Wednesday, October 25, 2023

Dkt Yonazi “Jitihada za Serikali na Wadau zachangia kuimarika kwa hali ya lishe na kupungua kwa viwango vya utapiamlo nchini”

NA. MWANDISHI WETU

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amesema Utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Pili wa Masuala ya Lishe wa mwaka 2021-22-2025/26 umekuwa na mafanikio makubwa kutokana na juhudi za pamoja za wadau wa lishe nchini na kupelekea kuimarika kwa kiasi kikubwa kwa hali ya lishe na kupungua kwa viwango vya utapiamlo kwa baadhi ya viashiria.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Wadau wa Lishe nchini unaofanyika Jijini Arusha katika Ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Mount Meru tarehe 25 Oktoba, 2023, Dkt. Yonazi amesema kupitia mkutano huo utaweza kujadili mafanikio hayo na kuona uwezekano wa mikoa mingine kutumia mbinu zilizotumika katika mikoa iliyopata mafanikio na dhairi kuwa kasi ya kupungua viwango vya udumavu kwa watoto nchini itaongezeka

Dkt. Yonazi amesema kiwango cha Udumavu kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano ambacho ndiyo kiashiria kikuu cha Utapiamlo kimepungua kutoka asilimia 34 mwaka 2016 hadi asilimia 30 mwaka 2022 na tathmini imeonesha kuwa mikoa saba imefanikiwa kupunguza vinwango hivyo kwa watoto zaidi ya asilimia 10 katika kipindi cha mwaka 2016 hadi 2022.

“Mafanikio mengine yanajumuisha kupungua kwa kiwango cha ukondefu kutoka asilimia 3.8 mwaka 2016 hadi asilimia 3.5 mwaka 2022 pamoja na kupungua kwa tatizo la upungufu wa damu miongoni mwa wanawake walio katika umri wa uzazi (miaka 15 hadi 49) kutoka asilimia 44.8 mwaka 2015 hadi asilimia 28.8 mwaka 2018.” alisema Dkt. Yonazi

Aidha, Dkt. Yonazi amesema licha ya mafanikio yaliyopatikana kupitia Utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Pili wa Masuala ya Lishe wa mwaka 2021-22-2025/26, amesema bado kuna changamoto ambazo zimeendelea kuongezeka ikiwemo kuongezeka kwa idadi ya watoto wenye udumavu ambapo takwimu zinaonesha kuongezeka kutoka 2,700,000 mwaka 2016 hadi kufikia 3,400,000 mwaka 2022.

“Ni wajibu wetu sote katika mkutano huu kuhakikisha mikakati na maazimio tutakayoyafikia yanalenga kupunguza changamoto zinazotukabili katika utekelezaji wa Mkakati Jumuishi wa Kitaifa wa Lishe, ikiwemo changamoto ya kuongezeka kwa idadi ya watoto wenye udumavu.” Alisema Dkt. Yonazi

Akitoa salamu za kwa niaba ya Wadau wa Lishe nchini, Mkuu wa Shughuli za Lishe kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF) Patric Codjia, amesema wataendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuhakikisha masuala ya lishe yanaendelea kuimarika na kuyafikia malengo yaliyopo.

“Tutaendelea kushirikiana na Serikali ya Awamu wa Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu kwa matokeo Chanya katika kuhakikisha masuala ya lishe yanapewa kipaumbele na kuwa na matokeo tayarijiwa na tumefarijika kuwa sehemu ya kongamano hili la wadau wa masuala ya Lishe,” alisema Patric

=MWISHO=

No comments:

Post a Comment