Tuesday, February 28, 2023

DKT.NDUMBARO AMEWATAKA VIONGOZI WA TAASISI ZA UTOAJI HAKI KUSHIRIKIANA KATIKA KUONDOA VIKWAZO VINAVYOKWAMISHA UTEKELEZAJI WA SHERIA YA WATOA TAARIFA

 4I6A6177.JPG


Na Okuly Julius-Dodoma

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.Dkt.Damas Ndumbaro ,amewataka viongozi wa taasisi za utoaji haki kushirikiana katika kuondoa vikwazo vinavyokwamisha utekelezaji thabiti wa Sheria ya watoa Taarifa na Ulinzi wa Mashahidi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Dkt.Ndumbaro ameyasema hayo leo Februari 28,2023 Jijini Dodoma, wakati wa hafla ya uzinduzi wa Kanuni za watoa taarifa na Ulinzi wa Mashahidi ,ambapo amesema kuwa taarifa zinaonesha kuwa utayari wa wananchi kutoa taarifa umeongezeka na walio wengi wako tayari kushiriki katika mapambano dhidi ya uhalifu kwa kufika katika vyombo vya sheria.

Amesema kuwa watanzania wakishiriki kwa pamoja katika kufichua maovu yakiwemo yanayosababisha hasara kwa taifa utasaidia kukuza uchumi na kuweka mazingira wezeshi kwa uwekezaji.

4I6A6210.JPG

"Ili tufikie malengo yaliyokusudiwa ya kuhakikisha tunafichua kila aina ya maovu yanayotokea ikiwemo ufisadi,ukiukwaji wa haki za binadamu na matumizi mabaya ya madaraka na mengine mengi yaweze kuripotiwa bila woga kwa maslahi mapana ya nchi yetu,"

Na kuongeza kuwa "Niwaombe tuendelee kutoa elimu ya kisheria kwa umma wa watanzania kuhusiana na sheria na kanuni tajwa ili wawe na uelewa na wajue umuhimu wa kuwafichua wahalifu wa makosa mbalimbali yanayotendeka katika jamii yetu ili mwisho wa siku matukio ya kiuhalifu yapungue na na hatimaye kuisha kabisa,"amesema Dkt.Ndumbaro

4I6A6242.JPG

Pia Dkt.Ndumbaro amewataka wananchi kutohofia kujitokeza kutoa taarifa za uhalifu na matendo ya aina zote yanayofanywa kinyume cha sheria, kwani taarifa hizo zitakuwa siri na zitafanyiwa kazi bila ya kuwataja watoa taarifa , pia mashahidi wanapotakiwa kufika mahakamani wasiogope kwani Kanuni hizo zinaweka mfumo wa kuwalinda ambao unaeleza masharti na namna za ulinzi huo.

"Kanuni hizi zinalenga kurahisisha utekelezaji wa Sheria na kuongeza ufanisi katika utekelezaji na kufikiwa kwa madhumuni ya Sheria. Sambamba na hilo, Kanuni hizi zitasaidia kuwapatia ulinzi wa kisheria wale wote wanaotoa taarifa za uhalifu wa makosa ya aina mbalimbali na hivyo kuwaongezea imani na usalama wao na hivyo kurahisha uendeshaji wa mashtaka,"amesisitiza Dkt.Ndumbaro

4I6A6230.JPG

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na ufuatiliaji Haki Kharist Luanda amesema kuwa kuzinduliwa kwa kanuni hizo inafungua milango kwa wananchi kuanza kutoa taarifa mbalimbali kwa kujiamini kwani kanuni hizo zimebainisha namna watoa taarifa na mashahidi watakavyopatiwa ulinzi.

"Kanuni hizi ni muhimu sana kwani zinamuhakikishia ulinzi mtoa taarifa na shahidi na kumtengenezea uhuru hata wakati wa kutoa ushahidi mahakamani kwa sababu kanuni hizi zimeshamuhakikishia usalama,"amesema Luanda

4I6A6061.JPG

Kanuni hizo za Watoa Taarifa na Ulinzi wa Mashahidi zimekuja baada ya Serikali, mwaka 2016 kuanza kutekeleza Sheria ya Watoa Taarifa na Ulinzi wa Mashahidi ya mwaka, 2016 (The Whistleblower and Witness Protection Act. 2016 ,sheria hiyo ikiwa na lengo la kuimarisha misingi ya utoaji haki jinai na kukuza utawala bora na mapambano dhidi ya uhalifu nchini.

No comments:

Post a Comment