Saturday, July 29, 2017

RC MAKONDA APOKEA TAARIFA YA OPARESHENI TOKOMEZA WIZI WA VIFAA VYA MAGARI

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mheshimiwa _*Paul Makonda*_ leo amepokea ripoti ya maagizo ya siku saba aliyoyatoa kwa Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam *DCP Lucas Mkondya* kuhakikisha wanatokomeza wizi wa vifaa vya magari.

Katika operesheni hiyo jumla ya *watuhumiwa 73* walikamatwa na vifaa vya Magari vilivyoibiwa ikiwmo Power Window *40, Radio 12Taa za Magari 105, Side Mirrors 92, Vitasa vya Magari 109,Bampa 4, Air Cleaner 1, Booster 3, Show Grill 6, Mashine moja ya kupandisha vioo na Tyre zilizotumika 2.*

Akizungumza baada ya kupokea Ripoti hiyo _*Makonda*_ amewataka wananchi wote waliopotelewa au kuibiwa vifaa vya magari kufika Jeshi la Polisi kanda Maalumu kwa Kamanda *Lucas Mkondya* kwaajili ya kurudishiwa vifaa vyao bila malipo.

Aidha _*Makonda*_ ameliagiza tena Jeshi la Polisi kusambaratisha wafanyabiashara wa magari (Madalali) wanaofanya biashara ya kuuza magari katika maeneo yasiyo rasmi na kusababisha serikali kukosa mapato.

_*“Sitaki kuona wafanyabiashara wa magari wanaofanya biashara kama udalali, magari yale hawalipii kodi na wanafanya biashara barabarani na wamechukuwa maeneo na mwisho wa siku kuwa kero kwa wananchi, ukienda maeneo ya Mlimani City kuna vijiwe, Mnazi mmoja nako wapo na sehemu nyingine, kuanzia leo watafute au wajiunge na watu wenye leseni ya kuuza magari ili na Serikali ipate Mapato”*_ Alisema _Makonda._

Mbali na hilo pia ameagiza Jeshi hilo kutokomeza maeneo ambayo yamekuwa yakitumika kama bandari Bubu na kusambaratisha wezi wa Magari ambao pia wamekuwa wakiiba Magari na kuuza kifaa kimojakimoja.

Amewasisitiza wananchi wote wanaokwenda kununua vifaa vya magari kuhakikisha wananunua kwenye maduka yaliyosajiliwa na pindi wanaponunua wahakikishe wanapatiwa risiti.

Kwa Upande wake Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam *DCP Lucas Mkondya* amesema kuwa watahakikisha wanatekeleza maagizo hayo kwa wakati huku akisisitiza kuwa oparesheni hizo ni endelevu.

No comments:

Post a Comment