Chama cha wafanyabiashara wanawake Mkoa wa
Mwanza(TWCC) kimeendelea kupanua wigo wake kwa Kufungua matawi mkoani humo na
kuvuna wananchama 70 wilayani Misungwi.
Katika hafla ya uzinduzi wa tawi hilo iliyofanyika
wilayani Misungwi Mkoani Mwanza, Mkuu wa wilaya ya Misungwi Veronica Kessy,
aliwataka wanawake Wilayani humo kuitumia TWCC kukamilisha ndoto zao za
kibiashara.
“ Natambua Misungwi wako wanawake wengi sana
wanaojishughulisha na biasahara kubwa, za kati na ndogo lakini pia kuna
wajasiliamali wadogo wadogo hivyo uwepo wa TWCC utawasaidia sana kuleta
mabadiliko katika biashara zenu.” Alisema Bi Kessy
Aidha aliwashauri wanawake wafanyabiashara wilayani
humo kujiunga na TWCC kwani kwa muda mrefu wamekuwa wakitoa fursa za mafunzo
kwa wanawake wafanyabiashara lakini pia kupitia maonyesho mbalimbali wamekuwa
wakiwakutanisha wanawake na kujifunza kutoka kwa wanawake wenzao.
“ TWCC wamekuwa na mtandao mkubwa na taasisi
nyingine ambazo zinajihusisha moja kwa moja na wafanyabiashara mfano taasisi za
kifedha , SIDO na taasisi zingine ambazo zinatoa elimu kwa wafanyabiashara
namna ya kuboresha na kukuza biashara zao.” Aliongeza Bi Kessy
Katika Risala yao waliomba Mkuu huyo awe mlezi wao
jambo ambalo alilikubali na kuahidi kuwapa ushirikiano katika kila jambo
linalohusu wanawake Wilayani humo.
Akizungumza na wazo huru Blog Mwenyekiti wa TWCC
Mkoani Mwanza Bi Fausta Ntara alisema lengo la kufungua tawi hilo wilayani
humo, ni kuhakikisha fursa mbalimbali za wanawake zinawafikia hata ambao wapo
vijijini.
Alisema mara nyingi fursa uwa zinafikia maeneo ya
Mijini tu hivyo baada ya kutambua kwamba hata maeneo ya nje ya Miji kuna
wajasiliamali wakaona waanze kupeleka huduma na huko, Tawi la Misungwi likiwa
ni tawi lao la pili kufunguliwa katika Mkoa wa Mwanza.
“TWCC ni kampuni ya wanawake wote na makampuni mengi
yanapokuja hufikia mjini na TWCC ni ya wanawake wote wajasiliamali na
wafanyabiashara sasa tukaona ni vyema tupeleke huduma hii kwa wanawake waliopo
nje ya Mji.” Alisema Bi Fausta
“ Wajasiliamali wengi wapo nje ya Mji waliopo mjini
ni wachache sana na wapo kwa sababu wengi wapo kwasababu waume wao wapo Mjini
na wengine ni waajiliwa lakini wengi wapo huku nje ya Mji.” Aliongeza Bi Fausta
Akizungumzia fursa mbalimbali zinazopatikana TWCC
alisema ni mafunzo wanayoyatoa kupitia taasisi wanazoshirikiana nazo, lakini
pia huwakutanisha wanawake wafanyabiashara kupitia maonyesho mbalimbali
wanayoandaa hivyo wanawake hujifunza kutoka kwa wanawake wenzao.
Kabla ya uzinduzi huo wanawake hao walipewa elimu na
mafunzo kutoka taasisi mbalimbali za kifedha na taasisi za kimafunzo ya
kibiashara ambazo zilihalikwa kutoa mada katika hafla hiyo
Bakari Ally Songwe Meneja wa SIDO Mkoani Mwanza aliyekuwa
mmoja wa wawezeshaji katika hafla hiyo alisema ni miaka kadhaa sasa SIDO
imekuwa ikitoa elimu na fursa kwa wafanyabiashara na wajasiliamali.
Alisema SIDO ina jukumu la kusimamia na kuendeleza
biashara na viwanda vidogo na inafanya kazi kubwa nne moja ikiwemo utoaji wa
mafunzo mfano ujasiliamali, mafunzo ya hati miliki, utengenezaji wa mashine
mbalimbali na utoaji wa mikopo kwa wafanyabiashara pamoja kuhakikisha bidhaa za
wafanyabiashara zinafika sokoni.
Mmoja wa wajasiliamali waliofika katika hafla hiyo
Bi Fortunata Nkwande mkazi wa Misungwi kata ya Ukiriguru mtengezenaji wa
sabuni, batiki, karanga za mayai na unga wa lishe ameupongeza sana uoingozi wa
TWCC kufungua tawi wilayani humo akiamini wataleta tija kubwa sana wilayani
humo.
“ Niwapongeze sana TWCC kutuona wanawake wa Misungwi
na tulikuwa tunapitwa sana na fursa mfano tuna changamoto kuhusu barcode, vifungashio naamini kupitia
viongozi wetu tutapata elimu na mafunzo ya namna bora za kufungasha na hivyo
kuongeza tija kwenye biashara zetu.” Alisema Bi Fortunata
No comments:
Post a Comment