Tuesday, November 23, 2021

NAIBU WAZIRI MABULA AANZA KUWASHUKIA WATENDAJI ARDHI WASIOTEKELEZA MAAGIZO YAKE

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na Watendaji wa sekta ya ardhi katika Manispaa na Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba akiwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Kagera tarehe 22 Novemba 2021. Kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Bukoba Moses Machali.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimkabidhi Hatimiliki ya ardhi mkazi wa kata ya Bakoba mtaa wa Nyakanyasi Manispaa ya Bukoba Bi. Grace Kokuledi wakati wa ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Kagera

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa wilaya ya Bukoba na wananchi aliowakabidhi hatimiliki za ardhi wakati wa ziara ya siku mbili mkoani Kagera

Na Munir Shemweta, BUKOBA

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameanza kuchukua hatua kwa watendaji wa sekta ya ardhi wanaoshindwa kutekeleza maagizo anayoyatoa wakati wa ziara zake kwa kumtaka Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Kagera Erick Makundi kuwaandikia barua ya kujieleza watumishi wawili wa Halmashauri na Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.

Watumishi wanaotakiwa kujieleza kwa nini wasiondolewe katika nafasi zao ni Mkuu wa Idara ya Ardhi na Mipango Miji Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera Catres Rwegasira na Kaimu Mkuu wa Idara ya Ardhi na Maliasili Halmashauri ya Bukoba ambaye pia ni Afisa Ardhi Mteule wa halmashauri hiyo Fidelis Alute.

Hatua ya Naibu Waziri Mabula inafuatia watendaji hao kushindwa kutekeleza maagizo waliyopewa kwa nyakati tofauti na Waziri huyo akiwa katika ziara zake mkoani Kagera ikiwa ni ufuatiliaji wa utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika maeneo mbalimbali nchini.

“Watendaji hawa lazima wajieleze kwa nini wasichukuliwe hatua na nitafuatilia maana tunachohitaji ni utii  kwa watumishi wa sekta ya ardhi huwezi kusafiri na kuja na kutoa maelekezo  halafu yasifafanyiwe kazi, hatuwezi kwenda na hali hiyo” alisema Dkt Mabula.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri Mabula kokote atakapopita na kukuta hakuna utekelezaji wa maagizo aliyoyaacha atachukua hatua kali kwa wahusika lengo likiwa kujenga nidhamu na kuhakikisha kero za wananchi katika masuala ya ardhi zinashughulikiwa.

Hata hivyo, Dkt Mabula ambaye alikuwa akizungumza na watendaji wa sekta ya ardhi katika Manispaa na Halmashauri za Bukoba mkoani Kagera tarehe 22 Novemba 2021 alisema, kutokana na baadhi ya watumishi wa sekta ya ardhi kufanya kazi kwa mazoea kuna haja ya kuwabadilisha vituo vya kazi watumishi waliokaa muda mrefu kwenye kituo kimoja.

“Tunahitaji kufanya reshuffle kwa  kuangalia muda ambao mtumishi amekaa kwenye kituo kimoja cha kazi maana tunapokuwa na mtu amekaa kituo cha kazi kwa zaidi ya miaka mitano anafanya kazi kwa mazoea na kukwamisha utendaji kazi” alisema Dkt Mabula.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Bukoba Moses Machali aliwaambia watumishi wa sekta katika halmashauri na Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera kujifunza kutelekeza maagizo yanayotolewa na viongozi na kwenda kinyume na maagizo hayo ni jambo baya.

Aidha, aliunga mkono maelezo ya Naibu Waziri kutaka watumishi wa sekta ya ardhi waliokaa katika kituo kimoja muda mrefu kubadilishwa vutuo vya kazi kwa lengo la kuleta ufanisi.

Pia Machali alisema, msisitizo wake ni kuwataka watendaji wa sekta ya ardhi kuwafuata wananchi kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero na migogoro ya ardhi katika maeneo yao badala ya kuwasubiri ofisini.

“Mhe Naibu Waziri nikuunge mkono katika hili la watendaji wa sekta ya ardhi kuwafuata wananchi katika maeneo yao kutatua migogoro ya ardhi maana hapa ofisini kwangu unakuta kuna foleni kama wodi ya wagonjwa hivyo haiwezekani mimi DC kubeba majukumu ya watu wakati wahusika wapo” alisema Machali.

No comments:

Post a Comment