Vyama
tisa vya siasa kati ya 22 vyenye usajili wa kudumu vipo hatarini
kufutwa kutokana na kushindwa kukidhi vigezo na matakwa ya kisheria
yaliyoviwezesha kupata usajili wa kudumu.
Hatua
ya kufutwa vyama hivyo, vikiwamo baadhi visivyo na ofisi za kudumu
(vyama vya mfukoni) itafikiwa ikiwa vitashindwa kujieleza kutokana na
makosa ambayo Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imebaini katika
ukaguzi uliofanyika hivi karibuni Bara na Visiwani.
Jukumu
kubwa la Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ni kusimamia, kuboresha,
kuendeleza na kudumisha demokrasia ya vyama vingi hapa nchini majukumu
ambayo yanatokana na Sheria ya Vyama vya Siasa Na. 5 ya mwaka 1992 na
Sheria ya Gharama za Uchaguzi Na. 7 ya mwaka 2010.
Majukumu
mengine ya ofisi ya msajili ni kusajili vyama vya siasa na kuvifuta
vyama ambavyo havikidhi matakwa ya sheria hiyo na kusimamia ugawaji wa
ruzuku ya Serikali kwa vyama vya siasa kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza
ofisini kwake jana, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis
Mutungi alisema uhakiki uliofanywa na ofisi yake katika vyama hivyo
upande wa Bara na Visiwani umebaini kasoro nyingi zikiwamo za ukiukaji
wa masharti ya usajili.
“Katika uhakiki uliofanywa na ofisi yangu tumebaini kasoro mbalimbali
ambazo kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa ni miongoni mwa vigezo
muhimu vinavyoangaliwa ili chama kiwe na sifa ya kusajiliwa,” alisema.
“Kasoro
tulizozibaini ni nyingi na baadhi ya vyama kutokana na mapungufu waliyo
nayo huhitaji kutoa nafasi tena….unaweza kuvifuta hapohapo.”
Msajili
hakutaka kutaja majina ya vyama hivyo ambavyo tayari vimeandikiwa barua
lakini alitaja makosa kuwa baadhi havina ofisi za kudumu Tanzania Bara
na Visiwani au upande mmoja na vingine havina anuani ya posta.
“Unakuta chama fulani kina ofisi labda Zanzibar lakini hakina ofisi Bara,”
alisema Jaji Mutungi. Alisema vyama vingine havina viongozi wa kitafa
kutoka pande mbili za Muungano na pia havina bodi ya wadhamini
iliyosajiliwa kwa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (Rita) kama
sheria inavyohitaji.
Katika
ukaguzi huo, Msajili alibaini pia kasoro nyingine kuwa ni kukosekana
kwa orodha ya wanachama wa chama husika jambo alilosema nalo ni muhimu
kila chama kuwa na orodha ya idadi ya wanachama wake.
Vilevile, baadhi ya vyama hivyo vimeshindwa kuonyesha akaunti ya fedha ya chama hali inayotia shaka namna vinavyojiendesha.
No comments:
Post a Comment