WAKATI
mwigizaji wa kundi la Orijino Komedi, Emmanuel Mgaya 'Masanja
Mkandamizaji' akiendelea kusakwa, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es
Salaam limesema unenguaji uliofanywa na wasanii wa kundi la Orijino
Komedi jukwaani wakiwa wamevalia sare za jeshi hilo ndiyo sababu ya
kuwakamata.
Juzi
usiku jeshi hilo liliwatia mbaroni waigizaji wanne wa kundi hilo kwa
kosa la kuvaa nguo zinazodhaniwa kuwa ni za Jeshi la Polisi kinyume cha
sheria na taratibu za nchi.
Waliokamatwa Jumanne na kuachiwa kwa dhamana juzi ni Lucas Lazaro (Joti), Serious David, Alex John na Isaya Gideon.
Kaimu
Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Naibu Kamishna Hezron
Gyimbi, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana,
alisema kitendo hicho cha kunengua mauno kilidhalilisha jeshi hilo na
waliwakamata ili kuwahoji na pindi watakapobaini uhalali wa sare hizo,
watawachukulia hatua zaidi za kisheria.
“Waigizaji
hawa wa komedi tumewaita ili kuwahoji kufahamu uhalali wa sare
walizokuwa wamezivaa ambazo zinafanana na za jeshi hili, kinyume cha
sheria za nchi.
“Lakini kama mlivyoona mkanda waliokuwa wamevaa, una tofauti gani na huu niliovaa?” alihoji Naibu Kamishna Gyimbi huku akionyesha mkanda wake.
Alisema
jeshi hilo lina miiko na kanuni zake, na hawaruhusiwi kushiriki
shughuli za sherehe na kucheza wakiwa wamevalia sare hizo.
“Siyo
Jeshi la Polisi tu, hata wengine; Magereza au JWTZ (Jeshi la Wananchi
la Tanzania) huruhusiwi kuvaa sare zao bila kibali maalum labda cha
kutaka kuelimisha jamii… lakini hawa hawakuwa na kibali na walivaa
wakiwa kwenye shughuli ya mwenzao,” alisema.
Naibu
Kamishna huyo Gyimbi alisema jeshi hilo linaendelea kumsaka Masanja kwa
kuhusika kwenye tukio hilo likiamini ni mshiriki anayeweza kufahamu
walikozipata sare hizo.
Alisema
Masanja ambaye hakuvaa sare hizo wakati wa sherehe hiyo ya mapokezi ya
harusi yake, pia alishiriki kwenye shughuli hiyo, hivyo wanataka kumhoji
wakiamini ana ushahidi wa tukio hilo.
"Masanja
tunamtafuta kama mhusika wa shughuli hiyo ambayo waigizaji wenzake
walivaa sare zinazodhaniwa kuwa ni za Jeshi la Polisi kinyume cha sheria
na taratibu za nchi,” alisema.
Aliongeza kuwa Masanja anatakiwa kujisalimisha polisi na watamkamata mahali popote atakapopatikana.
Video
za waigizaji hao wakiwa na nguo zinazodaiwa na Jeshi la Polisi kuwiana
na sare zao, zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii zikiwaonyesha wakitoa
burudani kwenye harusi ya Masanja.
Masanja alifunga ndoa, Jumapili iliyopita na waigizaji hao burudani kwenye tafrija ya kupongeza maharusi.
Katika
hatua nyingine, Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea na mwandishi
wa gazeti la Mwanahalisi na Mseto, Josephat Isango jana waliripoti
kituoni hapo kwa ajili ya kuitikia wito wa jeshi hilo.
Agosti
15, Kubenea aliripoti kituoni hapo na kuhojiwa juu ya makala
iliyochapishwa kwenye gazeti la Mwanahalisi, wiki tatu zilizopita
ikielezea hali ya ukiukwaji wa haki za kibinadamu Zanzibar.
Isango
naye aliripoti kituoni hapo na kuhojiwa kuhusu habari aliyoiandika
kwenye gazeti la Mseto lililofungiwa kwa miezi 36 na serikali wiki
iliyopita.
Isango aliandika habari kwenye gazeti la Mseto la Agosti 4 hadi 10 yenye kichwa cha habari 'Waziri amchafua JPM'.
Wote wawili walirudi kuendelea na shughuli zao na Isango alitakiwa kurudi leo, wakati Kubenea hakupangiwa siku ya kurudi.
No comments:
Post a Comment