Saturday, July 22, 2017

UVCCM: MTENDAJI KIKWAZO AJIONDOE SERIKALINI

Na mwandishi wetu Kigoma.

 Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) umewataka watendaji dhamana wa serikali na halmashauri za wilaya  kutojisahau badala yake wajione kuwa wana wajibu usiokwepeka wa kushirikiana na serikali ya Chama Cha Mapinduzi kilichoshinda na kuunda dola. 

Pia Umoja huo umesema Mtendaji yeyote wa Serikali anayedhani au kufikiri kuwa mfumo wa chama kushika hatamu umekwisha,  anakosea kwasababu kila pale chama kinaposhinda na kuunda dola, chama hicho ndicho chenye dhamana ya kuongoza . 

Matamshi hayo yametamkwa na Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM  Shaka Hamdu Shaka alipozungumza, makundi ya Vijana, wanachama wa CCM na jumuiya zake kwenye ofisi za ccm Kibondo Mjini Mkoani hapa. 

Shaka alisema CCM ndicho chama kilichoshinda uchaguzi mkuu wa oktoba  mwaka 2015 hivyo hakitakubali au kuvumilia kupuuzwa na mtumishi au mtendaji katika ngazi yoyote kwani bila kupatikana mtaji wa CCM  serikali isingeshika madaraka.

Alisema CCM  na jumuiya zake hakihitaji kuhasimiana wala kuvutana na mtendaji au mtumishi wa umma yoyote lakini hakitakaa kimya pale mtu mmoja atakapothubutu kusita kusimamia utekelezaji wa ilani aidha kwa kushawishiwa,  uzembe wake au kwa kutaka kukitunishia misuli. 

"Wapo watu bado wanadhani ati ndani ya vyama vingi hakuna  chama kinachoshika hatamu, hatamu ndani ya vyama vingi ni chama kupewa idhini ya kidemokrasia na wananchi hadi kuwekwa madarakani kikatiba na kisheria, ieleweke kuwa hakuna   ng'ombe wake mwenyewe  akakubali  kusimama mkiani" Alisema Shaka  huku akishangiliwa.

Aidha Shaka alifahamisha kuwa  ikiwa yupo mtendaji yeyote na mtumishi ambaye hayupo tayari kuonyesha ushirikiano katika Serikali inayoongozwa na Rais Dk John Magufuli, hana sababu hata moja ya kuendelea kubaki serikalini  badala yake ajitoe kisha aende mahali anakokuamini na kukuheshimu.

Hata hivyo kaimu  Katibu Mkuu aliwaasa wanachama hao wa CCM  kutojiona wanyonge mbele ya serikali yao na wala wasiwe wazito  katika kumfichua kiongozi au mwanachama msaliti, kuwadi au ndumilakumili kwani ccm haina njaa ya kubaki na wanachana wanokihujumu chama hicho .

"Usiku unashirikiana  na sisi katika mipango yetu ukiwa na sare ya kijani, asubuhi bila aibu unatuuza kwa bei nafuu huku ukiwa umevikwa gwanda, huwezi kuwatumikia mabwana wawili kwa wakati mmoja. Ondoka mwenyewe kwa hiari yako  bila  shari"Alieleza Shaka 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa uvccm mkoa wa Kigoma Peter Msanjila alisema UVCCM haitakubali kumvumilia mtendaji au mtumishi ambaye hapendi ushirikiano na ccm na watakuwa tayari kumjadili na kuutangaza hadharani usaliti na hujuma zake .

Msanjila alisema UVCCM inamsifu utendaji wenye uwazi, ukweli na uwajibikaji chini ya serikali ya awamu ya tano na kuwataka vijana nchini waendelee kumuunga mkono Rais Dk Magufuli kwasababu ni mpigania haki na usawa. 

No comments:

Post a Comment