SERIKALI imeagiza Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti mkuu wa hesabu za
Serikali ‘CAG’ kufanya ukaguzi wa Rasilimali watu na fedha katika
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ili kupunguza minong’ono ya wizi wa
fedha.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Nape Nnauye, alipofanya ziara ya kikazi katika ofisi za
shirikisho hilo jana, ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu ateuliwe kuwa
Waziri.
“Sheria inamruhusu Msajili wa Vyama vya Michezo na Baraza la Michezo
(BMT) kukagua mali na hesabu hivyo nimewaagiza mkaguzi mkuu wa hesabu za
serikali ili aje kufanya ukaguzi wa mali za TFFm ikiwemo rasilimali
watu na hesabu zote,” alisema Nape.
Pia Nape alisema ukaguzi ukishafanyika utaondoa dhana potofu ambayo
imejijenga kwa baadhi ya watu kuwa fedha zinazotoka Shirikisho la Soka
la Kimataifa (FIFA) na zile zinazotokana na wafadhili zinatumika vibaya.
Nape alimweleza Rais wa TFF, Jamal Malinzi kuwa anapata ujumbe mfupi
kuwa wafanyakazi hawajalipwa mishahara kwa miezi mitatu, jambo ambalo
Malinzi alikiri na kutolea ufafanuzi.
“Wafanyakazi wanadai mshahara wa mwezi mmoja kwani Julai wamelipwa
ila kocha mkuu wa timu ya Taifa Stars, Charles Mkwasa na msaidizi wake
Hemed Moroco wanatudai lakini hadi Oktoba tutakuwa tumewalipa,” alisema
Malinzi.
Katika hatua nyingine, Waziri Nape alizungumzia mchakato wa
mabadiliko kwenye klabu kongwe za Simba na Yanga na kusema kuwa serikali
inabariki lakini akatahadharisha taratibu na sheria zifuatwe.
“TFF usisubiri mpaka jipu liive ukiwa umekunja mikono ukiangalia
mambo yakienda ovyo ni lazima mhakikishe uuzwaji unakuwa wazi, sheria na
taratibu zinafuatwa ili kuondoa harufu ya rushwa na haki za wanachama
waliokuwa wamiliki kabla zilindwe,” alisema Nape.
“Mtu anamiliki mkono halafu anatangaza anauza mkono halafu anaununua
tena mwenyewe, haiwezekani lazima ajiondoe kwenye ushindani ili haki na
sheria zifuatwe,” alisema.
Nape alisema serikali inafuatilia kwa makini mchakato mzima hatua kwa
hatua ili haitasita kuingilia pale ambapo sheria zinakiukwa.
Aidha Waziri Nape alisema watashirikiana na TFF kutatua mgogoro wa
Stand United ili kunusuru ustawi wa maendeleo ya soka na kuahidi
kuzungumza na mdhamini wa timu hiyo ACACIA waendelee kuidhamini.
Pia ameagiza Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuwa
makini na chaguzi za mikoa na uchaguzi mkuu wa Shirikisho hilo
utakaofanyika mwakani ili kuziba mianya yote ya rushwa ili kuwapata
viongozi bora.
No comments:
Post a Comment