MWENYEKITI wa Jukwaa la
Wanawake wa mkoa wa Dodoma Mary Mabhaye amewataka wanawake wanaochukua
mikopo kutoka taasisi za kifedha kutokuwa watumwa kwa kushindwa kurejesha
kwa wakati.
Aidha,badala yake wawe
na elimu ya matumizi na nidhamu ya fedha za mikopo,ili waweze kumudu kurejesha
kwa wakati na wapatiwe mikopo tena.
Mabhaye amesema hayo
alipokuwa akizungumza na Wanawake kwenye semina ya Jukwaa la
Wanawake kwa ajili ya mafunzo ya kuwainua kiuchumi iliyofanyika Jijini Dodoma.
Alisema wanawake wengi
wamekuwa wakianzisha vikundi kwa malengo ya kukopa fedha ili waondokane na
utegemezi na umasikini lakini matokeo yake wakati wa kurejesha wanageuka
kuwa watumwa.
Alisema wanawake hao
badala yake wamekuwa watumwa na kusababisha hata familia zao kushindwa kuzilea
kutokana na kuwa na muda mwingi wa kuishi kwa kujificha.
“Tatizo walilonalo
baadhi ya wanawake wanaochukua mikopo hawana elimu ya kutosha juu ya
ujasiriamali,badala yake wanajikuta wakiangukia kwenye matumizi yasiyokuwa na
tija ambayo ujikuta wakishindwa kurudisha mikopo hiyo kwa wakati”alisema.
Mwenyekiti huyo,hata
hivyo amewashauri wanawake hao kujitokeza kugombea kwenye nafasi za
uongozi mbalimbali hapa nchini, ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Alisema wakijitokeza
wataweza kupata fursa mbalimbali nchini ambazo zitakazo wainua kiuchumi na
kuwasaidia wanawake wengine katika suala zima la kujipatia maendeleo.
Kwa upande wake Afisa Biashara
wa Jiji la Dodoma Donatila Donisi, amesema wanawake wamekuwa na mchango mkubwa
katika kuleta maendeleo kwa lengo la kukuza uchumi nchini hivyo
wamejiandaa vyema kutoa elimu kwenye vikundi vyao .
Donisi amesema kuwa
wanawake wengi wamekuwa wakianzisha vikundi mbalimbali katika suala zima
la kujikwamua kiuchumi.hivyo kwa upande wao kama Jiji wamejipanga katika
kuwapatia elimu ya ujasiliamari.
“Halmashauri ya Jiji
wataweza kutoa elimu hususani katika biashara wanazofanya kwa lengo la
kurasimisha ili kuwasaidia katika kutambulika na kupata masoko ya kufanyia
biashara kwa urahisi.
"Sisi kama Jiji
hususani kwenye ofisi ya biashara tutakuwa tayari kwa ajili ya kuwapa elimu
mbalimbali ikiwemo umuhimu wa kurejesha mikopo kwa wakati pamoja na ulipaji wa
kodi ili kuwezesha serikali kufanya maendeleo,"alisema.
Kwa upande wao washiriki
wa mafunzo hayo ya kujikwamua kiuchumi Juliana Sakaine,Ailen Salvatory
wamewashauri wajasiliamari kutengeneza bidhaa zitakazowafanya kuingia kwenye
soko la ushindani ndani ya nje ya nchi.
Walisema kuwa tatizo lililopo kwenye bidhaa nyingi zinazo tengenezwa hazina viwango na zilizo nyingi zinakosa masoko na kwa sababu hiyo watu bado wataendelea kuzipenda zinazotoka nje ya nchi.
No comments:
Post a Comment