WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa
amesema serikali imelipa Sh trilioni 1.2 kwa makandarasi wenye madeni
yao ya nyuma na mapya.
Ameagiza makandarasi hao kurejea haraka katika maeneo ya ujenzi wa
miradi ya barabara na madaraja na kuanza kazi hizo kwa kasi,
wasiotekeleza watanyang’anywa zabuni zao na kutopewa zabuni nyingine
tena nchini.
Amesema Serikali ya Awamu ya Tano, itahakikisha barabara zote
zinazojengwa katika kiwango cha lami, zinakamilishwa kwa muda uliowekwa
na katika ubora wa hali ya juu, hivyo makandarasi wote walipewa zabuni
kufanya kazi zao kwa kasi ya ‘Hapa Kazi Tu’ na si vinginevyo.
Profesa Mbarawa alitoa kauli hiyo juzi wakati alipofanya ziara ya
kushitukiza katika mradi wa ujenzi wa barabara ya Magole- Turiani kwa
kiwango cha lami pamoja na daraja kubwa la Divue ambalo ujenzi wake
ulisimama tangu Septemba 2014 hadi ulipoanza tena Juni mwaka huu.
Akiwa katika ukaguzi huo, alimtaka mkandarasi wa Civil Engineering
Construction Corporation (CCECC) kutoka China, kuongeza kasi ya ujenzi
wa barabara Magole- Turiani yenye urefu wa kilometa 48.6 kutokana na
udhaifu aliouonesha katika ujenzi wake, ama sivyo serikali
itamnyang’anya kandarasi hiyo.
Awali, Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Mkoa wa Morogoro
(Tanroads), Godwin Andalwisye akitoa taarifa kwa waziri, alisema mradi
wa barabara ya Magole- Turiani yenye urefu wa kilometa 48.6 ni sehemu ya
utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya Magole- Turiani- Mziha yenye urefu
wa kilometa 88.6 kwa kiwango cha lami.
No comments:
Post a Comment