Sunday, September 11, 2016
Ndalichako awaamsha walimu
WALIMU nchini wamesema Jumanne wataeleza madai yao ya nyuma ambayo bado wanaidai Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi.
Kauli hiyo imetolewa na Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba alipozungumzia kauli ya Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako kuwa wizara hiyo haina deni inayodaiwa na walimu nchini na kwamba madeni yaliyokuwepo ya Sh bilioni 22 yalishalipwa.
Mukoba alisema baada ya kusikia taarifa hiyo, amepata simu kutoka kwa walimu wa pande mbalimbali za nchi wakilalamikia, lakini aliwatuliza ili kufanya hesabu kisha kutoa hadharani takwimu za madeni yao yaliyobaki.
Alisema anafahamu madeni ya wizara hiyo na yale yanayotakiwa kulipwa na Ofisi ya Rais, Utumishi yakiwemo ambayo yeye mwenyewe alienda kuyakusanya mkoani Shinyanga ya wakaguzi na walimu ambayo ni madeni ya zamani, lakini mpaka leo hayajalipwa.
Alisema alipeleka wizarani mwenyewe na mengine kutoka mikoa mbalimbali ambayo yote hayajalipwa sasa anashangaa kusikia madeni yote yamelipwa kitendo ambacho kimewasononesha sana walimu.
“Jumanne tutatangaza kiasi cha deni ambalo walimu wanadai wakiwemo pia wakaguzi na wengine kwani bado wanadai fedha nyingi haiwezekani waziri kusema amelipa madeni yote ya zamani na kutaka yapelekwe mapya,” alisema Mukoba ambaye pia ni Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta).
Akizungumza katika kipindi cha Tunatekeleza kinachorushwa hewani na Kituo cha Televisheni cha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1), Waziri Ndalichako alisema madeni ya walimu yako ya aina mbili; moja ya mishahara ambayo wizara hawayashughulikii na yapo chini ya Ofisi ya Rais, Utumishi.
Alisema madai yanayowahusu ni yale yasiyo ya mishahara kama vile likizo, matibabu na mengineyo ambayo hadi sasa wamelipa Sh bilioni 22 na yanashughulikiwa na wizara hiyo na kuwataka walimu wenye madeni mapya wayawasilishe wizarani kwa ajili ya kuhakikiwa na kulipwa.
No comments:
Post a Comment