Friday, October 15, 2021

BENKI YA TCB KUTOA MAFUNZO YA KIBIASHARA KWA WANAWAKE MWANZA


Wafanyakazi WA benki ya TCB wakiwa katika picha ya pamoja

Meneja Masoko na mawasiliano makao makuu Grace Majige


Meneja wa Tawi la Pamba Alex Minai.

Benki ya Biashara ya Tanzania (TCB) imeandaa kongamano kubwa  litakalowakutanisha wanawake wafanyabiashara , wajasiliamali, waajiriwa, waliopo vyuoni  wateja wa benki hiyo na wasio wateja kwa lengo la kumfanya mwananmke kujitambua kuwa  yeye ana wajibu mkubwa katika kukuza uchumi wa Taifa.

Akizungngumza Oktoba 15, 2021 katika kipindi cha Morning Express kinachorushwa na City Fm Radio 90.5 ya Jijini Mwanza Meneja masoko na mawasiliano wa Benki hiyo makao makuu Grace Majige amesema kwa kutambua  mchango mkubwa wa mwanamke kuanzia ngazi ya familia kama kusomesha wameona waandae kongamano hilo ambalo mwanamke atajifunza mambo mbalimbali kutoka kwa wanawake wenzake.

“ Kila mmoja anatambua mwanamke ana mchango mkubwa sana  tangia ngazi za familia lakini pia hela anayopata mwananmke uwa inarudi nyumbani  hivyo sisi kama benki tunataka kumsaidfia mwanamke ajifunze mengi kutoka kwa wenzie lakini pia ajue kama ana mchango mkubwa sana kwenye taifa hili.” Amesema

Aidha amewataka wanawake wa Mwanza kuhudhuria  kongamano hilo kwani ni fursa pekee na muhimu kwa kila mmwanamke anayependa kushiriki katika kukuza uchumi wa Taifa na ambaye anapenda kujifunza kwani siku hiyo watawasikia wanawake mbalimbali  ambao wataelezea hatua, changamoto na mambo mbalimbali waliopitia mpaka kutimiza ndoto zao.

Kwa upande wake meneja wa Tawi la TCB lililopo Pamba Alex Minai amesema mbali na kongamano hilo Benki hiyo ya Serikali  imekuwa ikitoa huduma mbalimbali ikiwemo mikopo ya vikundi,  mteja wa biashara ya katikati, mteja mkubwa na makampuni.

“Kuna akaunti za vikundi, watu binafsi, za makampuni , za vikundi ambayo operesheni yake ni bure kabisa na katika kuelekea siku ya jumatatu tarehe 18 tuna akaunti maalumu kabisa kwa ajili ya wanawake inayojulikana kama tabasamu imbayo ipo kwa ajili ya mtu mmoja au kwa vikundi na siku hiyo ya kongamano tutawafungulia akaunti kwa watakaokuwa tayari.” Amesema  

Aidha amesema anawakaribisha wanawake wote wa Mkoa wa Mwanza  lakini watakaoshiriki ni wale tu ambao wamepewa mwaliko na kwa wale ambao bado hawajapata mwaliko  wanatakiwa kufika na  kujisajili katika mojawapo ya matawi yao yanayopatikana eneo la Liberty, Pamba na Kenyata

“Tungependa tuwe na wanawake wote lakini kwa sababu ya ufinyu wa eneo watakaohudhuria ni wale waliopewa mwaliko tu na ili uweze kushiriki fika katika matawi yetu uweze kujisajili kwani siku hiyo kuna vitu vizuri sana ambavyo vimeandaliwa na benki yetu. ” Amesema

Naye afisa kutoka kitengo cha bima Makao makuu Emmanuel Kaganda  amesema mafunzo mbalimbali yatatolewa kama  namna ya ukuzaji wa biashara pamoja na kutumia changamoto kama fursa na hii ni maalumu kwa wale ambao wakianzisha biashara inapokwama  kidogo tu huamua kuachana nayo.

“ Watu wengi wana ndoto ya kufungua na kuanzisha biashara mfano kufuga nk, sasa wengi ikitokea labda ameanza kufuga na ikitokea mfugo wake umekufa anaamua kuacha sasa kupitia mafunzo haya tunaamini tutazalisha wafanya biashara wasiokata tamaa.”  Amesema

Benki ya Serikali ya Biashara (TCB) ni muunganiko wa benki ya Maendeleo (TIB) na benki ya Posta (TPB) ambayo ilizinduliwa julai 15, 2021 na Waziri wa fedha Mwigulu  Nchemba ikiwa ni jitihada za serikali kujenga uchumi imara na shindani.

Kongamano hilo lenye kauli mbiu  ”nafasi ya mwanamke katika kukuza uchumi wa Taifa”  litafanyika katika ukumbi wa Rocky City Mall Mwanza Oktoba 18, 2021 kuanzia saa 1:30 asubuhi ambapo Zaidi ya wanawake 400 wanatarajiwa kuhudhuria.

No comments:

Post a Comment