MICHEZO sita ya Ligi Kuu Tanzania Bara inatarajiwa kuunguruma leo katika viwanja tofauti nchini.
Yanga itakuwa kwenye Uwanja wa Kaitaba dhidi ya Kagera Sugar, Azam FC
itakuwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi ikiwakaribisha maafande
wa JKT Ruvu. Yanga inasaka nafasi ya kuwa karibu na vinara wa ligi Simba
inayoongoza kileleni kwa pointi 26. Kwa vyovyote vile, ni lazima
ipambane kama kweli inahitaji kuwa karibu.
Timu hiyo inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo ikiwa na pointi 18
nyuma ya Stand United yenye pointi 20 na Simba 26. Tofauti yake na
anayeongoza ni pointi nane. Yanga tayari imeshacheza michezo tisa,
imeshinda mitano, sare tatu, na kupoteza mmoja. Mabingwa hao watetezi
iwapo watashinda mchezo huo watafikisha pointi 21.
Ikiwa wataruhusu kufungwa basi watakuwa kwenye uwezekano wa kushuka
katika nafasi ya tatu, kwani walioko nyuma yake wakishinda watapanda
juu. Kagera Sugar sio timu ya kubeza, kwani chini ya Kocha Mecky Maxime
imekuwa ikijitahidi kufanya vyema.
Huenda ukawa mchezo mgumu kwa kuwa kila mmoja atakuwa anahitaji
matokeo mazuri, Kagera ikitaka kushinda kuendelea kubaki nne bora, na
Yanga ikitaka ushindi ili kusudi kuwa karibu na wapinzani. Kagera Sugar
imeshacheza michezo 11, ikishinda mitano, ikipata sare tatu na kupoteza
mitatu ikishika nafasi ya nne kwa pointi 18 sawa na Yanga.
Mchezo mwingine ni Azam FC dhidi ya JKT Ruvu. Timu hii imeshacheza
michezo 10, imeshinda mitatu, imepata sare nne, imepoteza mitatu hivyo,
ina pointi 13 ikishika nafasi ya nane. Timu hiyo imekuwa haina mwenendo
mzuri tangu kuanza kwa Ligi Kuu Tanzania bara. Inacheza na JKT Ruvu
ambayo iko hatarini kushuka daraja kwani pia, haiko vizuri.
JKT Ruvu imeshacheza michezo 10, imeshinda mmoja, imepata sare sita,
imepoteza mitatu na kufikisha pointi tisa. Hautakuwa mchezo mrahisi kwa
kila mmoja, kwa vile wote huhitaji matokeo mazuri kuwa sehemu nzuri.
Mtibwa Sugar itawakaribisha Stand United kwenye uwanja wa Manungu,
mkoani Morogoro.
Mtibwa Sugar imecheza michezo 11, imeshinda minne, sare nne,
imepoteza mitatu na kufikisha pointi 16. Stand United inashika nafasi ya
pili ikiwa na pointi 20 baada ya kucheza michezo 11, imeshinda mitano,
sare tano na kupoteza mmoja. Hautakuwa mchezo mrahisi kwa kila mmoja,
zote ni timu nzuri na zinahitaji matokeo. Majimaji itaikaribisha Ruvu
Shooting.
Timu hiyo ambayo bado iko kwenye hatari ya kushuka daraja imekuwa
ikijitahidi katika michezo iliyopita na kufanya vizuri. Tayari imeshinda
michezo miwili, katika 11 iliyocheza na kufikisha pointi tisa. African
Lyon itakuwa mwenyeji wa Mbeya City. Imetoka kufungwa na Majimaji hivyo,
huenda ikalipiza kisasi kwa Mbeya.
Iwapo itashindwa kujitahidi kupata matokeo itaendelea kushuka.
Imefikisha pointi 10 katika michezo 11. Ndanda inaikaribisha Mwadui FC
kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona. Timu hizo zimetofautiana kwa pointi
tatu. Ndanda inashika nafasi 10 kwa pointi 13 na Mwadui ya 12 kwa pointi
10. Ushindi kwa kila mmoja ni muhimu.
No comments:
Post a Comment