Na Mathias Canal, Kalangala, Uganda
Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Kilimo imejipanga katika kuhakikisha inampatia mwekezaji eneo la kuwekeza kwenye zao la michikichi, kutoa elimu kwa wakulima na kuwasaidia kifedha ili kuhakikisha nchi inapunguza ama kumaliza kabisa kadhia ya kuagiza mafuta ya mawese kutoka nje ya nchi.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda tarehe 25 Novemba 2021 wakati alipotembelea kiwanda cha kuchakata mafuta cha kampuni ya Oil Palm Uganda Limited kilichopo katika kisiwa cha Kalangala nchini Uganda wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku nne nchini humo.
Waziri Mkenda amesema kuwa Serikali ya Tanzania itaimarisha mfumo wa kilimo cha Michikichi kwa kuhakikisha kuwa inatoa elimu ya kutosha kwa wakulima kwa utaratibu ambao utahusisha mashamba makubwa na mashamba ya wakulima wadogo ili kuwa na kilimo chenye tija kinachowakikishia soko kwenye viwanda.
“Mtazamo wetu sasa hivi tutakaporudi nyumbani tumewaomba mwezi wa 12 waende mkoa wa Kigoma na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma ameanza kuona sehemu ambayo itatusaidia kuwapa eneo kwenda kuwaandaa wakulima wa kule kwa ajili ya kujipanga kuandaa mashamba ” Amebainisha Waziri Mkenda
Amesema kuwa kwa namna yeyote ni lazima Serikali iandae fedha za kutosha kwa ajili ya kutoa elimu na kuwasaidia wakulima kwani kilimo cha zao la Michikichi hutumia miaka mitatu mpaka minne kabla ya kuanza kuvuna ili kuhakikisha wakulima wanafurahia kilimo hicho.
Pia waziri Mkenda amebainisha kuwa kwa sasa mikoa iliyoainishwa kwa kuanzia ni Mkoa wa Kigoma na Katavi ambapo amesema endapo kilimo hicho hakitawekewa mkazo nchi itaendelea kubaki kwenye kadhia ya kuagiza mafuta ya Mawese kwa gharama kubwa kutoka nje.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Kamishna Jenerali Thobias Andengenye amesema kuwa suala hilo linalotegemewa kuanzishwa na Serikali ya Awamu ya Sita katika Mkoa wa Kigoma ni la kuufungua mkoa huo kiuchumi kupitia mradi huo wa uzalishaji mazao ya michikichi.
Ameongeza kuwa kilimo cha zao la Michikichi ndicho kilimo chenye unafuu na uvumilivu na chenye urahisi wa kupata soko la uhakika hivyo wananchi na wakulima wa mkoa wa Kigoma wameisubiri fursa hiyo kwa muda mrefu na wapo tayari kuitumia ili kuleta mapinduzi ya kiuchumi.
Pia amebainisha kuwa Mkoa wa Kigoma una eneo kubwa la Kilimo na hali ya hewa rafiki kwa kilimo cha Michikichi hivyo mkoa huo unaweza ukawa ndio wazalishaji wakubwa Afrika nzima endapo wakulima wakiwezeshwa na wawekezaji wakijitokeza kuwekeza .
Naye Mkurugenzi wa Mazao wa Wizara ya Kilimo Nyasebwa Chimagu amesema kuwa wizara imejipanga na kudhamiria katika kuhakikisha kuwa nchi inajitosheleza kwa kuwa na uhakika wa mafuta ya kula na juhudi hizo zimeanza katika zao la Alizeti na pia kwenye zao la Michikichi.
Pia amebainisha kuwa jitiahada hizo zimeanza katika kuhakikisha zao la michikichi linafufuliwa hivyo kupitia ziara hiyo wamejifunza na kuona namna ya kufanya zao hilo kuwa zao la kibiashara.
Pia mebainisha kuwa Wizara imejipanga kufanya mageuzi kwa kufanya majukumu kama kuwaunganisha wakulima kwa pamoja kupitia vyama vya ushirika na kutambua mashamba yaliyopo na kuona maeneo yanayofaa kwaajili ya kilimo hicho.
Na jukumu lingine ni kuhakikisha kituo cha utafiti Nkinga Kigoma kuwa kitovu cha mafunzo kwa wakulima ili kuhakikisha kwamba wataalamu wanapata mafunzo na wakulima ili kile ambacho kimekusudiwa cha kuwa na mashamba ya pamoja pia wanakuwa na elimu ya Kutosha
No comments:
Post a Comment