Saturday, October 22, 2016

Kamati yamchachafya naibu waziri

NAIBU Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani na baadhi ya watendaji wa wizara hiyo, jana walinusurika kutimuliwa nje ya kikao cha Kamati ya Nishati na Madini, baada ya kuwasilisha taarifa isiyoendana na maagizo yaliyotolewa na kamati hiyo.

Wajumbe hao waligeuka mbogo mbele ya waziri na watendaji hao baada ya Kaimu Kamishna wa Nishati na Petroli, James Andilile kuwasilisha taarifa hiyo inayohusu changamoto zinazowakabili wadau wa mafuta.

Mara baada ya kuwasilishwa kwa taarifa hiyo, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Doto Biteko, alimtaka Waziri huyo na watendaji watoke nje wawajadili kwanza kutokana na kutoa taarifa isiyo na majibu yaliyoagizwa na kamati hiyo.

Baada ya kurejea ndani ya kikao hicho, mjadala wa kujadili taarifa hiyo uliendelea ingawa wajumbe wa kamati hiyo, walisisitiza kutoridhishwa na majibu ya taarifa hiyo.

Mbunge wa Biharamulo Magharibi, Oscar Mukasa, alionesha kusikitishwa na kitendo cha watendaji hao kuja na majibu yasiyojitosheleza katika masuala muhimu kama hayo ya vinasaba na mengineyo.

“Tunataka kupata maelezo ya kina kuhusu mambo haya ya changamoto za mafuta kwa wadau, sasa tunaomba iwe mwisho kwa watendaji wa wizara kukiuka maagizo yanayotolewa na kamati,” alisisitiza na kuongeza kuwa, dharau iliyooneshwa na watendaji imewakwaza wajumbe wa kamati hiyo.

Mbunge wa Kilombero, Suzan Kiwanga, alisema jambo hilo walijadili kwa kina kikao kilichopita na kutoa maagizo kwa watendaji hao, lakini cha kushangaza jana waliingia na kudai hawakuelewa maelekezo ya kamati jambo linaloonekana kama ni utani mbele ya kamati hiyo.

“Nawauliza mlipokuja na taarifa hii hapa mlikuwa mnatutania sisi? Msituletee utani na mambo ya ajabu ajabu tutakuja kuelewana vibaya, mnatuita wadau, sisi ni wadau wenu nyie, mnataka tumpelekee spika taarifa gani,” alihoji Kiwanga. Alifafanua kuwa maagizo yote yalitolewa katika kikao kilichopita ambapo walijadili mambo mengi yakiwemo masuala ya vinasaba, tozo na mengine mengi. “Shukuruni busara za mwenyekiti, la sivyo leo tulikuwa tunawatimulia mbali, hapa tunazungumza na wataalamu….kama hamtoshi kwenye nafasi zenu muondoke,” alisema.

Mbunge wa Mkinga, Dustan Kitandula, alisema anashukuru kuona jambo walilolisubiri kwa muda mrefu, la Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati, Maji na Mafuta (Ewura), kuingizwa na kuwa chini ya Wizara ya Nishati na Madini limefanikiwa kwani sasa muundo huo utamaliza malalamiko yote yaliyopo.

Awali, katika taarifa yake, Andilile alibainisha changamoto mbalimbali zinazowakabili wadau katika sekta ya mafuta kuwa ni vituo vya mafuta takribani 1,364 kujengwa mjini na si vijijini hali inayohatarisha maisha ya wananchi wa vijijini ambao hununua mafuta hayo kwa chupa.

Alisema changamoto nyingine ni ushiriki wa kampuni za ndani katika kuagiza mafuta ya pamoja na kuongeza maeneo ya hifadhi ya mafuta hadi mikoani kwani kwa sasa asilimia 80 ya hifadhi ya mafuta iko Dar es Salaam.

Dk Kalemani akijibu hoja hizo alisema amepokea malalamiko hayo na kuahidi kuyafanyia kazi, lakini pia aliomba wapewe muda mpaka jumanne ili wawasilishe taarifa hiyo, hoja ambayo ilipokelewa na kuridhiwa na kamati hiyo.

No comments:

Post a Comment