Saturday, June 24, 2017

Mpango asisitiza ulipaji kodi

 Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango

 Na Anastazia Anyimike, Dodoma

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema ni lazima kama taifa, kujenga utaratibu wa kila mtu kulipa kodi. Amesisitiza kuwa ‘amechoka kuombaomba’ kwa niaba ya taifa ili kutekeleza miradi ya maendeleo.

Akizungumza wakati wa kujibu hoja zilizojitokeza wakati wa kujadili Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2017 yenye marekebisho ya sheria 15, Mpango alisema ili taifa kuweza kupata maendeleo ni vyema Watanzania kujenga utamaduni wa kulipa kodi.

“Naomba niliambie bunge kuwa ni lazima kama taifa tujenge utaratibu wa kila mtu kulipa kodi, ni lazima, na ni lazima tupate mahali pa kuanzia, tusidanganyane, kama tunatafuta fedha ya maji, za dawa, za kujenga barabara, ninasema ‘nimeshachoka kuomba’.

“Watanzania wanao uwezo wa kuchangia maendeleo kulingana na kipato chao, lakini kwa mwaka huu tunachofanya ni kuwatambua ili tuweze kuwapatia sehemu mwafaka za kufanya biashara zao hilo ndio jambo la misingi,” alisema
.
Alisema uamuzi wa kujenga Tanzania ya viwanda chini ya utawala wa Rais John Magufuli, unahitaji hatua za kijasiri katika ukusanyaji wa mapato na Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2017 ambao umetafsiri hatua hizo kisheria.

Awali, akiwasilisha maoni ya Kambi ya Upinzani kuhusiana na Muswada wa Sheria ya Fedha mwaka 2017, Naibu Waziri Kivuli wa Fedha na Mipango, David Silinde alisema hatua ya Serikali kuwatambua wafanyabiashara ndogo ni njia ya kuwakamua ili walipe kodi huku wakiacha vyanzo vya uhakika kama sekta ya madini.

Akijibu hoja ya adhabu za makosa ya barabarani ni kama chanzo kipya cha mapato kwa Serikali, Mpango alisema sio kweli kwamba fedha ambazo zinakusanywa na Jeshi la Polisi ni chanzo cha mapato.

Alisema adhabu inayotolewa kwa madereva ni kuhakikisha madereva wanafuata na kutekeleza bila shuruti sheria za usalama barabarani kwa mujibu wa sheria “Hivyo si kweli hata kidogo kwamba adhabu imehesabika kama chanzo cha mapato,” alisema.

Akijibu hoja ya kuwa serikali kuhamishia fedha za taasisi na mashirika ya umma kwenda Benki Kuu (BoT) inakiuka sheria, Mpango alisema sheria haijakiukwa na kuwa utekelezaji huo uko kwa mujibu wa sheria za BoT.

“Serikali haijakiuka na hii ni kwa mujibu wa Sheria ya BOT Kifungu cha 32 (1) ambacho kinataka taasisi na mashirika ya umma kuhifadhi fedha zao BOT,” alisema. Akiwasilisha maoni ya Kambi ya Upinzani, Silinde alisema hatua hiyo inaondoa dhana ya ushindani wa kibiashara kwa mabenki na kuitaka serikali kuweka mfumo wa kudhibiti mashirika yanayotumia vibaya fedha zake wanapoweka fedha kwenye mabenki ya kibiashara.

Aidha, Mpango alisisitiza kuwa uamuzi wa kuongeza Sh 40 kwenye mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa, si kuongeza mzigo kwa wananchi, bali una lengo la kuwalinda Watanzania dhidi ya uchakachuaji wa mafuta.

No comments:

Post a Comment