Sunday, May 21, 2023

MCHENGERWA ATOA MIEZI MIWILI KUKAMILISHA MKAKATI WA KUONGEZA UZALISHAJI WA MAZAO YA NYUKI

 

Waziri wa Maliasili na Utalii Mohamed Mchengerwa akizindua kibanda cha kuuzia asali hafla iliyofanyika katika kilele cha maadhimisho ya siku ya nyuki Duniani iliyofanyika Kitaifa Mkoani Singida Leo Mei 21, 2023 katika Viwanja vya Bombadia.

Waziri wa Maliasili na Utalii Mohamedi Mchengerwa (Katikati), Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Marry Masanja (Kulia) na Thomas Apson Mkuu wa Wilaya ya Ikungi (Kushoto) wakiwa katika picha ya Pamoja baada ya kuzindua kitabu cha mwongozo wa uzalishaji wa mazao ya Nyuki kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya nyuki Mei 21, 2023 Mjini Singida.

Uzinduzi wa Mwongozo wa ufaugaji nyuki ukiendelea kwenye kilele cha Siku ya Nyuki Duniani.


Waziri wa Maliasili na Utalii Mohamed Mchengerwa akikabidhi tuzo kwa wadau mbalimbali wa nyuki na Misitu.

Waziri wa Maliasili na Utalii Mohamed Mchengerwa pamoja na Naibu Waziri Marry Masanja wakionyesha bidhaa zitokanazo na nyuki wakati walipokuwa wakitembelea mabanda kwenye maadhimisho ya nyuki mkoani Singida.

Ugawaji wa Tuzo na zawadi mbalimbali ukiendelea.


Na Hamis Hussein - Singida

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa amewataka watendaji wa sekta ya Misitu na Nyuki kukamilisha mkakati wa kuongeza uzalishaji wa asali toka tani 35000 za sasa hadi tani 138000 katika kipindi cha miezi miwili alioupa jina la mkakati wa “achia shoka kamata mzinga” huku akitaka eneo la misitu na asali kufanyiwa utafiti wa kutosha ili litumike kama zao jipya la utalii.

Mchengerwa ameyasema hayo leo Mei 21, 2023 kwenye Kilele cha maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani yaliyofanyika kitaifa katika Uwanja wa Bombadia mkoani Singida.

Akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho hayo amesema pamoja na uwepo wa maeneo makubwa yaliyohifadhiwa na yanayofaa kwa ajili ya kuzalisha mazao ya nyuki yenye viwango bora bado takwimu zinaonesha uzalishaji ni 23% ikilinganishwa na uwezo uliopo wa kuzalisha tani 138,000 kwa mwaka.

“Tuongeze uzalishaji maeneo haya ya uhifadhi wa nyuki ili asali tunayotengeneza hapa nchini ipate soko kimataifa, hii ndio kazi kubwa watalamu tunapaswa kufanya, Wizara iandae mpango ili tutoke kwenye uzalishaji wa 23% tutoke kwenye uzalishaji wa tani 35000 na tufike 138000 na huu mkakati Naibu Waziri niupate ndani ya Miezi Miwili”, Alisema Waziri Mchengerwa.

Katika kuhakikisha mkakati huo unakuwa na tija Waziri Mchengerwa ameagiza  Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Mfuko wa Misitu kuhakikisha wanawezesha wananchi hasa wale wanaopakana na maeneo ya hifadhi kwa kuwapatia mafunzo ya ufugaji nyuki wenye Tija  pamoja na mizinga ya kisasa ili maeneo ya uhifadhi yaweze kuwanufaisha wananchi.

Akitolea mfano amesema  Mkoa wa Singida umebarikiwa kuwa na uoto wa kipekee ujulikanao kwa jina maarufu kama Vichaka vya Itigi (Itigi Thicket) ambao upatikana katika nchi mbili tu duniani, yaani Tanzania na nchi ya Zambia ambao  katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni kumekuwa na kasi kubwa ya ukataji na uondoaji wa uoto huu kwa shughuli mbalimbali za kibinadamu.

Hali hii imesababisha sehemu kubwa ya ardhi iliyokuwa na uoto huu kubaki wazi na pia kumebainika kuwepo kwa mimea vamizi pale ambapo uoto huu ulipoondolewa kutokana na hali hiyo ameielekeza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuhakikisha kuwa maeneo yote yaliyobaki ambayo yenye uoto huo yanatambuliwa na kuhifadhiwa kisheria, pia wananchi waliopo kwenye maeneo hayo wanapewa elimu kuhusu utunzaji wa mazingira na ufugaji nyuki kibiashara.

Aidha amesema pamoja na faida nyingi tunazopata kutoka kwa mdudu nyuki bado nyuki anaweza kutumika kutupatia zao jipya la utalii ambapo amesema katika nchi ya Slovenia mdudu nyuki hutumika sana kwa ajili ya shughuli za utalii.

“Katika nchi ya Slovenia nyuki anatumika kwaajili ya utalii kwa kuwavutia watalii wa nchi mbalimbali kutembelea eneo hilo, hivyo niwaomba TFS Kuandaa baadhi ya maeneo ya Misitu yatumike kama kule ya Slovenia ili na sisi tuweze kutengeneza zao jipya la utalii, hatupaswi kushindwa na mataifa mengine tunapaswa kuwa namba moja katika uzalishaji wa nyuki na asali Duniani”, Alisisitiza Mchengerwa.

Naye Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo amekuwa akielekeza na kusisitiza kulinda Maliasili na kuendeleza utalii.

Aidha, amempongeza Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohammed Mchengerwa kwa kutembea takriban nchi nzima kuhamasisha utunzaji wa maliasili, mazingira na uendelezaji utalii.

Awali akitoa taarifa ya hali ya uzalishaji wa mazao ya Nyuki Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Singida ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Thomas Apson alisema kuwa Mkoa huo umehifadhi Hekta 476,361 za misitu ya asili pamoja na vichaka vya itigi vyenye ukubwa wa hekta 61,436.28 ambao ni uoto unaotoa asali asilia duniani.

DC Apson amesema kuwa Mkoa umeongeza wafugaji wa nyuki kutoka 5,675 mwaka 2017/ 2018 hadi wafugaji 12,133 mwaka 2022 ikiwa ni sawa na Asilimia 113.8% ambapo katika kipindi cha miaka mitano kuanzia 2017 hadi 2022 Mkoa umeshuhudia ukiingiza kiasi cha shilingi 890 zilizotokana na uzalishaji wa asali tani 89 na shilingi 140 zitokanazo na tani 20 za nta.

 

No comments:

Post a Comment