Daudi
Felix Ntibenda jana asubuhi alikuwa na majukumu ya kufungua mikutano
miwili na kufanya shughuli nyingine kwa nafasi yake ya mkuu wa Mkoa wa
Arusha, lakini hakuweza kuyatimiza kikamilifu majukumu hayo kwa kuwa
Rais John Magufuli alikuwa na mawazo tofauti na mipango yake.
Ingawa haikufahamika sababu ya kuondolewa kwake, huenda mvutano baina yake na Umoja wa Vijana wa CCM Mkoa ukawa umechangia.
Saa
2:12 asubuhi jana, Ofisi ya Waziri Mkuu ilikuwa imeshatoa taarifa kuwa
uteuzi wa Ntibenda umetenguliwa na nafasi yake imechukuliwa na Mrisho
Gambo ambaye aliteuliwa hivi karibuni kuwa mkuu wa Wilaya ya Arusha.
Taarifa hiyo ya Ofisi ya Waziri Mkuu haikueleza sababu za kutenguliwa uteuzi wa Ntibenda ambaye amekuwa Arusha tangu mwaka 2014.
Kwa
mujibu wa taarifa hiyo, Ntibenda, ambaye alikuwa Mkuu wa Wilaya ya
Karatu kabla ya kuteuliwa kushika wadhifa huo mwaka 2014, amehamishiwa
ofisi ya Waziri Mkuu ambako atapangiwa kazi nyingine.
Jana,
Ntibenda alikuwa akisubiriwa kufungua mkutano wa shirika la kimataifa
la afya kwa vijana (AMREF) na tayari tangu asubuhi alikuwa ofisini kwake
kujiandaa kwa majukumu hayo ya siku.
Mbali
na mkutano huo, Ntibenda alitarajiwa kushiriki kama mwenyeji katika
mkutano wa Mfuko wa Maendeleo (Tasaf) ambao ulishirikisha wakuu wote wa
mikoa ya Kanda ya Kaskazini pamoja na wakuu wa wilaya.
Kwenye
mkutano wa AMREF, Ntibenda alisubiriwa kwa muda mrefu hadi habari za
kutenguliwa kwa uteuzi wake ziliposambaa, ndipo akateuliwa mganga mkuu
wa mkoa, Frida Mokiti kufungua mkutano huo.
Habari
za uhakika kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa zinasema kuwa kabla ya kuibuka
kwa taarifa za kutenguliwa kwake, Ntibenda alikuwa na mazungumzo na
Gambo ofisini kwake.
Haikujulikana
mara moja mambo waliyozungumza wawili hao, ingawa tangu Ntibenda
ateuliwe kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha kumekuwa na utulivu wa kisiasa.
Ntibenda
alikuwa kwenye mzozo na viongozi wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM),
ambao walikuwa wakimlalamikia kuingilia majukumu ya jumuiya hiyo.
Mwenyekiti
wa UVCCM wa mkoa, Lengai ole Sabaya aliwaambia waandishi wa habari
mapema wiki iliyopita wakati akisoma maazimo ya kamati ya utekelezaji,
kuwa mkuu huyo anakwamisha utendaji wao.
Katika
taarifa hiyo UVCCM ilisema kitendo cha Ntibenda kuingilia kati sakata
la mikataba ya wapangaji katika maduka ya jumuiya hiyo ni kuwakwamisha.
Baadaye
kundi la viongozi hao wa UVCCM pia lilidaiwa kuandika barua ya
kumlalamikia Ntibenda kutokana na kutoridhishwa na utendaji wake.
Hata
hivyo, Ntibenda alikanusha tuhuma zote za UVCCM kumtetea mmoja wa
wapangaji na kusema anasikitishwa na madai hayo dhidi yake.
Uteuzi wa Gambo
Wakati Ntibenda akienguliwa, baadhi ya viongozi wa UVCCM jana walikuwa wenye furaha baada ya Gambo kupandishwa cheo.
Mbunge wa viti maalumu, Catherine Magige alimpongeza Rais Magufuli kwa uteuzi wa Gambo ambaye alisema ni zao la jumuiya hiyo.
Magige alisema uteuzi huo unaonyesha jinsi gani Rais Magufuli alivyo na imani na vijana na akawataka kuendelea kumuunga mkono.
“Tunaamini Gambo ataleta mabadiliko makubwa ya utendaji katika Mkoa wa Arusha kwa kuwa ni mchapakazi,” alisema.
Wakati Magige akisema hayo, Ole Sabaya alisema Rais Magufuli amesikia kilio chao.
“UVCCM tulikuwa na malalamiko juu ya utendaji wa mkuu wa mkoa, sasa tunashukuru sana Rais Magufuli kusikiliza kilio chetu,” alisema Ole Sabaya.
Kuondolewa Ntibenda
Lakini
hali ilikuwa tofauti kwa mbunge wa Arusha, Godbless Lema aliyesema
anaona vurugu zikirudi na kwamba uteuzi wa Gambo ni kama mkakati wa
kuhakikisha wapinzani wanasambaratishwa mkoani Arusha ambako ni moja ya
ngome za Chadema.
Lema,
ambaye amekuwa katika mgogoro na Gambo katika siku za karibuni, alisema
kada huyo ameteuliwa ili kuidhibiti Chadema, jambo ambalo chama hicho
hakitakubali.
“Hivi
karibuni nilimwambia mkuu wa mkoa Ntibenda kuna watu wanakutafuta, sasa
wamefanikiwa. Lakini mimi naona Arusha ijayo itakuwa na vurugu tofauti
na utulivu uliopo sasa,” alisema.
Hata hivyo, alisema Chadema imejipanga kuendelea kufanya siasa za kistaarabu na kamwe haitakubali kuhujumiwa na mtu yeyote yule.
Alipotafutwa jana asubuhi, Gambo alisema hana cha kuzungumza na kwamba hakuwa na taarifa rasmi.
Gambo,
ambaye jana alishiriki mkutano wa Tasaf kwa nafasi yake ya mkuu wa
Wilaya ya Arusha na baadaye kuondoka, alisema alikuwa hajapata taarifa
rasmi.
Hata
hivyo, akiwa kwenye mkutano baadhi ya wakuu wa mkoa na wakuu wa wilaya
za mikoa ya Kanda ya Kaskazini, walimpongeza kwa uteuzi huo.
Katibu
Tawala wa Mkoa wa Arusha, Richard Kwitega alisema alipata taarifa za
uteuzi huo jana asubuhi na alipata maelekezo kuwa Gambo anatakiwa Dar es
Salaam.
“Nilipata taarifa rasmi ya uteuzi wake na tayari tulikuwa naye hapa ofisini ili kuweka taratibu za kwenda kuapishwa,” alisema.
Alisema
Gambo atarejea Jumamosi na atapokewa na wafanyakazi na baadaye
kushiriki mapokezi ya Mwenge wa Uhuru wilayani Ngorongoro.
No comments:
Post a Comment