MKUU wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Rais mstaafu Jakaya Kikwete
amekitaka chuo kikuu hicho (UDSM) kilinde hadhi yake ya kuendelea kuwa
kiongozi katika utoaji wa elimu bora, ambayo itasaidia taifa kuwa na
wataalamu wenye kusaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili
kijamii.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya miaka 55 ya Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam jana, Kikwete alisema hatua ya chuo hicho kufikisha umri huo
ni wazi kuwa kimekomaa na kimetoka katika hatua mojawapo ya makuzi na
kwenda nyingine, hivyo kinastahili kuwa chachu ya maendeleo kwa kutoa
wahitimu wenye kuleta mabadiliko katika nchi.
Kikwete ambaye aliteuliwa hivi karibuni kuwa mkuu wa chuo hicho,
alisema licha ya chuo hicho kutoa mchango mkubwa kwa nchi ikiwa ni
pamoja na kutoa viongozi wa nchi na wataalamu ambao wamekuwa msaada
mkubwa katika kutunga sera za nchi, kinatakiwa kutoa wahitimu ambao
wanakidhi soko la ajira.
"Nawasihi mafanikio ambayo mmeyapata kwa miaka 55, endeleeni kuwa
kitovu cha kutoa elimu bora, Chuo Kikuu cha Dar es Salam kiongoze
wengine wafuate," alisema Rais Kikwete ambaye pia ni miongoni mwa
wahitimu waliosoma chuoni hapo katika miaka ya 1970.
Alitoa mwito kwa uongozi wa chuo hicho kuhakikisha wanakuja na mambo
mapya ya maendeleo ya kukijenga chuo hicho na sio mambo mapya ya kubomoa
mambo mazuri ya maendeleo ambayo yamepatikana chuoni hapo miaka ya
nyuma.
Akizungumzia uongozi wake kama mkuu wa chuo, alisema mara tu baada ya
kuteuliwa kuwa mkuu wa chuo, alichofanya ni kukutana na wadau
mbalimbali wa ndani na nje ya chuo ili kujua matatizo yanayokikabili
chuo hicho na namna ya kutatua changamoto hizo.
Alisema licha ya kuelezwa changamoto nyingi, ikiwemo ukosefu wa
hosteli kwa wanafunzi, alichofanya ni kukutana na Rais John Magufuli
kumwelezea changamoto hizo ambazo zinahitaji msaada wa serikali na ndio
maana Rais alienda kuzindua ujenzi wa hosteli chuoni hapo. Aliahidi
kushirikiana na Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kushughulikia
kero mbalimbali zinazokikabili chuo hicho.
"Nitatumia uwezo wangu wote kuhakikisha tunapunguza kero hizo kwa manufaa ya chuo hiki,” alieleza Kikwete.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza
Mukandala alitaja changamoto zinazokikabili chuo hicho kuwa ni pamoja na
ufinyu wa bajeti ambao umesababisha kuwa kikwazo cha ujenzi na
ukarabati wa miundombinu ya chuo hicho pamoja na kukwamisha shughuli za
utafiti.
Pia alisema chuo hicho kinakabiliwa na uhaba wa maabara, ofisi na
uhaba wa hosteli za wanafunzi na nyumba za wafanyakazi. Changamoto
nyingine aliyoitaja ni uhaba wa wahadhiri wenye uzoefu katika fani
mbalimbali.
"Tunaishukuru serikali na wahisani mbalimbali kwa kuendelea
kushughulikia changamoto hizo, baadhi ya vyumba vikubwa vya mihadhara
vimejengwa pamoja na maabara. Pia tunashukuru uamuzi wa serikali kuamua
kujenga hosteli yenye uwezo wa kubeba wanafunzi 4,000,” alisema Profesa
Mukandala.
Profesa Tade Aina kutoka Chuo Kikuu cha Lagos, Nigeria ambaye ndiye
aliyetoa mhadhara maalumu wa Mkuu wa Chuo katika mada yake
iliyozungumzia taasisi za elimu ya juu za Afrika, alishauri vyuo vya
afrika vitoe elimu inayoendana na mahitaji ya taifa na bara la Afrika.
No comments:
Post a Comment