Monday, July 24, 2017

POLEPOLE AWAASA WAJUMBE WA HALMASHAURI KUU YA MKOA WA KILIMANJARO KUISHI MISINGI YA CCM MPYA

Akiwa ziarani Mkoa wa Kilimanjaro Ndg.Polepole katibu wa NEC Itikadi na Uenezi alipata nafasi ya kuwa mgeni kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya Mkoa wa Kilimanjaro.
Amewasisitiza Wajumbe wa kikao kuishi misingi ya CCM MPYA kwa kutosita kuambiana ukweli wakati wa kuchakata majina ya wagombea wa nafasi mbalimbali na kutoweka urafiki, uswahiba na undugu katika hatua ya kupitisha majina.

Akifafanua baadhi ya misingi ya Mageuzi Makubwa yanayofanywa na CCM, ameeleza, “
*Tunataka mtupatie viongozi ambao ni waaminifu, waadilifu, wachapa kazi, wanyenyekevu, wanaochukia rushwa, wanaochukizwa na ubadhirifu wa mali za Chama na Umma, watu ambao wataweka mbele maslahi ya Chama na wanachama na kuhamasisha umoja katika chama chetu*

Kikao cha Halmashauri kuu Mkoa wa Kilimanjaro kimefanyika katika ukumbi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro na kuongozwa na Mwenyekiti  wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro Ndg. Iddy Juma.

Pamoja na mambo mengine Ndugu Polepole amewaomba wajumbe wa kikao Kuhakikisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinakuwa  sauti ya wananchi na kuielekeza Serikali yao nini shida na changamoto za wananchi. Pia Chama kinapaswa  kifafanue serikali inafanya nini na kwanini. Aidha amesisitiza viongozi kutokuwa na haya katika kusimamia kweli na kuhakikisha wanatenda haki na  kutokumuonea mtu yeyote katika mchakato wa uchaguzi.

*Kikao hiki ni moja wapo ya vikao muhimu kabisa, kikao cha ngazi ya juu chenye dhamana ya kuona nani anafaa kuwa kiongozi wetu. Mtupatie viongozi ambao wakisimama hata wasiyo wanaCCM watatuheshimu na kutuamini* alisema Ndugu Polepole.

Ndg. Polepole alihitimisha kwa kuwatakia wajumbe viongozi kikao chema cha Halmashauri Kuu ya Mkoa wa Kilimanjaro.

Ndugu Humphrey Polepole yupo ziarani mkoa wa Kilimanjaro, kuimarisha na kuhuisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) hasa kipindi hiki cha Mageuzi Makubwa yanayofanywa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Ziara hii ni muendelezo wa ziara za kichama na vikao vya ndani vyenye lengo la kutoa hamasa, kuvumisha umuhimu wa Mageuzi ya Chama, kuimarisha Chama na kutatua kero za wanachama.

IMETOLEWA NA,
IDARA YA ITIKADI NA UENEZI
CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM)

No comments:

Post a Comment