Wednesday, September 14, 2016

Makala:Mfumo wa anwani za makazi utasaidia kukusanya mapato nchini

sigala
Balozi wa Balozi wa Anwani za Makazi Duniani Prof. Anna Tibaijuka akimkabidhi Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu Prof. Norman Sigala anwani ya makazi kwa niaba ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania Dkt. Tulia Ackson wakati wa wa hafla ya uzinduzi wa Mwongozo wa Mfumo wa Anwani za Makazi na Mwogozo wa Postikodi katika ukumbi wa Pius Msekwa Bungeni Mjini Dodoma.

sigala1
Balozi wa Balozi wa Anwani za Makazi Duniani Prof. Anna Tibaijuka akimkabidhi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. George Simbachawene anwani ya makazi wakati wa wa hafla ya uzinduzi wa Mwongozo wa Mfumo wa Anwani za Makazi na Mwogozo wa Postikodi katika ukumbi wa Pius Msekwa Bungeni Mjini Dodoma.

Na Eleuteri Mangi na Beatrice Lyimo, MAELEZO, Dodoma.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema kuwa Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi una manufaa mengi ambao utarahisisha ukusanyaji wa mapato kutoka vyanzo mbalimbali nchini.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema hayo leo mjini Dodoma wakati alipokuwa akizindua Mwongozo wa Mfumo wa Anwani za Makazi na Mwongozo wa Postikodi ambao utatumika nchi nzima.

“Kama kila mlipa kodi tutamfahamu kwa uhakika anaishi wapi,   tutamutoza kodi stahiki na hili ni jambo muhimu la utawala bora” amefafanua Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa uwepo wa anwani ya makazi nchini utasaidia kurahisisha ukusanyaji wa mapato mbalimbali ikiwa ni jukumu muhimu la utawala bora.

Aidha, amesema kuwa mfumo huo wa anwani za makazi utaiwezesha  Serikali kuwahudumia wananchi wake kirahisi ikiwa ni pamoja na kutoa ulinzi, kurahisisha mawasiliano miongoni mwa wananchi na Serikali.

Vile vile mfumo huo utasaidia kurahisisha na kuongeza ufanisi katika utoaji huduma za kijamii, huduma za kibiashara, huduma za dharura na uokoaji, kurahisisha sensa, kuboresha daftari la wapiga kura, kuboresha huduma za posta na kuwezesha utoaji wa biashara mtandao.

Waziri Mkuu ameongeza kuwa katika nchi nyingi za viwanda na nchi zilizoendelea suala la miundombinu ikiwemo Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi ni muhimu na linaeleweka kwa kila mtu katika kuanzisha, kukuza na kuendeleza uchumi wa viwanda.

“Kwa kutumia mfumo huu, viwanda viwe vikubwa au vidogo vinatambulika viko wapi kwa anwani zao za makazi na hivyo kuweza  kupima kirahisi ukuaji wa viwanda” alifafanua Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu amesisitiza taasisi zote za umma na zile za binafsi zianze kutumia anwani za makazi na postikodi ili kuchochea kasi ya maendeleo ya nchi ikiwa ni pamoja na kutumia katika makusanyo ya mapato.

Waziri Mkuu Majaliwa amewasisistiza wadau wote nchini kuzingatia kuwa na anwani ni haki ya kila mtu na pia kupata huduma za msingi kupitia mfumo huo ni haki ya kila mtu.

Aidha, dhana ya kuwa “dunia ni kijiji” inapaswa kuwa chachu ya kupata huduma zote mahali ulipo, inahitaji juhudi za makusudi za kuhakikisha Tanzania imekuwa sehemu ya kijiji hicho na inakuwa ni moja ya mataifa kinara wa kutoa huduma mbalimbali kwa ufanisi kwa kutumia Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi.

Kwa upande wake Balozi wa Anwani za Makazi Duniani Prof. Anna Tibaijuka amesema kuwa anajivunia mradi huo kutekelezwa nchini ambao utasaidia kuonesha watu mahali wanapoishi ambapo Tanzania imefanikiwa kuwa na anwani za makazi nchi nzima licha ya changamoto ya  kuwa na miji mingi ambayo haijapangwa.

Zao la anwani za makazi linatokana na Umoja wa Posta Dunia (UPU) iliyopitishwa katika mkutano mkuu wa 25 uliofanyika mjini Doha, Qatar mwaka 2012 ambao ulipitisha azimio la kuzitaka nchi zote duniani kuhakikisha kuwa kila mtu anakuwa na anwani.

No comments:

Post a Comment