Thursday, February 10, 2022

NAIBU KATIBU MKUU YAKUBU HAJARIDHISHWA NA KASI YA UJENZI WA JENGO JIPYA LA WIZARA

  

Na Eleuteri Mangi- WUSM, Dodoma

Naibu Katibu Mkuu wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu Februari 10, 2022 ametembelea eneo la ujenzi wa jengo jipya la Wizara hiyo linalotarajiwa kuwa na ghorofa sita ambalo linajengwa Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma.

“Siridhishwi na kasi ya ujenzi wa jengo hili inavyokwenda, wafanyakazi wapo kidogo, boresheni utendaji kazi kwa kasi zaidi ili kuendana na malengo na matarajio ya Serikali ambayo yamewekwa” amesema Naibu Katibu Mkuu Yakubu.

Mradi wa jengo hilo la kisasa la Wizara unatekelezwa na kujengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na Mshauri Mwelekezi ni Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ambapo Naibu Katibu Mkuu Yakubu amewataka wataalamu hao kuongeza kasi ya ujenzi wa jengo hilo na liendane na thamani ya fedha iliyopangwa kutekeleza mradi huo huku akitahadharisha jengo hilo liendane na viwango vilivyopangwa kwa kuwa wameaminiwa kwa uzoefu wao katika masuala ya ujenzi nchini.

Kwa upande wake Mhandisi msimazi wa jingo hilo kutoka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Mhandisi Omari Chitawala amesema wamepokea maelekezo hayo na watayafanyia kazi haraka ili kutekeleza mradi huo kwa wakati kulingana na maelekezo ya Serikali.

Hadi kukamilika ujenzi wa jengo hilo utagharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 22.843 ambazo zitatolewa na Serikali kulingana na taratibu zilizowekwa ambapo linatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 24 sawa na miaka miwili kuanzia Septemba 2021.

No comments:

Post a Comment