MAJAJI wa Mahakama Kuu nchini wametakiwa kufanya kazi yao kwa
kuzingatia maadili ya taaluma hiyo wakati wote, kwa kuwa watanzania
wanategemea kutendewa haki na kwa wakati mahakamani.
Akifungua Mkutano wa Majaji Wafawidhi na Majaji Waliosikiliza Kesi za
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, unaotathmini usikilizwaji wa kesi hizo
jijini Arusha jana, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Ferdinand
Wambali alisema watanzania wana imani na mahakama, hivyo ni muhimu kwa
majaji hao kutenda haki wakati wote.
Alisema majaji hao wamekutana ili waweze kupata nafasi ya kujadili
changamoto mbalimbali, zilizojitokeza wakati wa kusikiliza kesi
zilizohusu uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na kubadilishana mawazo namna ya
kuzimaliza kwa haraka kesi zinazohusu uchaguzi kwa siku za mbele.
Jaji Wambali alisema jumla ya kesi 53 za ubunge, zilizotokana na
uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, zilifunguliwa katika Mahakama Kuu Kanda za
Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Mbeya, Moshi, Mtwara na Mwanza. Kanda
nyingine ni Shinyanga, Songea, Sumbawanga na Tanga.
Jaji Wambali alisema kati ya kesi hizo, kesi 31 zilimalizika katika
hatua za awali na kesi 22 ziliendelea. Mpaka sasa kesi 19 zimemalizika
na kuongeza kuwa kesi tatu bado ziko mahakamani.
Alieleza kuwa ni jambo la kujivunia kwa Mahakama ya Tanzania, kwa
kuwa kesi zote 196 zilizotokana na uchaguzi wa madiwani zilimalizika
mapema katika mahakama mbalimbali za Hakimu Mkazi nchini.
Alisema katika kipindi cha mwaka mmoja tangu kufanyika kwa Uchaguzi
Mkuu nchini, zaidi ya asilimia 94 ya kesi za uchaguzi zilizofunguliwa
kwenye Mahakama Kuu, zimemalizika wakati asilimia 100 ya kesi zote za
udiwani zimemalizika.
Jaji Kiongozi aliwapongeza majaji na mahakimu wote, kwa kumaliza kesi
kwa ufanisi na kwa wakati, licha ya changamoto mbalimbali wanazozipitia
watumishi hao wa mahakama wakati wanaposikiliza kesi zinazotokana na
uchaguzi.
Aidha, Jaji Wambali alilishukuru Shirika la Maendeleo la Umoja wa
Mataifa (UNDP) kwa kufadhili mafunzo mbalimbali ya majaji na mahakimu,
yaliyotolewa kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. Mkutano wa
siku nne wa Majaji Wafawidhi pamoja na Majaji waliosikiliza kesi za
uchaguzi, ulianza jana jijini Arusha na umefadhiliwa na shirika hilo.
No comments:
Post a Comment