Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ambaye pia
ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, amekutana na kufanya
Mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Uganda Mheshimiwa Yoweri Kaguta
Museveni, ambapo pamoja na mambo mengine wamekubaliana kujengwa kwa
bomba la kusafirisha mafuta kutoka Bandari ya Tanga nchini Tanzania hadi
nchini Uganda.
Rais
Museveni alimtembelea Rais Magufuli katika Ikulu ndogo ya Arusha jana
jioni mara baada ya kuwasili hapa nchini akitokea nchini Uganda, ambapo
leo atahudhuria Mkutano Mkuu wa 17 wa kawaida wa wakuu wa nchi wanachama
wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, utakaofanyika katika Hoteli ya
Ngurudoto Jijini Arusha.
Akizungumza
baada ya viongozi hao kufanya mazungumzo ya faragha, Rais Magufuli
alisema wamekubaliana kutekeleza mradi huo wa bomba la kusafirisha
mafuta kutoka Tanga hadi Uganda, kwa manufaa ya nchi zote mbili na nchi
nyingine za Afrika Mashariki.
Alisema bomba hilo litakuwa na urefu wa kilometa 1,120 na kwamba mradi huo utazalisha ajira za watu zaidi ya 15,000.
Rais
Magufuli aliongeza kuwa pamoja na kujengwa kwa bomba la mafuta, pia
walizungumzia kuongeza biashara ndani ya nchi za jumuiya ya Afrika
Mashariki, kujenga viwanda na kuzalisha ajira zaidi kupitia sekta
mbalimbali za uzalishaji mali.
Aidha,
Rais Magufuli alisema katika Mkutano huu nchi wanachama watajadili
maombi ya nchi ya Sudan Kusini kupata uanachama ndani ya Jumuiya ya
Afrika Mashariki.
Alibainisha
kuwa, kwa Sudan Kusini kuwa mwanachama Jumuiya ya Afrika Mashariki,
itakuwa na uwezo wa kufanya biashara katika eneo lenye takribani watu
milioni 150 na hivyo kupata manufaa makubwa zaidi.
Kwa
upande wake Rais Yoweri Kaguta Museven pamoja na kuunga mkono
yaliyosemwa na Rais Magufuli alimpongeza kwa kasi yake nzuri aliyoanza
nayo katika uongozi, na alisema ni matumaini yake kuwa nchi wanachama wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki, sasa zitakuwa katika nafasi nzuri ya
kwenda kwa kasi ya Rais Magufuli katika maendeleo.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Arusha
01 Machi, 2016
No comments:
Post a Comment