Friday, July 3, 2015

kipindupindu huko S/Kusini

29 wapoteza maisha kwa kipindupindu huko S/Kusini
Watu wasiopungua 29 wamefariki duniani kufuatia mlipuko wa maradhi ya kipindupindu huko Sudan Kusini huku mamia ya wengine wakiwa katika hatari ya kuambukizwa ugonjwa huo. Ripoti iliyotolewa na Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF imebainisha kwamba, kuna kesi 484 za ugonjwa huo zimeripotiwa vikiwemo vifo vya watu 29 huku sita kati ya waliofariki dunia kwa maradhi hayo wakiwa ni watoto wa chini ya umri wa miaka mitano. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watoto elfu tano walio chini ya umri wa miaka mitano, wako hatarini ya kufa kutokana na ugonjwa huo, ikiwa hatua za dharura hazitachukuliwa. Ugojwa huo ni hatari zaidi hasa miongoni mwa watoto kwa sababu husababisha mwili kupoteza maji mengi kutokana na kutapika na kuharisha. Shirika la Afya Duniani (WHO) linafanya juhudi za kuwahamasisha watu kuhusu jinsi ya kuzuia ugonjwa huo na pia kutoa chanjo. Mwezi uliopita Wizara ya Afya ya Sudan Kusini ilitangaza kuwa watu wasiopungua 18 waliaga dunia kwa ugonjwa wa kipindupindu. Shirika la Afya Duniani(WHO) limetangaza kuwa mwaka jana mlipuko wa kipindupindu uliiathiri Sudan Kusini ambapo watu zaidi ya 6400 waliambukizwa na 167 miongoni mwao walifariki dunia.

No comments:

Post a Comment