Friday, March 10, 2023

Majukumu Kuhamishiwa Sekta Binafsi Chanzo Mikataba 209 Kuvunjwa TASAC


Na Saida Issa, Dodoma 

SHIRIKA  la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limesema sababu ya kuvunja mikataba ya vijana 209 waliokuwa wakifanya mafunzo ya vitendo pahala pa kazi (internship) ni baadhi ya majukumu ya shirika hilo kuhamishiwa sekta binafsi. 

Akizungumza leo jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Ndg. Kaimu Mkeyenge amesema vijana hao walikuwa wakifanya kazi ya uhakiki wa shehena(cargo tallying).

"Mnamo Julai 2022 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilifanya mabadiliko ya Sheria ya Uwakala wa Meli Tanzania, Sura 415 kupitia Sheria ya Fedha Na. 5 ya Mwaka 2022 kwa kufuta majukumu ya kipekee ya uwakala wa meli,

"Majukumu yaliyofutwa ni uhakiki wa mizigo, udhibiti wa nyaraka na kupunguza wigo wa jukumu la kufanya uwakala wa forodha katika bidhaa zilizokuwa zinagombolewa na kuondoshwa na TASAC chini ya kifungu cha 7(1)(a), (b), (c) na (d)," ameeleza Ndg. Mkeyenge. 

Pamoja na hilo, Ndg. Mkeyenge amesema mikataba hiyo ilivunjwa kwa kufuata sheria na muongozo wa mafunzo ya vitendo pahala pa kazi uliotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu.

No comments:

Post a Comment