YANGA jana imerejesha furaha kwa mashabiki wake baada ya kushinda
mabao 3-0 dhidi ya Majimaji katika mechi ya Ligi Kuu iliyochezwa kwenye
Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam.
Mabingwa hao watetezi wa ligi hiyo wamepata ushindi jana baada ya
kutoka sare ya bila kufungana katika mechi dhidi ya Ndanda iliyochezwa
Mtwara, Jumatano ya wiki hii.
Yanga ilipata bao la kuongoza katika dakika ya 20, likifungwa na Deus
Kaseke aliyeuwahi mpira wa penalti iliyopigwa na Simon Msuva.
Awali, mwamuzi wa mechi hiyo Emmanuel Mwandebwa wa Arusha alitoa
penalti kwa Yanga baada ya mchezaji wa Majimaji kushika mpira eneo la
hatari na ndipo Msuva alipopiga penalti mara ya kwanza, lakini mwamuzi
alimtaka kurudia tena akidai alikosea, akaipiga mara ya pili ikaamuliwa
kurudia tena, akapiga mara ya tatu mpira ukagonga mwamba na ndipo Kaseke
alipouwahi na kuujaza wavuni.
Kipindi cha kwanza kiliisha kwa Yanga kuongoza kwa bao 1-0. Katika
kipindi hicho, Yanga walitengeneza nafasi nyingi lakini walishindwa
kuzitumia huku Majimaji wakicheza kwa kuzuia zaidi. Amisi Tambwe
aliifungia Yanga bao la pili dakika ya 81 kwa kichwa, ikiwa ni baada ya
kufunga katika dakika ya 74 na mwamuzi kulikataa akidai mfungaji
aliotea.
Dakika tano baadaye, Tambwe aliongeza bao la tatu kwa pasi ya Juma
Mahadhi. Kutoka kwenye uwanja wa Sokoine Mbeya, Azam jana iliendelea
kuzoa pointi kwenye uwanja huo baada ya kuifunga Mbeya City mabao 2-1.
Kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona, Ndanda ilitoka sare ya bila
kufungana na Kagera Sugar.
Huku kwenye uwanja wa Mwadui Shinyanga, Mwadui imetoka sare ya mabao
2-2 na Stand United. Katika uwanja wa Mabatini Mlandizi, Ruvu Shooting
iliitambia JKT Ruvu kwa kuifunga bao 1-0. Ligi hiyo inaendelea tena leo
kwenye uwanja wa Uhuru ambapo Simba itaikaribisha Mtibwa Sugar ya
Manungu, Turiani.
Mechi hiyo inatarajiwa kuwa kali na ya vuta nikuvute kutokana na timu
hizo kutambiana kwa zamu kila zinapokutana. Timu hizo zinakutana zikiwa
na makocha wapya Joseph Omog wa Simba na Salum Mayanga wa Mtibwa na
wote wakionesha kuwa wanalitaka taji kulingana na ubora wa vikosi vyao.
Mtibwa Sugar inapokutana na Simba au Yanga ni wazi kuwa hucheza kwa kukamia, lakini mwisho wa siku mmojawapo huibuka na ushindi.
Msimu uliopita timu hizi zilikutana raundi ya kwanza Januari 16,
mwaka huu Simba ikaibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mchezo uliochezwa
kwenye Uwanja wa Taifa, pia ilipokutana katika raundi ya pili Mei 15,
mwaka huu bado Simba ilishinda bao 1-0.
No comments:
Post a Comment