Mwenyekiti wa Shirikisho la Umoja wa Wamachinga(SHIUMA) Ernest Matondo akitoa shukrani kwa niaba ya Wamachinga kwa Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chaula (mwenye ushungi) kwa kuendesha kikao kilichoazimia kutatua changamoto za Wamachinga nchini. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Amon Mpanju.
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chaula akihitimisha kikao kati ya Wizara na Viongozi wa shirikisho la Umoja wa Wamachinga SHIUMA kilichofanyika Jijini Dodoma kwa siku mbili. Kulia ni baadhi ya viongozi wa SHIUMA.
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chaula akijadili jambo na baadhi ya Wakurugenzi wa Idara kutoka Wizara hiyo mara baada ya kikao kati ya Wizara na Viongozi wa shirikisho la Umoja wa Wamachinga SHIUMA kilichofanyika Jijini Dodoma kwa siku mbili.
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chaula katika picha ya pamoja na Viongozi wa SHIUMA Taifa mara baada ya kikao kati ya Wizara na Viongozi wa shirikisho la Umoja wa Wamachinga SHIUMA kilichofanyika Jijini Dodoma kwa siku mbili. Kulia ni Mwenyekiti wa SHIUMA Ernest Matondo, kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa shirikisho hilo Steven Lusinde.
Picha zote na kitengo cha Mawasiliano Serikalini WMJJWM
.
Na WMJJWM, Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na Shirikisho la Umoja wa Wamachinga (SHIUMA), imeazimia kuhakikisha sheria ndogo zinazowahusu wamachinga zinatafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili ili Wamachinga wote waweze kuzielewa.
Maazimio hayo yamefikiwa wakati wa kuhitimisha kikao cha siku mbili kati ya Wizara na Viongozi wa SHIUMA kutoka Mikoa ya Tanzania Bara kilichoongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chaula kilichofanyika Jijini Dodoma.
Akifunga kikao hicho, Dkt. Chaula amewataka Wamachinga kushirikiana na Serikali kutekeleza maazimio waliyojiwekea kwa wakati kwa maslahi yao na Taifa kwa ujumla.
” Kufikia tarehe 16 Machi wanasheria wa SHIUMA kwa kushirikiana na wanasheria wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum na Ofisi ya Rais TAMISEMI wakamilishe kutafsiri Sheria hizo” amesema Dkt. Chaula.
Dkt. Chaula ameyataja maazimo ya kikao hicho kuwa ni pamoja na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum iboreshe madawati ya kushughulikia masuala ya Wamachinga kwa kushirikiana na Ofisi Rais TAMISEMI hadi Halmashauri, ili kusaidia kutatua changamoto kwenye maeneo yao.
Ameyataja maazimio mengine kuwa ni Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI kuhakikisha Mamlaka za Serikali za Mitaa zinapanga na kuweka miundombinu wezeshi katika maeneo ya shughuli za Wamachinga kwa kushirikiana na Viongozi wa Wamachinga wa eneo husika, kuandaa kanzidata ya Wamachinga na Wizara kutembelea maeneo ya masoko ya Wamachinga ili kutatua changamoto zilizopo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa SHIUMA Taifa, Ernest Matondo ameishukuru Serikali kwa kuwakutanisha Wamachinga na kuahidi kushirikiana na Viongozi pamoja na Wamachinga mikoa yote ili kufanikisha kufika mbali na kutoka katika umachinga na kuwa wafanyabishara wa kati na wakubwa.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Serikali za Mitaa kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Nuru Namoroma amewahakikishia Wamachinga wote kuwa Ofisi hiyo itaendelea kuratibu masuala yao kwa ufanisi zaidi katika ngazi ya Serikali za Mitaa kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum ili wawe na mazingira mazuri ya kufanya biashara.
Aidha, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na SHIUMA kuratibu maadhimisho ya wiki ya Wamachinga itakayofanyika tarehe 29 Juni kila mwaka.
No comments:
Post a Comment