Kuelekea miaka 60 ya
Uhuru wa Tanganyika na 59 ya Jamhuri, Wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza
imezindua tamasha la mawasiliano, utalii, utamaduni pamoja na maonyesho ya
biashara litakalovikutanisha vikundi mbalimbali vya Sanaa, utamaduni , ngoma
asilia na vikundi vya wafanyabiashara .
Akizungmza na waandishi
wa habari Novemba 19, 2021 Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe, Amina Makilagi
alisema anawashukuru sana waandaaji wa maonyesho ya tamasha hilo kuichagua
Nyamagana kuwa sehemu ya maonyesho hayo.
“ Maonyesho haya ya
kibiashara, utalii na mawasiliano katika
nchi yetu, tunataka kwenda kuonyesha jamii namna tulivyopiga hatua katika
Nyanja mbalimbali kama unavyojua Jiji la
Mwanza ndo kitovu cha kila kitu na tunatengeneza uchumi wa buluu kupitia
uvuvi.” Alisema Mhe, Makilagi
Alisema Mwanza ni
kiungo kikubwa cha mawasiliano kwa Mikoa ya Kanda ya Ziwa na nchi jirani hivyo
kupitia maonyesho hayo ni fursa kubwa na kipekee kwa Mkoa wa Mwanza kuyatumia
na kujiletea maendeleo kwani kutokea Mwanza unaweza kupeleka bidhaa zako Kenya,
Uganda na hata Burundi.
“ Mwanza ni kitovu cha
mawasiliano, Mwanza ni lango la kuingia na kuunganisha mikoa ya Kanda ya Kanda
ya ziwa na kitovu cha biashara katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa maonyesho yamekuja
hapa tunaenda kuitangazia jamii kwamba wapi tulipotoka katika kupigania uhuru .”
Aliongeza Mhe, Makilagi
Aidha kupitia maonyesho
hayo kutakuwa na banda maalumu ambalo litakuwa likionyesha na kuelezea harakati
zilizokuwa zikifanywa na hayati Baba wa Taifa katika kupigania uhuru ili
Watanzania waweze kujifunza.
Naye Mratibu wa Tamasha
hilo Buche Buche Enos amesema Lengo la Tamasha hilo kuhamasisha utalii Mkoani
Mwanza nani fursa ya pekee kutangaza
vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo ili jamii ivitambue na kuanza
kuvitembelea kwa lengo la kujifunza masuala mbalimbali yahusuyo utalii.
Alisema katika tamasha
hilo la siku 10 ambalo limeanza tarehe 19 - 29 Novemba litapambwa na michezo na
mashindano mbalimbali yakiwemo mashindano ya mitumbwi yakihusisha mitumbwi 15
ya wanawake itakayobeba wanawake 3 na
mitumbwi 25 ya wanaume itakayobeba wanaume 3 kila mmoja kufikisha idadi
ya wanaume 75 .
Kwa upande wake Afisa
utamaduni Mkoa wa Mwanza Bi Agnes Majinge alisema ndani ya siku 10 hizo
watakusanya wajasiliamali, wafanyabiashara lakini pia watahamasisha utalii wa
kitamaduni kwa vile Mwanza kuna vivutio vingi vya utalii.
“Jiji la Mwanza lina
fursa nyingi za kibiashara, tutakuwa na mashindano ya ndoma, kwaya, kazi za
mikono mfano usukaji wa mikeka lakini pia tutakuwa na taasisi mbalimbali za
kibiashara na watoa huduma kama ngoma nk.” Alisema Bi Agnes
Alisema katika
maonyesho yanayoendelea katika uwanja wa Malamala uliopo Igoma wameandaa maeneo
kulingamna na aina ya bidhaa mfano kuna maeneo ya wafanyabiashara wa kazi za
utamaduni, kazi za mikono, kuchora, kuchonga,
biashara ndogondogo na wajasiliamali.
Akizungmzia mashindano ya Mitumbwi Bi Majinge alisema zawadi mbalimbali zitatolewa kwa washindi kuanzia mashindano ya ngoma za asili , mitumbwi, kwaya na muziki wa kizazi kipya.
No comments:
Post a Comment