Waziri wa Nishati na Madini wa Burundi Mhe. Ibrahim Uwizeye akizungumza mara baada ya kuwasili mkoa wa Kagera kujifunza kujifunza zaidi kuhusu Sekta ya Madini hususan utekelezaji wa mradi mkubwa wa uchimbaji wa madini ya nikeli.
Ikiwa umepita mwezi mmoja tu tangu kufanyika kwa Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini wa mwaka 2022, tayari Waziri wa Nishati na Madini wa Burundi Mhe. Ibrahim Uwizeye amefika nchini kwa lengo la kujifunza zaidi kuhusu Sekta ya Madini hususan utekelezaji wa mradi mkubwa wa uchimbaji wa madini ya nikeli.
Ziara ya Waziri wa Nishati na Madini wa Burundi nchini inakuja baada ya kuhudhuria mkutano wa madini ambao ulikuwa wa manufaa kwa nchi hiyo. Hivyo, alimuomba Waziri wa Madini kuja kujifunza zaidi kutoka kwa Tanzania kutokana na namna ilivyofanikiwa katika usimamizi wa Sekta ya Madini ikiwemo utekelezaji wa miradi mikubwa ya madini ili hatimaye rasilimali madini zinazopatikana nchini Burundi zilinufaishe taifa hilo.
Akizungumzia lengo la ziara hiyo, Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko amesema imelenga kujifunza kupitia mradi huo ili kuona namna ambavyo nchi hiyo inaweza kujifunza kutoka Tanzania na namna ambavyo nchi hizo zinavyoweza kushirikiana katika utekelezaji wa miradi ya namna hiyo na kuongeza kuwa, ni mapema sana kusema kitakachofuata baada ya ziara hiyo.
“Mradi wa Kabanga Nikeli na Msongati nchini Burundi ni mmoja, jiolojia ya Kabanga na Msongati ni moja na kama mnavyojua jiolojia haina mipaka isipokuwa mipaka ya kiutawala. Pia, wamefika kuona namna nchi hizi zinavyoweza kufanya ili hatimaye ziweze kuwa mfano bora wa ushirikiano kwa mataifa mengine Afrika,” amesema.
Aidha, Waziri Biteko amemuelezea waziri huyo kuwa ni mtu mwenye kiu na wivu wa maendeleo ya kuona rasilimali madini inalinufaisha taifa hilo kwa kuwa amekuwa akifuatilia Sekta ya Madini nchini kwa kipindi kirefu na kuongeza, “nimpongeze sana waziri wa Burundi kwa kuwa na wivu wa rasilimali madini kwani tusipokuwa na wivu wa rasilimali zetu baadaye tutachekwa.’’
Aidha, Waziri Biteko ameonya kuhusu wale wote wanaotegesha kwa lengo la kunufaika na malipo ya fidia na kueleza kuwa hawatalipwa chochote isipokuwa tu kwa wananchi wenye uhalali wa kulipwa. Pia, ameongeza kuwa, Serikali haitawavumilia wale wote wanaofanya vitendo vya tegesha.
Kwa upande wake, Waziri Uwizeye amesema ujumbe wake umefika nchini kujifunza ili mradi huo uweze kuzinufaisha nchi zote ikiwemo kuhakikisha nchi hiyo pia inachimba madini hayo na hivyo kuiomba Tanzania kuipa nafasi ya kujifunza kuhusu utekelezaji wa mradi huo kwa kuwa jiolojia ya madini hayo pia inapatikana nchini humo.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Kanali Mathias Kahabi amemhakikishia Waziri Biteko kuwa, Wilaya hiyo haitokuwa kikwazo cha utekelezaji wa mradi wa uchimbaji wa nikeli. Ametumia fursa hiyo kuelezea masuala muhimu matatu ambayo tayari yamefanywa na wilaya hiyo, ikiwemo kufanya zoezi la kutambua maeneo ya kupisha mradi; mazungumzo ya awali kati ya wawekezaji na wananchi katika ngazi zote; na mapitio ya makubaliano ya kuhamisha wananchi.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya ametumia fursa hiyo pia kumuomba Waziri Biteko kuweka msukumo ili kuwezesha mradi huo kuanza kwa wakati uliopangwa.
Akizungumza katika ziara hiyo, Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Dkt. Gilly Maleko amesema baada ya kuwepo mahusiano mazuri ya kidiplomasia kwa nchi hizo ambazo zimekuwa marafiki kwa miongo mingi, ilionekana kuwa ipo haja ya kukuza mahusiano ya kiuchumi.
Naye, Balozi wa Jamhuri ya Burundi nchini Tanzania, Gervouis Abayeho, amesema baada ya kufahamu kuwa Tanzania ina uzoefu wa muda mrefu katika Sekta ya Madini, nchi hiyo imeona ipo haja ya kujifunza kutoka Tanzania ili kupata uzoefu utakaoiwezesha nchi hiyo kusimamia Sekta ya Madini kwa manufaa ya nchi hiyo ikiwemo kuzisaidia nchi hizo kugeuza sura za kiuchumi kwa mataifa hayo.
Kadhalika, Mbunge wa Jimbo la Ngara Mheshimiwa Ndaisaba Ruhoro, ameihakikishia nchi hiyo kuwa kama mbunge wa eneo hilo atahakikisha anapambania ujenzi wa miundombinu muhimu ikiwemo barabara na umeme ili utekelezaji wa mradi huo ufanyike kikamilifu. Ameitaka nchi hiyo kuendelea na mipango ya kuchimba madini hayo kwa kuwa miundombinu itaboreshwa.
“Burundi haipo karibu na bandari, ikichimba nikeli itapitisha kwetu tutapata fedha lakinipia kama nchi, tutanufaika na madini kutoka nchi jirani,’’ amesema Ruhoro.
Kwa upande wake, Meneja Mkazi wa Kampuni ya Tembo Nikeli Benedict Busunzu akiwasilisha taarifa kuhusu mradi huo amesema uhai wa mgodi unatarajiwa kuwa zaidi ya miaka 30 na kuongeza kuwa, tayari Kampuni hiyo imepata mbia mwenza Kampuni ya BHP ambayo ni kampuni kubwa ya madini duniani inayotarajiwa kuleta mapinduzi makubwa ya kiteknolojia katika utekelezaji wa mradi huo. Ameitaja teknolojia hiyo kuwa ni ya Hydrometallurgy kuwa ni ya kwanza kutekelezwa duniani ambayo pia, itakuwa rafiki mkubwa wa mazingira.
Busunzu ameitaja nikeli ya Kabanga kuwa ni ya daraja la juu duniani na kuutaja mradi huo kuwa na manufaa makubwa ya kiuchumi kwa Tanzania.
Akizungumzia soko la madini hayo duniani, amesema ni yanahitajika sana kutokana na kuhama kwa matumizi ya teknolojia na kueleza kuwa, kabla ya kuzuka kwa vita ya Urusi na Ukraine bei ya madini hayo kwa tani ilikuwa ni Dola za Marekani 21,000 na kupanda hadi Dola za Marekani 51,000 na ndani ya muda mfupi kufikia Dola za Marekani 100,000 kwa tani moja ya nikeli. Ameongeza kuwa, hivi sasa bei yake imeshushwa hadi kufikia Dola za Marekani 48,000 kwa tani ili kulinda mwenendo wa soko lake.
No comments:
Post a Comment