Na Mathias Canal na George Binagi, Kahama- Shinyanga
Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko amefanya mazungumzo na ujumbe wa viongozi kutoka mgodi wa Nyanzaga (Nyanzaga Mining Company Limited) utakaojengwa Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza lengo ikiwa ni kupata mrejesho wa maandalizi ya awali kabla ya mgodi huo kuanza uzalishaji.
Dkt. Biteko amefanya mazungumzo hayo Jumatano Januari 26, 2022 na kutumia fursa hiyo kueleza utayari wa Serikali kuweka mazingira rafiki kwa mgodi huo ikiwemo kufikisha huduma muhimu kama nishati ya umeme, maji na barabara ili kurahisisha shughuli kuanza.
Ujumbe huo kutoka mgodi wa Nyanzaga ukiongozwa na Meneja Mkuu, Damien Valent umemhakikishia Waziri Biteko kuwa maandalizi ya ufunguzi wa mgodi huo yanaendelea vyema ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini ya ardhi ili kuwalipa fidia wananchi watakaopisha shughuli za mgodi.
Mgodi wa Nyanzaga ni miongoni mwa migodi minne iliyokabidhiwa leseni za uchimbaji mkubwa wa madini ya dhahabu mwezi Desemba mwaka jana katika hafla iliyoshuhudiwa na Rais Samia Suluhu Hassan ambapo unatarajiwa kuendeshwa kwa ubia kupitia kampuni ya pamoja baina ya Serikali na mwekezaji iitwayo Sotta Mining Corporation Limited ambapo Serikali ina hisa za asilimia 16 na mwekezaji asilimia 84.
MWISHO
No comments:
Post a Comment