Thursday, October 27, 2016

SERIKALI:KUELEKEA MABADILIKO YA UENDESHWAJI WA VILABU VYA SIMBA NA YANGA MICHAKATO ILIYOKUWA IKENDELEA MARUFUKU

kiganja
Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT) Mohamed Kiganja.

Na.Alex Mathias,Dar es salaam

Baraza la Michezo la Taifa limeagiza michakato yote inayoendelea kubadilisha umiliki wa timu kutoka kwa Wanachama kwenda kwenye umiliki wa hisa na ukodishwaji kwa vilabu vyote vya michezo usitishwe mara moja hadi marekebisho ya katiba zao kwa mujibu wa sheria ya Baraza la Michezo la Taifa na kanuni za Msajili Namba 442 kanuni ya 11 ya kifungo kidogo cha 1-9 yatakapofanyika.

Akizungumza na waandishi wa Habari Katibu Mkuu wa BMT Mohamed Kiganja, amesema kuwa baraza linapenda kuona kwamba wahusika wakuu wa jambo hilo hasa klabu za Simba na Yanga wanafuata sheria na taratibu za nchi katika kufikia malengo yao.

Aidha amesema kuwa endapo vilabu hivyo kama vitaendelea na mchakato huo kabla ya taratibu za kurekebisha katiba zao kisheria ni kosa na hatua stahiki zitachukuliwa dhidi ya watakaokiuka maelezo hayo.

“Hivi karibuni imeibuka michakato ya watu wakitaka kubadilisha umiliki wa vilabu vya wanachama na kuvielekeza kwenye utaratibu wa hisa na ukodishwaji,vitendo hivi vimesababisha migogoro mikubwa ambayo inaashiria uvunjifu wa amani ndani ya tasnia ya michezo kwani imefikia hatua watu wanaenda mahakamani mfano mzuri ndani ya klabu ya Yanga”alisema Kiganja.

Ameongeza kuwa makundi ya wapenzi na wanachama wamejikita katika mijadala ambayo hatma yake ni kuzidi kuibomoa jamii badala ya kuijenga na kuimalisha michezo nchini.

Aidha amesema kuwa kuna mipasuko ambao umepelekea baadhi ya wanachama wameona kuwa hawaridhishwi na mwenendo mzima na pengine hata taratibu za suluhu zilikiukwa na kuona hazifai na kuamua kukimbilia Mahakamani.

“Kutokana na hali hiyo BMT kama chombo pekee cha kisheria kilichopewa dhamana ya kusimamia Michezo nchini,hakiwezi kuvumilia ukiukwaji wa Sheria na taratibu zinazoendelea na kuashiria kutoweka kwa amani kwenye tasnia ya Michezo”alisema Kiganja.Hivyo basi,Baraza linasitisha michakato yote inayoendelea ya kutaka kubadilisha umiliki wa timu kutoka kwenye mfumo ulipo sasa na ni vyema vilabu vikaendelea kubaki kuwa mali ya Wanachama.

“Kama kuna mdau yeyote ambaye ana nia ya kumiliki klabu ya Mchezo wowote ule ni vyema akaanzisha timu yake kama bwana Said Salim Bhakhresa alivyoamua kuanzisha klabu ya Azam FC”alisema Kiganja.

No comments:

Post a Comment