Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo
Na Veronica Mheta, Arusha
MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Arusha, Catherine Magige amewaomba wananchi kumuunga mkono Rais John Magufuli kwa jitihada anazofanya kukabiliana na ufisadi huku Magige akikabidhi vitanda, magaodoro na shuka zilizotolewa na Rais kwa zahanati na vituo vya jijini Arusha.
Alitoa mwito huo wakati akizungumza katika Kituo cha Afya cha Levolosi mjini hapa alipokuwa anakabidhi msaada wa vitanda 25, magodoro 25 na shuka 25, vyote vikiwa na thamani ya Sh milioni 14.2 vilivyotolewa na Rais Magufuli kwa ajili ya vituo saba vya afya na zahanati tano za jijini humo.
Alisema inashangaza kuona baadhi ya watu wakibeza jitihada za Rais Magufuli kwa kuwakamata mafisadi pamoja na kuziba mianya ya rushwa, hivyo ni vema wananchi wenye nia njema kwa taifa wakaendelea kumuunga mkono ili kuwezesha kupatikana kwa maendeleo na huduma bora za kijamii.
“Naomba tumuunge mkono Rais wetu kwani anafanya jitihada mbalimbali za kusaidia wananchi ndio maana ametoa vitanda hivi na vitu vingine kusaidia jamii nami nimemuwakilisha na nawaomba wauguzi na madaktari kutoa huduma bora kwa wananchi,” alisema Magige.
Mganga Mkuu wa Jiji la Arusha, Dk Simon Chacha alisema msaada huo utawezesha kinamama na wagonjwa mbalimbali kupata huduma bora za afya. Chacha aliwatoa hofu wananchi akisisitiza kuwa endapo kutokuwa na malalamiko ya huduma mbovu za afya, waziwasilishe kwa viongozi wahusika ili wahusika wachukuliwe hatua.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Gabriel Daqqaro ametoa rai kwa wananchi kuendelea kuunga mkono jitihada hizo za Rais ili kupata maendeleo. Awali, Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Athumani Kihamia alisema vifaa hivyo vitagaiwa vituo vya afya vya Kaloleni, Levolosi, Themi, Ngarenaro, Terrat huku zahanati ambazo ni Olorieni, Terrat, Nasodoito, Elerai na Sombetini navyo vikipata mgao huo
No comments:
Post a Comment