Wednesday, February 23, 2022

NDOTO YA SINGIDA YA KIJANI IMEANZA KUTIMIA KUPITIA UPANDAJI MITI

 

Mkuu wa Wilaya Singida Mhandisi Pasikas Muragili akipanda  mti pembezoni mwa ziwa Kindai hivi karibuni

 


Zoezi la upandaji miti likiendelea ziwa Kindai Mkoani Singida



Miti aina ya mikorosho ikiwa kwenye viriba ambayo imekuwa ikigawiwa kwa wananchi wa mkoa wa Singida  kwa ajili ya kupanda katika mashamba yao lengo likiwa ni kuhifadhi mazingira na kuongeza kipato


Mkuu wa Wilaya Singida Mhandisi Pasikas Muragili akimwagilia mti ambao ameupanda pembezoni mwa ziwa Kindai hivi karibuni.

 

Na Bashiri Salum - Singida

Ukisoma vitabu mbalimbali vya dini utabaini kwamba kabla ya kuumbwa kwa mwanadamu yaliumbwa mazingira ikiwepo mimea ambako humo ndipo alipowekwa Adamu kwenye bustani maalum ambapo aliishi kwa kula matunda.

Kwa kuwa mimi sio msomi mzuri wa elimu ya dini siku moja nikalazimika kuwasiliana na Mwalimu wa dini ya kiislamu Shekhe Mteti Huseni wa Usangi Mwanga Kilimanjaro nikitaka kujua uhusiano wa dini na mazingira na mchango wake katika kulinda mazingira.

Shekhe Mteti akanieleza kwamba kuna uhusiano mkubwa baina ya dini na mazingira huku akibainisha kwamba Mwenyezi Mungu amewataka waja wake kupanda miti ya matunda na kivuli na kwamba atakuwa na malipo makubwa kwa mwenyezimungu kwa yeyote atakaye panda miti na wengine wakayatumia matunda hayo au kivuli kupumzika.


Upandaji wa miti na utunzaji wa mazingira kwa ujumla ni sehemu ya ibada kwa mwanadmu  hivyo kwa atakayeyaharibu mazingira kwa namna yeyote atakuwa anatenda makosa makubwa ambalo angetakiwa kutubu kwa Mwenyezimungu.

Kwa maelezo hayo ya Shekhe yanamaanisha kwamba kama mtu atakayeharibu mazingira anatenda dhambi ni dhahiri kwamba atakaye tunza mazingira kwa namna yeyote ile atakuwa anafanya ibada na atapata malipo kwa Mwenyezimungu.


Kwa kipindi cha hivi karibuni  viongozi wa Mkoa wa Singida walifanya ibada kubwa kwa kudhamiria kubadilisha mazingira na muonekano wa mkoa huu kwa kusimamia zoezi la upandaji miti katika maeneo ya hifadhi, sehemu za kupumzikia, majumbani, kingo za barabara na mashuleni lengo likiwa ni kuondoa hali ya jangwa ambayo ilikuwa ikinyememelea mkoa huo.

Viongozi hao akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilithy Mahenge na wakuu wa wilaya za Mkoa  huo walitangaza kila jumamosi kuwa siku ya usafi na upandaji wa miti zoezi ambalo lilizinduliwa na Mkuu wa wilaya ya Singida Mhandisi Pasikas Muragili katika maeneo ya ziwa kindai kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa ambapo kwa siku hiyo pekee miti 2,000 ilipandwa.

Akiwa katika uzinduzi huo Mhandisi Muragili akawataka wananchi  kutumia mbinu mbadala za kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa yanayosababishwa na athari za mabadiliko ya Tabianchi ili kupata  Mazingira  Safi na kuondoa uwezekano wa kupata Upungufu wa chakula katika ngazi ya Kaya.


Hii inatokana na ukweli kwamba athari za ukosefu wa miti hautatenganishwa na mabadiliko ya hali ya hewa yanayosababisha upungufu wa mvua na kusababisha changamoto za kuwa na kilimo kisichokidhi mahitaji ya walaji.


Ni katika uzinduzi huo Mkuu wa Wilaya alipotangaza mkakati wa kupanda miti ambapo kila kaya ilitakiwa kuwa na miti isiyopungua mitatu (3) hadi mitano (5) katika maeneo ya  miji, na miti kumi (10) hadi kumi na tano (15) kwa maeneo ya mipaka ya mashamba lengo likiwa ni kubadilisha hali ya hewa .

Wakati wa uzinduzi huo DC Mhandisi Muragili akawaomba wananchi wa Singida kutokubali kutenda dhambi ya uharibifu wa mazingira na badala yake wafanye ibada hiyo ya kupanda miti na kuhakikisha wanaitunza.

Katika utekelezaji wa Mkakati wa upandaji na utunzaji wa miti mkoani singida  Kaimu Mkuu wa Idara ya Mazingira Manispaa ya Singida Bi Shuku Kaishwa  anasema wameandaa Mpango wa kuhamasisha jamii  na taasisi kuanzisha mashamba ya Miche pamoja kueleza jamii faida zitokanazo na mazao ya miti pamoja na   upandaji wa miti aina ya mihimbo katika vyanzo vya maji.

Jitihada za kuelimisha wadau mbalimbali wa mazingira zimekuwa zikitajwa kufanyika hasa kwa wafugaji ambao wamekuwa wakilaumiwa kuwa Ng’ombe wanakula na kuvunja miti lakini pia baadhi ya wafugaji kukata miti hovyo wakiamini kwamba wanafukuza wadudu wajulikanao kama mbung’o ambao wanasababisha magonjwa kwa mifugo yao.

Ni kutokana na sababu hiyo Afisa Mazingira huyo akatoa wito kwa  jamii ya wafugaji na wataalamu wa mifugo kuendelea kuielimisha jamii juu ya ufugaji wa ndani (zero Grazing) ili kuepuka kusambaza kwa mifugo nje na kuharibu miti iliyopandwa huku akiwataka wananchi kuhamasika na kuanza kutumia nishati mbadala ambayo itapunguza matumizi ya kuni na mkaa.

Ukweli ni kwamba Singida ina ukubwa wa kilometa za mraba 49.438 ambapo kati ya eneo hilo Km 95.5 ni yale maeneo yanayozungukwa na maji ya maziwa ya Eyasi,Kitangiri,Singidani  na Kindai hii inafanya enoeo la nchi kavu kubaki Kilomita za mraba  49342.5.

Katika taarifa ya utekelezaji ya ilani ya Ccm ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015-2020 katika kipindi cha mwaka 2017/2018 Mkoa wa Singida ulidhamiria kukuza uchumi kwa kupitia shughuli za upandaji wa miti na hifadhi ya misitu ya asili kwa kupanda miti 10,500,000.

Lengo likiwa ni kuongeza kiwango cha mavuno ya asali kupitia miti kutoka tani 286 mpaka tani 350 kwa mwaka pamoja na uongezaji wa mazao yatokanayo na miti ikiwemo mbao, Gundi matunda na hewa safi.

Ambapo ilikadiriwa kuongeza hifadhi ya misitu kutoka hekta 308,000 hadi hekta 333,000 ikiwa ni mpango wa uhifadhi wa rasilimali za misitu na kuongeza mazao ya nyuki .

Kwa kuwa mkoa wa Singida  unakadiriwa kuwa na Kaya 255,613 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 ili kufikia idadi ya miti milioni kumi na laki tano kila kaya ilitalazimika  kupanda miti 41 ili kufikia idadi inayotakiwa.

Kwa mujibu wa kitabu kilichofahamika kwa jina la Singida region investment guide ya mwaka 2020 na kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi inaonesha kwamba eneo la vijijini linakadiriwa kuwa na kaya 219,827 sawa na 86% na mjini kuna kaya 35785.2 sawa na 14%.

Kama kila kaya katika maeneo ya mjini Mkoani hapa watapanda miti mitatu (3) watakuwa na jumla ya miti 880.2 bila kuhusisha miti ya taasisi kama mashule ,pamoja na miti mingine iliyopo kando ya barabara na kwenye sehemu  za umma.

Kwa upande wa vijiji kama kila kaya kati ya kaya 219,827 itapanda miti kumi (10) kutakuwa na idadi ya miti 2,198,270 hivyo kufanya mkoa mzima wa singida kuwa na miti mipya 2,199,150.2 ifikapo 2025

Kwa kiasi hicho cha miti kinadhihirisha kwamba baada ya miaka mitatu mkoa wa Singida utakuwa umechangia kwa kiasi kikubwa katika kupunguza hewa ukaa hapa nchini na dunia kwa ujumla na kupunguza changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi.

Ni kweli kabisa kwamba ipo mikoa ambayo ishafanya zoezi hili la upandaji wa miti lakini haikuweza kufanikiwa kwa sababu mbalimbali baadhi ya watu walioulizwa  ni kitu gani kifanyike ili mkoa wa singida uweze kuwa na miti endelevu  wakawa  na haya ya kusema

Mhandisi Pasikasi Muragili mkuu wa wilaya ya singida alisema ili zoezi hili liwe la kudumu na liweze kufanikiwa wananchi  wahakikishe kwamba wanatekeleza maagizo yanayotolewa na viongozi  ili kusaidia kuifikia dhamira ya singida ya kijani

Aidha Muragili akawashauri  viongozi wa ngazi za vijiji na kata kusimamia ipasavyo kwa kutoa taarifa sahihi zitakazo saidia kukamilisha mipango hiyo.

Ili kuboresha na kutunza mazingira ni muhimu kuanzisha vilabu mbalimbali vya mazingira katika mashule ili kupandikiza mawazo ya kimazingira kwa vijana nakuwashirikisha viongozi wa dini katika  kuhamasisha utunzaji wa mazingira.

 

No comments:

Post a Comment