Serikali
za Tanzania na Israeli zimekubaliana kuinua Sekta za Maji na
Umwagiliaji kwa kuweka mikakati madhubuti, ili kuleta mapinduzi katika
sekta hizo nchini katika kufanikisha lengo la taifa la kuwa na uchumi wa
viwanda.
Makubaliano
haya yalifikiwa jana na Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson
Lwenge na Balozi wa Israeli nchini, Yahel Vilan katika mazungumzo
yaliyofanyika katika Makao Makuu ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji,
Ubungo Maji, baada ya Balozi huyo kutembelea wizara hiyo.
"Tunapenda
kushirikiana na Serikali ya Israeli kwa kupata utaalamu wa kutoa huduma
ya majitaka na jinsi ya kuyatibu na kuyatumia kwa matumizi mengine,
ambayo kwa sasa ni moja ya changamoto kubwa, ikizingatiwa ongezeko la
huduma ya majisafi inaambatana na ongezeko la majitaka na kufikia mwaka
2020 ni lazima tuwe tumefanikiwa katika jambo hilo", alisema Mhandisi Lwenge.
Waziri
Lwenge aliendelea kusema Tanzania pia ingependa kuwa na ushirikiano na
Israeli kwenye kilimo cha umwagiliaji, lengo ni kuhakikisha Tanzania
inaongeza eneo linalotumika kwa kilimo cha umwagiliaji kutoka hekta
461,326 za sasa mpakakufikia hekta 1,000,000.
Vilevile,
kuhifadhi maji kwa kujenga mabwawa na matumizi ya maji yaliyo chini ya
ardhi kwa ajili ya umwagiliaji kwenye maeneo yenye changamoto ya maji
kama Dodoma, Katavi na Singida ili kuwepo chakula salama na cha kutosha
nchini.
Katika mazungumzo hayo Balozi Vilan alisema maji ni moja ya kipaumbele katika maeneo ya ushirikiano wao na Tanzania.
Na
Israeli iko tayari kuisadia Tanzania kwenye suala la majitaka, kwani ni
taifa linaloongoza duniani kwa huduma ya kutibu majitaka, zaidi ya
asilimia 85 ya majitaka hutibiwa na kutumika tena kwa matumizi
mbalimbali. Hivyo, wako tayari kwa kushirikiana na Tanzania katika jambo
hilo.
"Israel
piaipo tayari kuwajengea uwezo watanzania katika sekta ya kilimo cha
umwagiliaji,kwa kwenda kujifunza Israeli tunavyofanya na jinsi
tulivyopiga hatua kubwa katika sekta hiyo.
"Nina
hakika ndani ya miaka kumi ijayo Tanzania itakuwa imepiga hatua kubwa
kimaendeleo katika sekta hii, kwa kuwa ina maji ya kutosha, ardhi ya
kutosha na hali ya hewa ni nzuri kwa kilimo," alisema Balozi Vilan.
Hii
ni sehemu ya ziara ya Balozi wa Israeli nchini ya kutembelea wizara
mbalimbali Tanzania kwa lengo la kukuza ushirikiano wa nchi hizo mbili
katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo.
No comments:
Post a Comment