Tuesday, January 18, 2022

JAMII MKOANI SINGIDA YAHIMIZWA KUFUNGAMANA NA MUNGU

 


 




Kwaya ya Gosipo ya kanisa la Pentekoste (FPCT) Singida mjini kati,ikitumbuza kwenye ibada ya kwanza ya mwaka huu (2022).


NA NATHANIEL LIMU - SINGIDA

WAUMINI na wasio waumini wa madhehebu mbalimbali ya dini mkoani Singida,wameshauriwa kutenga muda kwa ajili ya kumshukru Mungu kwa kitendo chake cha kuwavusha salama mwaka jana (2021),ambao uligumbikwa na changamoto nyingi ngumu kupitiliza,ikiwemo kuondokewa ghafla na kipenzi cha wanyonge Hayati Dk. John Magufuli na Aliyekuwa rais wa awamu ya tano .

Wito huo umetolewa askofu mstaafu wa kanisa la Pentekoste (FPCT) Singida mjini kati,Dk.Paulo Samweli,wakati akizungumza muda mfupi kabla ya mahubiri maalum ya kuaga mwaka 2021 na kukaribisha mwaka mpya wa 2022,kufanyika.

DK.Samweli alisema sio Tanzania pekee iliyopita katika kipindi kigumu mwaka jana,ni karibu dunia nzima zikiwemo nchi zilizoendelea katika nyaja zote.

Amefafanua kwamba mapema mwaka jana, wakati nchi mbalimbali duniani ikiwemo zilizoendelea kama Marekani kujifungia ndani ya nyumba kukwepa corona,Watanzania waliendelea kuchapa kazi halali.Pia walihudhuria nyumba za ibada bila masharti yo yote.

Aidha,askofu huyo mstaafu,alisema kitendo cha kuondokewa ghafla na Hayati Dk.Magufuli sio tukio la kitoto,ni tukio ngumu mno.Watanzania walitaraji katika awamu yake ya mwisho,angeenda kuiletea nchi maendeleo ambayo yageishangaza dunia.

“Kwa ujumla sisi sote bila kujali itikadi zetu za dini na kisiasa, tunawajibika kufanya ibada kwa ajili ya kumshukuru Mungu kutuvusha salama mwaka jana. Vilevile tuombe mwaka huu tuliouanza juzi uwe wa amani na utulivu mkubwa.”,alisema askofu Dk samweli.

Awali mwinjilisti wa kanisa hilo,Ernest Samsoni,alisema mwaka mpya wowote ule, unatawaliwa na mabadiliko mapya ya kila aina.

“Mwaka mpya unakuwa na namba  mpya,umri wa mtu tarakimu za namba zinabadilika, mambo ya mtu binafsi yanabadilika, kifamilia na hata Taifa kuna kuwa na mabadiliko mengi ili kuendana  na wakati. Kupitia mabadiliko hayo mhusika kwa vyo vyote,atapiga hatua kiuchumi na kijamii” alisema.

Pia  mwinjilsti huyo, amezitaka kwaya mbalimbali za kanisa hilo kutanua wingo zaidi wa nyimbo zao, ili ziwafikie watu wengi zaidi.

“Nyimbo zenu kama zitaendelea kusikika tu ndani ya kanisa letu, kitendo hicho kitakuwa kama mnajichimbia ndani ya box.Kuwenu wabunifu na hakikisheni kazi yetu inajulikana ndani na nje ya mkoa wa Singida na ikiwezekana nje ya nchi”,alisema Mwinjilsti Ernest kuzishauri kwaya hizo.

Katika ibada ya kwanza kwa mwaka huu iliyofanyika 02/01/2022 Askofu Dk.Samweli,alisema katika  mwaka ulioanza juzi,kanisa litatekeleza maagizo yaliyopo kwenye kitabu kitakatifu cha Tito 03 mstari mdogo wa 14  unaosema ‘Watu wetu nao wajifunze kudumu katika matendo mema,kwa matumizi yaliyo lazima,ili wasiwe hawana matunda’.

Akifafanua,alisema kila muumini wa kanisa hilo analo jukumu la kuhakikisha kanisa linasonga mbele kwa matendo mema,ili makanisa mengine yakimbilie kujifunza uendeshaji bora wa kanisa.

“Kanisa lazima liwe na mabadiliko yenye tija zaidi.Tuwe wabunifu tutembelee nyumba zingine za ibada ili kujifunza kutoka makanisa mengine.Tukijifunza yale mazuri na yanayompendeza Mungu,kanisa letu litasogea  mbele.Lakini tusipojifunza,kanisa litadumaa na halitakuwa na mambo mapya”,amesisitiza Dk.Samweli.

 

 


 

No comments:

Post a Comment