Thursday, July 23, 2015

DAR WAFURIKA VITUO VYA BVR

Wananchi wakiwa katika folen kusubri huduma na mmoja wao akiwa katika eneo la kupigwa picha.

Maelufu ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, jana walijitokeza kwa wingi katika siku ya kwanza ya uandikishaji wapigakura katika mfumo wa kisasa wa kielektroniki (BVR), licha ya kuwapo kwa changamoto kadhaa.

Katika vituo vingi, licha ya wananchi kujitokeza kuanzia mapema alfajiri, changamoto kadhaa zilijitokeza, ikiwemo mashine kushindwa kufanya kazi kutokana na hitilafu, hivyo kuchelewesha uandikishaji, ingawa baadaye ufumbuzi ulipatikana Wachangishana pesa.

Katika Kituo cha Shule ya Msingi Tabata Kisukuru, Manispaa ya Ilala, licha ya kituo kuwa na mashine mbili, zote zilishindwa kuwaka kutokana na kutokuwa na umeme huku kifaa cha umemejua kikielezwa kuwa na hitilafu.

Kutokana na hali hiyo, wananchi walihamasishana kuchanga Sh 100 kila mmoja ili kupata Sh 30,000 za kulipia umeme uliokuwa umeombwa na watumishi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutoka nyumba ya jirani.

Baada ya mjadala, baadhi ya wananchi hao waliofikia 800 waligoma kulipa wakidai Serikali ilishatenga fedha za uandikishaji wapigakura. Hali hiyo ilisababisha kuchelewa zaidi kwa kazi ya kuandikisha wapigakura.
Pamoja na kuchelewa huko, baadhi ya wananchi hawakukata tamaa, mpaka alipokuja ofisa mwingine wa tume aliyetengeneza vifaa vya umeme jua na ndipo uandikishaji ukaanza majira ya saa saba.
Wachezeana rafu

Wakati wakisubiri kuandikishwa, baadhi ya wananchi walijikuta wakitafuta mbinu ya kuwahi kuandikishwa, kwa kughushi namba zao, mathalani, aliyekuwa kwenye nafasi ya 300 na kupewa namba 300, alifuta sifuri moja ili isomeke 30.

Kuna waliofanikiwa, lakini wengine walikwama kutokana na kutumia wino tofauti na ule ulioandikwa katika karatasi za awali na wahusika. Pugu ‘ngoma’ yalala Katika kituo cha Pugu Stesheni, wananchi wapatao 500 waliowahi katika kituo hicho kujiandikisha, walitakiwa kurudi nyumbani na kurejea leo kutokana na mashine kusumbua na kuwa itaandikisha watu 10.

Kituo cha Mistuni A na B kulikuwa na misururu kutokana na kazi ya uandikishaji kutoanza kutokana na ubovu wa vifaa.

Mpaka HabariLeo inafika kwenye vituo hivyo viwili majira ya saa 6 mchana, hakuna mwananchi yeyote aliyeandikishwa kutokana na mashine ya kituo cha Mistuni A kusumbua kamera huku Mistuni B mashine ya kuchapa karatasi kukorofisha.

“Mpaka sasa bado hatujaanza kuandikisha, mashine moja kamera inasumbua, na mashine nyingine inasumbua na ndio mafundi wanahangaika kutengeneza. Muda wowote mashine zitakapotengamaa basi tutaanza kuandikisha,” alisema ofisa wa tume ambaye alikataa kutaja jina lake.

Katika kituo cha uandikishaji cha Majengo Vingunguti, HabariLEO ilishuhudia umati wa watu wakizozana wakiwa kwenye mstari, hali ambayo imechangiwa na kuchelewa kuanza kwa kazi hiyo.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mitaa wa Majengo Vingunguti, Chande Msoke alisema kumekuwapo na tatizo la kuchelewa kwa vifaa, jambo ambalo limefanya kazi hiyo ianze kwa kuchelewa saa tatu, jambo ambalo limesababisha mizozo ya hapa na pale.

“Watu wamefika hapa saa 11: 30 asubuhi, vifaa na ufungaji wa turubai umechelewa jambo ambalo limesababisha vurugu za hapa na pale. Tulichofanya tuliwaandikisha wale waliofika mapema na pale kazi ya uandikishaji ilipoanza ndio walioanza kuhudumiwa. Aliongeza: “Kutokana na kuchelewa kuanza watu wamekuwa wakali kiasi ambacho hata akija mama mjamzito, mzee au mlemavu wanakataa kumpisha, haya yote yanachangiwa na kuchelewa jambo ambalo linafanya watu kukaa sana kituoni.

Kuhusu kasi ya kuandikisha, Msoke alisema imekuwa ikienda taratibu kutokana na mashine kushindwa kutambua alama za vidole kwa baadhi ya watu ambao inawachukua dakika 45 kukamilisha kazi hiyo.
“Wale ambao mashine inashindwa kutambua alama za vidole, tunawataka wakanawe mikono na sabuni, na kama bado itakuwa shida, basi tunamtaka arejee kesho,” alisema.

Katika kutuo cha Mchafukoge, Mnazi Mmoja, kazi ya uandikishaji ilichelewa na ilianza saa 3 asubuhi kutokana na kuchelewa kufikishwa vifaa huku kazi hiyo ikifanyika taratibu sana.
Katika kituo cha Majani ya Chai, Kipawa, shughuli ya uandikishaji ilianza saa tatu asubuhi na baada ya kuhudumia watu watano mashine ilikorofisha hivyo kufanya kazi hiyo kusimama kwa muda.
Ubungo yale yale

Wakati hayo yakitokea katika Manispaa ya Ilala, katika wilaya ya Kinondoni nako uandikishaji ulianza kwa kusuasua, licha ya wananchi kujitokeza kwa wingi. Ilielezwa uchelewaji huo ulitokana na mashine hizo kuletwa juzi usiku na hivyo kazi ya ufungaji kuchelewa, ikielezwa kila kituo kina mtaalamu mmoja wa teknolojia ya habari na mawasiliano (IT).

Katika kituo cha kujiandikisha cha shule ya msingi Ubungo Plaza, Mwandishi Msaidizi wa kituo hicho, Charles Samson akiwa na wenzake wawili, walionekana kukaa bila kufanya jambo lolote huku amezongwa na watu na kusema mashine hizo zilipokelewa juzi usiku, hivyo hazijawekewa software.

Alisema hatua hiyo inatokana na kuwa mtaalamu wa IT kutoka NEC kuwa mmoja katika kata hiyo ya Ubungo, hivyo walimsubiri hadi alipokamilisha kazi na uandikishaji kuanza baada ya saa nne. Aidha, ilielezwa baadhi ya watu waliokuwa na haraka za kuendelea na shughuli zao, walishindwa kusubiri wakiahidi kurudi baada ya mambo kuwa sawa.

Nako Mbezi Beach katika eneo la Miti Mirefu mpaka kufikisha saa nne asubuhi uandikishaji ulikuwa haujaanza kutokana na kuwa vifaa hivyo vilikuwa havijafika, jambo lililofanya watu kuondoka katika vituo huku wengine wakibaki na kupigwa na jua.

Huku eneo la kawe walichelewa kuanza uandikishaji licha ya vifaa hivyo kuwa vimefika kutokana na kudaiwa kuwa umeme ni mdogo hivyo mashine hizo hazikuweza kufanya kazi mpaka kufikia saa nne asubuhi.

Temeke nao wachelewa Kama ilivyokuwa Ilala na Kinondoni, wakazi wa Temeke nao walijitokeza kwa wingi katika vituo mbalimbali vya uandikishaji, huku changamoto ikiwa vifaa, ingawa baadaye ilipatiwa ufumbuzi.

Katika kituo cha Mtaa wa Mwembebamia kata ya Chamazi, baadhi ya watu wananchi waliojitokeza kujiandikisha walililamikia ucheleweshwaji uliofanywa na waandikishaji hao kwani hadi kufikia saa 3 asubuhi uandikishaji ulikuwa bado haujaanza.

Wakizungumza na gazeti hili, walidai kuwa walifika mapema katika kituo hicho kwa matarajio kuwa waandikishaji hao wangefuata ratiba na kuanza saa 2 ili waweze kuwahi katika shughuli zao zingine.

Ramadhani Issa, mkazi wa Mwembebamia B, alidai licha ya utaratibu wa kutoa namba kwa kila mwananchi anayefika kuwa mzuri, lakini utaratibu huo una dosari kubwa kwani baadhi ya watu walifika mapema lakini walipewa namba za mwishoni tofauti na waliochelewa, suala linaloonekana kuwa ni kama kuna upendeleo.

Katika Kata ya Maganga iliyopo Temeke watu waliojitokeza na walilalamikia waandikishaji kwenda taratibu kutokana na mashine kuchelewa kufanya kazi, huku mtu mmoja akilazimika kutumia hadi dakika 20 ili kupiga picha. Kwa upande wa kata ya Azimio, watu wengi pia walijitokeza huku changamoto ya kuchelewa kufika kwa wahusika na mashine kuwa chache.

Wanung’unikia mashine
Wananchi wa Kata ya Mzinga Manispaa ya Ilala, wamelalamikia usumbufu walioupata kwa mashine za uandikishaji kugoma kufanya kazi kutokana na tatizo la mtandao, jambo lililosababisha uandikishaji kuanza saa tano asubuhi kwa kutumia mashine moja.
Akizungumza na gazeti hili jana, mkazi wa kata hiyo, Saidi Ndembo alisema wananchi wa kata hiyo walipata usumbufu mkubwa kwasababu walifika kituoni hapo kujiandikisha alfajiri, lakini mashine hazikuwa zikifanya kazi.

Alisema kutokana na mashine kusumbua na kulazimika kutumia mashine moja badala ya mbili zilizokuwepo kituoni hapo, wananchi walitangaziwa kuondoka kituoni na kubaki watu 150 ambao wataandikishwa na wakati huo kituo kilikuwa na watu zaidi ya 500 kitendo ambacho kilizua mzozo.

Imeandikwa na Annastazia Anyimike, Theopista Nsanzugwanko, Regina Kumba na Sophia Mwambe.

No comments:

Post a Comment