Thursday, July 23, 2015

23 kizimbani kwa tuhuma za ugaidi




WATU 23 wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka ya ugaidi, kukutwa na silaha na vifaa vya kutengenezea milipuko.

Washitakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka sita kwa siri mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Kwey Rusema.

Washitakiwa katika kesi hiyo ni Jafari Hassan, Sadick Shaban, Ibrahim Abdallah, Said Hamisi, Ally Ayoub, Saidi Waziri, Juma Ally, Shomary Said, Khatib Hassan, Issa Hassan na Nurdin Salum.

Wengine ni Hamad Omary, Salum Hamisi, Ahmad Yussuf, Hamisi Hussein, Hamisi Miraji, Ally Juma, Abdallah Hamisi, Abdillah Ismail, Shaibu Sam, Seif Ramadhani, Hassan Abdallah na Abdul Rashid.

Kwa mujibu wa kesi hiyo iliyosomwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Peter Njike akisaidiwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Joseph Maugo, washitakiwa wanakabiliwa na mashitaka ya ugaidi, kukutwa na silaha pamoja na vifaa vya kutengeneza milipuko na kukutwa na sare ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ).

Katika hati ya mashitaka, inadaiwa kati ya Desemba mosi 2014 na Juni 30 mwaka huu, katika maeneo la Mbagala Kilungule, Temeke Dar es Salaam na kijiji cha Kibindu Bagamoyo, washitakiwa walikula njama ya kufanya makosa ya ugaidi.

Aidha, inadaiwa kati ya Desemba mosi 2014 na Juni 20, mwaka huu, katika eneo la Mbagala Kilungule, Hassan akiwa mmiliki wa nyumba iliyopo Mbagala Kilungule, aliwahamasisha washitakiwa wenzake kufanya vitendo vya ugaidi.

Wakili Njike aliendelea kudai kuwa Hassan, Said na Abdallah kati ya Desemba Mosi, 2014 na Juni 20,2015 huko Mbagala Kilungule waliandaa mkutano wa kuwezesha kufanyika kwa vitendo vya ugaidi.

Katika mashitaka mengine, Njike alidai kati ya Desemba Mosi, 2014 na Juni 20, mwaka huu, Hassan aliwaingiza washitakiwa Shaban, Abdallah, Hamis, Ayoub, Said, Hassan, Salum, Omary, Hamis, Yusuf, Hussein na Ramadhan ili washiriki katika vitendo vya ugaidi.

Aidha inadaiwa Juni 30, mwaka huu katika eneo la Mbwewe Mkwajuni Bagamoyo, Shaban, Abdallah na Salum walikamatwa wakiwa na silaha aina ya SMG yenye namba ya siri 14302621, risasi 50 za SMG, 10 za shotgun, jambia, visu vinne na vifaa vya kutengeneza milipuko.

Katika mashitaka mengine inadaiwa Juni 26, mwaka huu katika kijiji cha Kibindu Bagamoyo kwa hali ya kuhatarisha usalama wa nchi, Ally alikamatwa akiwa na sare za JWTZ. 

Washitakiwa hawakuruhusiwa kujibu mashitaka kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, isipokuwa Mahakama Kuu.

Upande wa Jamhuri ulidai kuwa bado wanaendelea na upelelezi wa kesi hiyo. Washitakiwa walirudishwa rumande hadi Agosti 4, mwaka huu itakapotajwa tena .

No comments:

Post a Comment