Ilala, Dar es salaam
Mkuu wa Wilaya ya Iala Mh. Sophia Mjema, Leo amepokea maandamano ya madereva wa bodaboda wilaya ya Ilala zaidi ya 200 yenye lengo la kuunga mkono na kumpongeza Mhe. Rais John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa aliyoifanya katika kipindi alichokuwa madarakani. Akizungumza mmoja wa Madereva hao kwa niaba ya wenzake katika risala yao walisema *“Madhumuni ya mkusanyiko huu ni kumpongeza Rais wetu, Mzalendo namba moja, Mwana Mapinduzi, mtu jasiri,mpenda maendeleo, mtetezi wa wanyonge, mwana magogoni na siyo mwingine bali ni Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli”*
Aidha vijana hao walitaja sababu ya kuchukua uamuzi huo ambayo ni uthubutu wa aina yake aliouonesha Rais Magufuli ikiwemo kuzuia kusafirishwa nje machanga wa madini (Makinikia) ambayo yameligharibu taifa letu matrilioni ya shilingi, mapambano ya kiuchumi, ujenzi wa miundombinu ikiweno Reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa, kusimamia makusanyo ya kodi pamoja na kuwapigania wanyonge kama vile wafanyabiashara wadogo (machinga) na bodaboda.
Wakieleza kilio chao na kumuomba Rais Magufuli kuwatetea, walisema *“….tunaomba kuwasilisha changamoto zetu chache ambazo tuna imani Baba yetu Rais wetu Magufuli kututetea. Tunaomba atusaidie kuwepo na mfumo mzuri wa usafiri wa bodaboda utakaokuwa unaheshimika na kutambulika na nyombo vya usalama. Mpango huu utaifanya shughuli yetu ya bodaboda kutambulika rasmi ili kunufaika na fursa zitolewazo na serikali”*.
Changamoto zingine walizotaja ni pamoja na vitendo vinavyofanywa na kampuni ya kukamata pikipiki ya tambaza ambayo vijana wake hukamata bodaboda bila utaratibu hivyo kusababisha ajali, utozaji wa faini bila risiti hivyo kuashiria kwamba ni vitendo vya ukwepaji wa kodi. Jeshi la polisi nalo liliguswa kuwa ni moja ya vyombo vinavyolalamikiwa ambapo baadhi ya Askari wake wanajihusisha ni vitendo vya kuomba rushwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mh. Sophia Mjema aliwashukuru kwa uzalendo mkubwa walioufanya kuamua kuwa sehemu ya ujenzi wa Tanzania mpya chini ya Rais Magufuli. _*Amepiga marufuku vijana wa ulinzi shirikishi wa Tambaza kuacha kukamata bodaboda na badala yake kazi hiyo ifanywe na Jeshi la Polisi ambao ndiyo wenye taaluma ya ukamataji. Vile vile Mh. Mjema amemtaka Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Ilala kufanya uchunguzi wa tuhuma za rushwa kwa askari ambayo orodha yao ilitolewa kwa Mkuu wa Wilaya na kukabidhiwa kwa Kaimu Kamanda wa Polisi Ilala, kisha kuwachukuliwa hatua wale wataobainika na hatia*_.
Kuhusu kuwarasimisha bodaboda, Mkuu huyo wa Wilaya alisema kuwa, _*huu ni mpango uliopo kwenye Ilani ya CCM 2015/ 2020 wa kurasimisha shughuli mbalimbali zinazofanywa na wananchi hasa wanyonge ili watambulike rasmi, walipe kodi na wanufaike na fursa mbalimbali zinazotolewa na serikali. Hivyo, aliwaahidi kulichukua ombi hilo na kulifanyia kazi kwa kushirikiana na TRA, NIDA, SUMATRA, Polisi na wawakilishi wa bodaboda wenyewe ili kwa pamoja watafute mfumo mzuri wa kufanikisha jambo hili*_.
Mwisho aliwataka bodaboda hao kufuata sheria na taratibu, kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii ili kujiwekea akiba, kunufaika na mafao yatolewayo na kupata bima ya afya kwa ajili yao na familia zao.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala ndugu Edward Mpogolo aliwapongeza vijana hao kwa moyo wa uzalendo walioonesha kwa nchi yao na kwamba kama ilivyowezekana kwa wamachinga ambao kwa sasa mchakato wa kuwarasimisha unaendeleo, na wao pia chini ya uongozi wa Magufuli inawezekana.
Mara kadhaa wazungumzaji walilazimika kukatisha hotuba zao kwa shangwe na vifijo zilizokuwa zikioneshwa na vijana hawa huku wakinyanyua kofia zao juu kama ishara ya utii kwa Rais wao Mh. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Shughuli hii pia ilihudhuliwa na Viongozi wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Ilala, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala na Maafisa wengine wa serikali.
No comments:
Post a Comment