Rais wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli
RAIS Dk John Magufuli amemuagiza Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage kuwanyang’anya viwanda watu wote waliouziwa viwanda na Serikali na baadaye kuvitelekeza ili wapatiwe wawekezaji wengine wanaoweza kuviendeleza.
Aliyasema hayo juzi wakati akihitimisha ziara yake ya siku tatu katika mkoa wa Pwani. Alisema viwanda 197 viliuzwa kwa watu mbalimbali kwa lengo la kuviendeleza, lakini viwanda hivyo vimekufa na vingine kubadilishwa matumizi, jambo ambalo linarudisha nyuma juhudi za kutekeleza mpango wa ujenzi wa viwanda.
“Mheshimiwa Waziri, wale waliopewa viwanda miaka ile kwa kuuziwa bei ya chee, tukitegemea kwamba vile viwanda vitaendelea kufanya kazi, lakini wamevitelekeza na vingine havipo kabisa, usiwe na kigugumizi na wala usiangalie sura, wanyang’anye, wale wawekezaji wenye nia ya kujenga viwanda wapewe, kiwanda sio mwanamwali wa kumtunza ndani, kinatakiwa kifanye kazi kitoe ajira na Serikali ipate mapato,” alisema Rais Magufuli.
Alitoa agizo hilo baada ya kuweka jiwe la msingi la kiwanda cha kusindika matunda cha Sayona Fruits Ltd kilichopo katika Kijiji cha Mboga wilayani Bagamoyo, ambacho kikikamilika kitakuwa na uwezo wa kusindika tani 300 za matunda kwa siku, kuajiri wafanyakazi 800 na kitawanufaisha wakulima 30,000.
Kiwanda hicho kinajengwa na Mtanzania Subhash Patel kwa gharama ya zaidi ya Sh bilioni 120. Kabla ya kuweka jiwe la msingi la kiwanda hicho, Rais Magufuli alitembelea kiwanda cha kutengeneza dawa za viuadudu cha Kibaha ambacho kimejengwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na Cuba kwa gharama ya Dola za Marekani Milioni 22.3 kwa lengo la kuzalisha dawa za kuangamiza viluilui vya mbu na kutokomeza ugonjwa wa malaria.
Akiwa kiwandani hapo, Rais Magufuli aliiagiza Wizara ya Fedha na Mipango kutoa Sh bilioni 1.3 kwa ajili ya kununulia lita takribani 100,000 za viuadudu zilizokwama kiwandani hapo kutokana na halmashauri za majiji, manispaa, miji na wilaya kutozinunua.
Alielekeza kuwa halmashauri zote, zitakazopangwa kuchukua viuadudu hivyo, ziwe zimechukua kabla ya mwisho wa mwezi huu. “Hatuwezi kuwa tunaanzisha viwanda kama hiki cha dawa halafu hatuvitumii, kinazalisha dawa wanatumia watu wa nchi zingine wakati sisi tunaendelea kufa kwa malaria,” alisisitiza Rais Magufuli.
Katika siku hiyo ya mwisho ya ziara yake, Rais Magufuli pia alizindua barabara ya Bagamoyo – Makofia – Msata yenye urefu wa kilometa 64. Aliipongeza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na wote waliofanikisha ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami, akisema itatatua tatizo la msongamano wa magari katika barabara ya Chalinze – Dar es Salaam na inapita katika eneo la Bagamoyo, ambalo litajengwa bandari mpya na eneo la viwanda.
Ujenzi wa barabara hiyo yenye madaraja makubwa matatu, umegharimu Sh bilioni 213 ikiwa ni fedha zilizotolewa na Serikali ya Tanzania. Rais Magufuli pia alizindua kiwanda cha kukausha matunda cha Elven Agri Company Ltd kilichopo Kijiji cha Mapinga, Bagamoyo, ambacho kina uwezo wa kukausha tani 60,000 za matunda kwa mwaka na kimewekezwa na mwekezaji Mtanzania kwa gharama ya takribani Sh bilioni 26.4.
Akiwa kiwandani hapo, Rais Magufuli alisema Serikali yake haitatoa fidia kwa watu ambao wanadai kulipwa fidia kutokana na maeneo yao kuchukuliwa ili kupisha mradi wa ujenzi wa eneo la bandari na viwanda la Bagamoyo. Aliagiza watu waliofanya njama za kulipwa fidia wakati hawakustahili fidia hizo, warudishe fedha mara moja kabla hatua za kisheria hazijaanza kuchukuliwa dhidi yao.
No comments:
Post a Comment