MWAKILISHI katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Said Soud Saidi wa chama cha AFP
MWAKILISHI katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Said Soud Saidi wa chama cha AFP aliyeteuliwa na Rais, Dk Ali Mohammed Shein amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitakuwa na kazi rahisi ya kushinda katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, kwa kuwa kinatekeleza na kusimamia ilani ya uchaguzi bila porojo.
Soud alisema hayo wakati akichangia hoja mbalimbali za wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, ambazo zinatokana na utekelezaji wa ilani ya uchaguzi na ahadi kwa viongozi kwenda kwa wapiga kura katika kipindi cha harakati za uchaguzi mkuu.
Huku akionesha kitabu cha Ilani ya uchaguzi ya CCM, alisema kwa asilimia kubwa mambo mengi ambayo yameahidiwa na viongozi wakuu ambao walipita kila sehemu kuinadi ilani hiyo, yametekelezwa kwa vitendo.
Alitoa mfano kuwa, Rais Shein ametekeleza ahadi zake nyingi alizozinadi kwa wapigakura, tena ndani ya kipindi kifupi cha mwaka mmoja na nusu tangu alipoingia madarakani. Alisema vyama vingi vya siasa nchini, ilani zake ni za ubabaishaji tu huku wengine wakiwa na ndoto za mchana za kuifanya Zanzibar kuwa Singapore ya Afrika, lakini ukimuuliza kwa njia zipi na mikakati ipi, hawezi kukwambia.
Alisema yeye hawezi kupata usingizi kwa kulala bila ya kuipitia Ilani ya uchaguzi ya CCM, ambayo ni ukweli uliodhihiri imetayarishwa kitaalamu kutokana na mahitaji yanayokwenda na wakati.
“Mheshimiwa Spika tuwe wakweli vipo vyama hapa vya siasa vilikuwa vikinadi ilani yake kwa kuigeuza Zanzibar kuwa Singapore ya Afrika lakini ukiwauliza kwa njia zipi hawakujibu... hawa CCM mikakati yao inakubalika kwa sababu unaona kila siku mabadiliko makubwa,” alisema.
Aliyataja mambo ambayo yamefanikiwa kusimamiwa katika ilani ya uchaguzi ni kuwawezesha wazee waliofikia umri wa miaka 70, kupata pensheni jamii na hivyo kupunguza ukali wa maisha.
Alisema ni nchi chache sana duniani pamoja na bara la Afrika, zilizofanikiwa kulipa pensheni ya aina hiyo kwa wazee waliofikisha umri wa miaka 70.
No comments:
Post a Comment