WANASAYANSI zaidi ya 400 kutoka nchi mbalimbali duniani wanatarajiwa kukutana nchini kujadiliana na kubadilishana ujuzi unaotokana na tafiti mbalimbali zinazohusu afya.
Wataalamu hao watakutana katika Kongamano la Tano la Kisayansi la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), litakalofanyika kwa siku mbili kuanzia Juni 29, mwaka huu jijini Dar es Salaam huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kongamano hilo, Makamu Mkuu wa Chuo wa MUHAS, Profesa Ephata Kaaya alisema katika kongamano Chuo hicho kitaeleza mafanikio ya tafiti na athari zake kwa upande wa kijamii na maendeleo ya uchumi.
“Katika Kongamano la Tano la Kisayansi, Chuo kitaonesha matokeo ya tafiti za hivi karibuni ya kisayansi kutoka miradi mbalimbali ya tafiti zinazotoka ndani na nje ya nchi katika miaka ya nyuma,” alisema.
Alisema baadhi ya matokeo ya tafiti zitakazowasilishwa ni pamoja na namna ugonjwa wa malaria unavyoweza kutokomezwa kwa kutumia njia mpya ya kufuatilia wagonjwa na kutoa dawa kwa watu walio katika hatari ya kupata maambukizi.
Tafiti nyingine ni maradhi ya figo na mengine yanayowakabili akinamama wakati wa kujifungua, pamoja na utoaji wa mafunzo ya chakuka na virutubisho kwa akina mama wenye watoto wadogo.
Alisema jambo la muhimu katika kongamano hilo ni jamii ya wanataaluma wa MUHAS kupata kushirikishana matokeo yao na kubadilishana mawazo na wataalamu pamoja na wadau wengine ndani na nje ya nchi, hatua inayolenga kuboresha afya ya jamii kupitia tafiti.
Alisema kaulimbiu ya mwaka huu: “Kutafsiri matokeo ya tafiti kwa vitendo ili kufikia maendeleo endelevu,” imechaguliwa mahususi ili kusisitiza umuhimu wa matumizi ya matokeo ya tafiti za kisayansi katika kuleta ufumbuzi wa matatizo ya kiafya, kimaendeleo na kijamii.
Alisema katika kongamano hilo, makala 122 zitawasilishwa kwa njia ya maongezi ambazo zitaangukia katika mada ndogo za utafiti wa msingi katika masuala ya afya, utafiti wa magonjwa yasiyoambukiza, tafiti za mifumo ya afya, afya ya mazingira, huduma za tiba, dawa za asili na tiba mbadala, teknolojia ya habari, mawasiliano pamoja na afya.
Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Elimu Endelevu na Maendeleo ya Kitaaluma, Dk Doreen Mloka alisema kongamano hilo litatoa fursa zaidi kwa wanasayansi chipukizi kuendeleza vipaji vyao.
No comments:
Post a Comment