Tuesday, January 17, 2017

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU HALI YA CHAKULA





Mhe.  Dr. Charles John Tizeba (MB)
Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi

         1.0    UTANGULIZI
 
Hadi kufikia katikati ya  mwezi Januari, 2017 hali ya chakula na upatikanaji wa chakula hapa nchini inaonyesha kuwa bado ni ya kuridhisha na hasa upatikanaji wa vyakula kama mchele na maharage ikilinganishwa na zao la mahindi. Pamoja na hali hii bei za baadhi ya vyakula zimeanza kupanda kufuatia mazao kidogo kuingia sokoni kwa wakati huu kunakochangiwa na mwenendo usioridhisha wa unyeshaji wa mvua za vuli na kuchelewa kuanza kunyesha kwa mvua za msimu katika maeneo mengi ya nchi.
2.0   HALI YA MAZAO MASHAMBANI
Hali ya mazao mashambani kutoka mikoa mbalimbali katika kipindi cha mwezi Desemba, 2016, inaonyesha kutoridhisha katika baadhi ya maeneo kutokana na uhaba wa mvua na mtawanyiko usioridhisha. Hata hivyo maeneo mengi ya nchi yamekuwa yakiendelea na uandaaji wa mashamba, kupanda, kupalilia na usambazaji wa pembejeo za kilimo. Kutokana na uhaba wa mvua na kuwa na mtawanyiko usioridhisha, hali ya unyevunyevu katika udongo si ya kuridhisha kwa ustawishaji wa mazao ya kilimo yanayohitaji maji mengi. 

Taarifa ya hali ya upatikanaji wa mvua kutoka mikoa inayopata mvua za vuli, zinaonyesha kuwa kwa ujumla mvua zimechelewa kuanza na zimenyesha katika kiwango cha wastani na chini ya wastani zikiwa na mtawanyiko usioridhisha.  Mikoa ya Kagera, Mwanza, Geita, Kilimanjaro, Arusha, Mara, Pwani, Tanga, Morogoro pamoja na sehemu ya mkoa wa Shinyanga na Simiyu na zilipoanza kunyesha zilikuwa chini ya wastani. Mazao yaliyopandwa katika baadhi ya maeneo hayo yameathirika kutokana na ukame uliojitokeza ukiwamo mkoa wa Kagera wilaya za Kyerwa, Missenyi na Karagwe. Mikoa iliyobakia mvua zimeanza kunyesha ingawa mtawanyiko wake sio wa kuridhisha.

3.0   HALI YA UPATIKANAJI CHAKULA KATIKA MIKOA
 
Kulingana na taarifa kutoka mikoani hali ya upatikanaji wa chakula katika masoko yaliopo katika halmashauri zote za mikoa unaridhisha isipokuwa bei ya mahindi imepanda ikilinganishwa na mwaka 2016 kipindi kama hiki. Hii inatokana na kutoingia sokoni kwa mazao mapya ya msimu wa mvua za vuli. Maeneo yaliyotolewa taarifa kuwa na uhaba mengi ni yale yaliyoonekana wakati wa tathmini ya awali ya uzalishaji msimu wa 2015/2016. Maeneo yaliyoongezeka ni kutoka katika mikoa ya Geita, Tabora na Kagera. Pamoja na kuwa mvua za vuli hazijanyesha vizuri na hivyo kutokuwepo kwa mazao mapya sokoni, mikoa bado imeonyesha kuwa na ziada ya chakula. Takwimu katika Kiambatisho hiki, kwa mazao yasiyonafaka hazijabadilishwa katika mlinganisho wa nafaka (Grain equivalent). Aidha, Mikoa  yenye kivuli taarifa zake ni za mwezi Novemba 2016 na baadhi ya mikoa takwimu zake zimetolewa katika mfumo wa wanga na zimeonyeshwa katika kipengele cha nafaka.

4.0   HALI YA UNUNUZI NA HIFADHI YA CHAKULA
Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kwa mwaka wa fedha 2016/2017 umepanga kununua jumla ya tani 100,000 za chakula. Hadi kufikia tarehe 8 Januari, 2017, Wakala umenunua jumla ya tani 62,087.997 za mahindi sawa na asilimia 62 ya lengo ililojiwekea. Kati ya kiasi hicho, tani 38,162.280 zimenunuliwa kupitia vituo vya ununuzi na tani 23,925.717 kupitia vikundi vya wakulima. Aidha, hadi kufikia tarehe 12 Januari, 2017 Wakala una akiba ya tani 88,152.443 za mahindi.

5.0   TATHMINI YA KINA YA HALI YA CHAKULA NA LISHE
Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, FAO, TFNC pamoja na  Wadau wengine wanaendelea kufanya tathmini ya kina ya hali ya chakula na Lishe nchini katika kipindi hiki. Tathmini inatarajiwa kukamilika tarehe 28 Januari, 2017 na itazihusisha Halmashauri 55 zenye maeneo yenye uhaba wa chakula ili kubaini kaya zilizoathirika na uhaba wa chakula na mahitaji yao. Tathmini hiyo inayosimamiwa na kuratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, itaiwezesha Serikali kupata taarifa za uhakika zaidi kuhusu hali ya chakula na lishe, hasa katika maeneo ambayo yalionekana kuwa na upungufu katika tathmini ya awali na yale yaliyojitokeza mara baada ya kufanya tathmini .

6.0   MWENENDO WA BEI ZA MAZAO YA CHAKULA
Serikali inaendelea kufuatilia mwenendo wa bei za mazao ya chakula hususan Mahindi na Mchele ili kujiridhisha uwepo wake na upatikanaji wake sokoni. Mwenendo wa bei za mazao haya sokoni kwa kipindi cha mwezi Desemba, 2016 kutoka kwenye masoko 13 kati ya 25 ya miji mikuu hapa nchini umekuwa ukipanda na kushuka kutokana na sababu mbalimbali. 

Bei za Mahindi, Mchele na Maharage

Bei ya wastani ya mahindi katika msimu wa chakula na soko kwa mwaka 2016/2017 imekuwa na mwelekeo wa kupanda kuanzia mwanzo wa mwezi Julai, 2016. Bei hii iko juu ikilinganishwa na bei katika kipindi kama hicho mwaka 2015/16. Katika kipindi cha mwezi Desemba 2016, bei ya mahindi kwa gunia la kilo 100 imepanda na kufikia wastani wa shilingi 84,577.00 ikilinganishwa na Desemba 2015 ambapo gunia la kilo 100 liliuzwa kwa wastani wa shilingi 65,104.00.

Kwa upande wa mchele bei ina mwelekeo wa kushuka ambapo bei ya wastani kwa mwezi Desemba 2016 kwa gunia la kilo 100 ilikuwa shilingi 151,957.00 ikilinganishwa na kipindi kama hiki mwaka 2015 ambapo gunia liliuzwa kwa shilingi 176,237.00. Bei ya maharage inaonyesha kushuka kidogo kutoka wastani wa shilingi 172,852.00 mwezi Desemba 2015 na kufikia wastani wa shilingi 171,251.00 mwezi Desemba 2016.

Kupanda na kushuka kwa bei kwa kipindi kama hiki ni jambo la kawaida kwani mwanzo wa msimu hakuna mazao yanayoingia sokoni na hivyo hupelekea bei kupanda na mwanzo wa mavuno bei hushuka kutokana na mazao mengi kuingia sokoni. Aidha hali ya mwenendo usioridhisha wa unyeshaji wa mvua za vuli na za msimu kwa kipindi cha 2016/17 kwa ajili ya upatikanaji wa chakula kwa mwaka 2017/18 katika maeneo mengi ya nchi, imechangia wafanyabiashara wa nafaka nchini na hasa zao la mahindi kuingiza zao hili kidogo kidogo sokoni, hivyo kuongeza kasi ya uhitaji kutoka kwa wananchi na kusababisha bei kuzidi kupanda. 

Hali halisi ya mwenendo wa bei katika masoko, unaonyesha kuwa bei ya juu kabisa ya mahindi imeonekana katika soko la Lindi ambapo gunia la kilo 100 liliuzwa kwa wastani wa shilingi 150,000.00 wakati bei ya juu ya mchele pia imeonekana katika soko la Lindi ambapo gunia la kilo 100 liliuzwa kwa wastani wa shilingi 245,000.00 na bei ya juu kabisa kwa maharage imeonekana katika soko la Lindi ambapo gunia la kilo 100 liliuzwa kwa wastani wa shilingi 243,333.00. Bei ya chini kwa mahindi ilionekana katika soko la Mbeya ambapo gunia liliuzwa shilingi 62,600.00. Mchele bei ya chini ilionekana katika soko la Geita ambapo gunia liliuzwa kwa wastani wa shilingi 99,000.00 na maharage bei ya chini yaliuzwa kwa shilingi 136,400.00 katika soko la Mbeya.

7.0   HITIMISHO

Serikali itaendelea kufuatilia mwenendo wa uzalishaji na upatikanaji wa chakula hapa nchini. Pale itakapobainika kuwa kuna uhitaji wa chakula, Serikali itachukua hatua stahiki. Wafanyabiashara wanahamasishwa kununua mazao ya chakula katika maeneo yaliyo na ziada na kuweza kuyauza katika maeneo yenye uhaba. Serikali itaendelea kuhimiza kusindika mazao ya chakula kwa kuyaongezea thamani na kuyauza katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Kutokana na hali ya mwenendo wa unyeshaji wa mvua za vuli na msimu kutokuridhisha katika maeneo mengi ya nchi Serikali inapenda kutoa ushauri kwa wakulima kutumia mbegu zinazokomaa mapema na kupanda mazao yanayostahimili ukame. Wakulima wanashauriwa kutumia kwa uangalifu na kuhifadhi akiba ya chakula cha kutosha kwa matumizi katika kaya. Sekta binafsi inahamasishwa kuendelea kushiriki katika kutoa masoko ya kununua na kuuza mazao katika maeneo yenye ziada na kuyauza katika maeneo yenye uhaba.
Mhe.  Dr. Charles John Tizeba (MB)
Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi
16 Januari 2017

No comments:

Post a Comment