Tuesday, November 23, 2021

WILAYA YA UKEREWE YAZINDUA MKAKATI WA KUPAMBANA NA MARALIA




Katika kukabiliana na maambukizi ya Ugonjwa wa Maralia, Wilaya ya Ukerewe Mkoani Mwanza kwa kushirikiana na Shirika la ABT ASSOCIATES wamezindua mpango kabambe wa unyunyuziaji wa dawa ya kuulia mazalia ya mbu majumbani(Ukoko).

Zoezi hilo limezinduliwa Novemba 21, 2021 katika Kijiji cha Namagondo kata ya Namagondo na Mkuu wa Wilaya hiyo Canal Denis Mwila huku akiwataka watendaji wa zoezi hilo kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao kiuweledi mkubwa ili kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa na Serikali yanafikiwa.

“Ndugu zangu kwanza kabisa tufahamu hali ya maralia ni mbaya maambukizi ni asilimia 31.2%  kwahiyo tunatakiwa kuhakikisha maralia inaisha kama walivyofanikiwa Zanzibar.”Alisema Canal Mwila

Aidha alitoa wito kwa Halmashauri ya Ukerewe baada ya ABT kumaliza mradi huo, waendelee kutoa elimu kwa wananchi jinsi ya kujikinga na Maralia huku akitoa onyo kwa wale wote ambao wamejipanga kukwamisha zoezi hilo.

“Ndugu wananchi zoezi hili lipo kwa mujibu wa sheria ya afya ya mwaka 2009 kifungu cha 1 kinasema ni namna gani mtu atakayezuia chanjo au mazoezi ya kujikinga na Maralia atakachofanyiwa faini yake ni 500,000 hadi 1,000,000 au kifungo cha miezi sita (6) kwa kuwa nia ya Serikali ni njema niombe ushirikiano na kama itashidikana tutatumia nguvu kidogo.” Alisema Canal Mwila

Ameongeza kuwa kumekuwepo na dhana ya upotoshaji juu ya zoezi hilo huku baadhi ya watu wakisema kuwa dawa hizo zinapunguza nguvu za kiume au kuleta kunguni akisema jambo ambalo si kweli huku akitaja kufanikiwa kwa zoezi hilo kutategemea ushirikiano wa  serikali, timu inayofanya kazi, ABT, wanyunyuziaji na wanchi kwa ujumla.

Ukerewe inatajwa kuwa na maambukizi makubwa ya Maralia kwa asilimia 51.7% kwa takwimu za mwaka 2017 kwa Wilaya zinazounda Mkoa wa Mwanza,   ambapo maambukizi hayo kimkoa  ni  asilimia 8.2% na Kitaifa yakiwa ni asilimia 7.5%.

Akitoa taarifa ya mapambano dhidi ya ugonja huo, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Dkt Getera Nyangi alisema Wilaya ya Ukerewe imeendelea na mpambano dhidi ya ugonjwa huo kwa kutumia njia shirikishi kati ya jamii na wadau wa afya ABT ASSOCIATES na wadau wengine waliopo Wilayani humo, ili kufikia Lengo la kupunguza maambukizi kutoka asilimia 51.7% za mwaka 2017.

Aidha Wilaya ya Ukerewe mpaka kufikia  Oktoba mwaka 2021 ilifanikiwa kupunguza Maralia hadi kufikia asilimia 31.2% ikiwa Lengo la Kitaifa kupunguza kiwango cha maambukizi kufikia asilimia 3.5% ifikapo mwaka 2025 ambapo hali ya maambukizi itapungua kwa asilimia 74%.

“ Mikakati mbalimbali imekuwa ikitekelezwa ikiwemo, utoaji wa elimu ya afya juu ya madhara ya Maralia, kuhimiza na kusimamia shuguli mbalimbali za usafi wa mazingira, pamoja na kuendeleza zoezi la kunyunyuzia dawa ya kibiolojia ili kuharibu mazalia ya mbu waenezao Maralia.” Alisema Dkt Mwila

Mikakati mingine ni vituo vya kutolea huduma za afya kuweka bajeti kwa ajili ya kununulia dawa za kibiolojia, kuhimiza wananchi kulala ndani ya chandarua chenye viuatilifu, kuhimiza wanawake wajawazito kuhudhuria kliniki na kupatiwa dawa za SP pamoja na upuliziaji wa dawa ya ukoko majumbani zoezi linaloendelea mpaka sasa.

Kwa upande wake Joshua Mutagahywa afisa Mazingira na usalama kazini kutoka Shirika la  ABT ASSOCIATES ameupongeza uongozi wa wilaya ya Ukerewe kwa ushirikiano mkubwa ambao amekua akiupata kutoka ngazi mbalimbali za uongozi.

“Kwanza tunashukuru kwa ushirikiano kutoka kwa ofisi ya Mkurugenzi na hasa  idara ya mipango, watendaji wa kata, wa vijiji mpaka wa vitongoji kwa kutupa takwimu sahihi za nyumba ambazo wtu wanalala ambazo ndo hasa lengo lengo la unyunyuziaji.

Vilevile aliiomba Serikali ya wilaya kuhakikisha inaendelea kuwaelimisha wananchi umuhimu wa zoezi hilo ili kusiwepo na ugomaji wa namna yoyote ile kutoka ka wananchi na viongozi.

“Sisi tunalenga kunyunyuzia nyumba 125,250 kwa matayarisho yetu kuanzia madawa, vifaa,  muda na watendakazi tunaweza kuzifikia hizi nyumba lakini tunaweza kukwama iwapo kuna baadhi ya wananchi na viongozi ambao wanazuia hili zoezi hivyo tunaomba serikali iweze kuwashawishi kusiwepo na sababu za ugomaji” Aliongeza Afisa Mazingira wa ABT

Zoezi la upuliziaji dawa ya ukoko majumbani ni moja ya afua zinazotekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwenye mapambano dhidi ya ugonjwa hatari wa Maralia katika Wilaya ya Ukerewe ikitekelezwa na Wizara ya Afya Maendeleo  ya Jamii, Jinsia wazee na watoto, Mpango wa Taifa wa kudhibiti Maralia, Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe kwa kushirikiana na Shirika la Abt Associaes kwa ufdhili wa          Shirika la Kimataifa la misaada kutoka Marekani USAID.

Zoezi hilo limeanza tokea tarehe Novemba 18 mwaka huu na linatarajia kukamilika Disemba 18 Wilayani humo likihusisha wapuliziaji 517 katika kambi 25 zilizopo wilayani humo.

No comments:

Post a Comment