Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu akiwa ofisini mara baada ya kukabidhiwa ofisi na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo ambaye kwa sasa amestaafu Gishuli Charles.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu akiwa na kamati ya ulinzi na usalama Wilayani humo
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu wakikabidhiana nyaraka na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo ambaye kwa sasa amestaafu Gishuli Charles.
Na Mathias Canal, Singida
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu ametangaza rasmi siku ya Jumatano kuwa siku ya kazi za pamoja katika majengo ya Umma katika Vijiji vilivyopo Wilayani humo.
Tangazo hilo amelitoa kwenye halfa iliyofanyika katika ukumbi wa Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida wakati anakabidhiwa ofisi na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo ambaye kwa sasa amestaafu Gishuli Charles.
Mtaturu amesema kuwa Uongozi utachagua kama ni Shule, Zahanati au Utengenezaji wa Barabara n.k.ambapo Wananchi wote watapaswa kushiriki kazi hiyo ili warejeshe moyo wa kushiriki shughuli za maendeleo ambapo mkuu huyo amesema yeye atafanya kazi ya kupita katika maeneo tofauti kuungana na Wananchi katika kukamilisha kwa vitendo jambo hilo..
Amewakumbusha wananchi kuwa wakati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na wenzake waliokuwa wanaanza harakati za kudai Uhuru walienda Umoja wa Taifa wakahakikisha tunaweza kujitawala na kujisimamia wenyewe bila mkoloni.
Mwaka 1961 tulipopata Uhuru Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alieleza sasa tumepata uhuru tubadili malengo ya Taifa iwe ni Uhuru na Kazi aliamini kupitia kazi tutapata maendeleo.
Awamu ya Tano imekuja na kauli mbiu ya “HAPA KAZI TU”; kwa maana hiyo hiyo kuhimiza Wananchi kufanya kazi na kazi ndio kipimo cha utu.
Mkuu huyo amesema kuwa wananchi wote wanapaswa kufanya kazi kwa bidii ili kuweza kuboresha maisha ya kila mmoja na familia zetu kwa ujumla.
Mkuu huyo amesema kuwa Kwa mujibu wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi mwaka 2015 – 2020. Ibara ya 49 imeeleza Serikali kuongeza huduma za Afya, kuongeza Wataalamu wa Afya kwenye Zahanati, Vituo vya Afya, Hospitali za Wilaya n.k.
Amesema Ilani imetambua yaliyotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Nne katika Sekta ya Afya kama msingi wa kuendeleza juhudi zaidi kupiga vita Malaria, UKIMWI, Vifo vya Mama na Mtoto n.k. Uboreshaji na upatikanaji wa dawa na vifaa tiba.
Katika Wilaya ya Ikungi kuna upungufu wa asilimia 62% ya Zahanati hivyo kufanya akina Mama Wajawazito kutembea mwendo mrefu kufuata ushauri wa kitaalamu.
Huduma ya kuzuia maambukizi ya VVU kwenda kwa mtoto (PMTCT) vimeongezeka ila bado havitoshi; Vituo vya tiba vya maangalizi ya wanaoishi na VVU (CTC) bado ni vichache sana.
Ili kutatua changamoto ya huduma duni za afya Mtaturu ameshauri Wananchi kuhamasishwa kujiunga kwenye Mifuko ya Bima ya Afya kama NHIF, CHF n.k. na kusema kuwa Faida ya kujiunga na Bima ya Afya msingi wake ni kuwa ugonjwa hauna taarifa hivyo unaweza kuugua siku hauna fedha Bima ikakusaidia.
Katika sekta ya upatikanaji maji safi na salama amesema kuwa Ni lengo la Serikali kuhakikisha Wananchi wake wanapata Maji Safi na Salama kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo na Wananchi hivyo ameahidi Kuzipa uwezo Kamati za Maji katika Vijiji ili kusimamia Miradi iliyopo iwe endelevu ikiwemo kusoma Mapato na Matumizi kwa Wananchi kwa Mujibu wa Sheria.
Katika swala la Ukusanyaji wa Mapato Mtaturu amesema kuwa Changamoto iliyopatikana kipindi kilichopita ni kuwa chini ya 80% ya lengo la ukusanyaji mapato hivyo Kuanzia tarehe 01Julai, 2016 Serikali imeamua sasa Halmashauri zitakusanya zenyewe mapato badala ya Wazabuni.
Miraji Mtaruru amezungumzia pia suala la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi SURA YA TANO YA ILANI YA UCHAGUZI MKUU YA CHAMA CHA MAPINDUZI Ibara ya 56. Imeeleza dhamira ya kuwezesha Wananchi kiuchumi kupitia Ushirika (SACCOS& VICOBA) ikizingatiwa kupitia vikundi ndio mahali pekee unaweza kuwapatia mitaji na kutakuwa na nidhamu ya fedha.
Hivyo amewahimiza Maafisa Ushirika, Maendeleo ya Jamii kuendelea kuwajengea uwezo Wananchi ili kurahisisha Serikali kushusha fedha za mitaji.
Katuika swala la Watumishi Hewa Mtaturur amesema kuwa Pamoja na juhudi za Serikali kuboresha masilahi ya Watumishi ila kumejitokeza uzembe mkubwa wa watu kulipwa wasiostahili.
“Natoa muda wa Wiki moja Mkurugenzi na timu yako mnipatie taarifa kamili kuhusu Wafanyakazi hewa na imebainika Idara ya Elimu ndio inayoongoza kuwa na Watumishi hewa, swali la kujiuliza Afisa Utumishi, Mratibu Elimu Kata ambao kazi yao kila siku ni kushughulika na Kada hiyo anakuwa hajui kama kuna watu wanalipwa wasiokuwepo kazini? Hali hii haikubaliki na hakika tutachukua hatua kali kwa yeyote atakayebainika kuingizia Serikali hasara ya aina yeyote.” Amesema Mtaturu
Mkuu huyo amesema kuwa Serikali ya awamu ya Tano imeamua kupitia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi Ibara ya 51; imefafanua namna Elimu iliyowekewa msisitizo. Elimu ya Awali; Elimu Msingi na Sekondari hadi Chuo Kikuu ikiwa ni pamoja na Kuboresha masilahi ya Walimu ikiwa pamoja na madai yao ili wapate moyo wa kufanya kazi kwa bidii zaidi, na Ahadi ya Elimu bila kulipa ada Shule ya Msingi hadi Kidato cha Nne imeanza utekelezaji mwaka huu ingawa imekutana na changamoto kwa kupata upungufu wa Madarasa n.k.
Aidha Pamoja na hayo bado kuna baadhi ya watoto wenye sifa za kwenda Shule hawajaandikishwa; kimsingi ni haki ya kila mtoto kupatiwa Elimu, hivyo wazazi wasiowapeleka Watoto Shule wanakiuka Sheria.
Mtaturu ametoa maagizo ya Watoto wote waliofikia umri wa kwenda Shule; Maafisa Tarafa, Watendaji Kata na Vijiji wampepe taarifa na hatua walizochukua.
“Kuhusu upungufu wa Nyumba za Walimu, Vyumba vya Madarasa, Maabara zisizokamilika, matundu ya vyoo, vitendea kazi n.k. ni lazima tuweke mpango wa pamoja kuondoa changamoto hizo ili kuhakikisha Watoto waliopo Shuleni wanapata elimu bora” Amesema Mtaturu
Wilaya ya Ikungi ina jumla ya wakazi 272,959 na ongezeko la watu kwa mwaka ni 2.8% hivyo sasa kunakadiriwa kuwa 303,000 kwa mwaka 2015/2016 kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2012
No comments:
Post a Comment