukuru.

Ndg Shaka (MNEC) amesema kuwa kauli yoyote inayotolewa na Rais ni sheria hivyo kila mwananchi wakiwemo watendaji mbalimbali wa Serikali wanapaswa kutekeleza kwani  wasipofanya hivyo ni kukiuka taratibu na sheria za nchi.

"Ndugu zangu kukiuka maagizo ya Rais ni utovu wa nidhamu na kwa mujibu wa sheria za nchi yetu mtovu yeyote wa nidhamu anapaswa kuchukuliwa Hatua Kali za kisheria" Alisema Shaka

Alisema kuwa Mhe Rais Magufuli hivi karibuni alipiga marufuku utozwaji wa ushuru wa mazao kwa wakulima na wafanyabiashara wadogo na kuwaagiza wakuu wa mikoa kote nchini Kusimamia ipasavyo jambo hilo ambalo limekuwa kero inayogandamiza watanzania wanyonge.

"Hivyo kufuatia kauli hiyo ambayo inalandana na Ilani ya ushindi ya Chama Cha Mapinduzi ya  Mwaka 2015-2020 ni wazi kuwa kila mtendaji ama wa Serikali ama wa chama anapaswa Kusimamia ilani ipasavyo" Alisema Shaka

Awali Kaimu Katibu Mkuu huyo alizindua  mashina ya wakereketwa Kakukuru Kijijini Murutilima na  kuzindua Shina la Wakereketwa eneo la Kitanga katika Kata ya Kakukuru.

Katika Hatua nyingine Shaka alisema kuwa Vikundi vyote ambavyo vimeanzishwa na kusajiliwa kwa mujibu waTaratibu vinapaswa kuandika barua ya kuomba fedha za mikono zinazotolewa na Halmashauri Asilimia 5 kwa Vijana na Wanawake.

Ziara hiyo ya siku moja Wilayani Ukerewe imemalizika ambapo kesho Julai 24, 2017 Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa Ndg Shaka Hamdu Shaka ataanza ziara ya siku moja katika Wilaya ya Ilemela.

MWISHO.

Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa Ndg Shaka Hamdu Shaka akizungumza Wakati wa Ziara yake WILAYANI Ukerewe

No comments:

Post a Comment