Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda (Wa Pili Kushoto) akizindua Viwanda viwili cha kusaga mahindi na kuchakata alizeti vilivyopo ofisi za Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB) eneo la Kizota Jijini Dodoma, jana tarehe 19 Agosti 2021. Wengine pichani ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini Mhe Jabir Shekimweri (Wa Kwanza KUshoto), Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mhe Antony Mavunde (Wa Pili Kulia) na Mkurugenzi wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Dkt Anslem Moshi (Wa kwanza kulia). (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Na Mathias Canal, Wizara ya
Kilimo-Dodoma
Waziri wa Kilimo, Prof. Adolf
Mkenda ameitaka Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB) kuhakikisha inafanya
maamuzi yake kibiashara ili kujiepusha na anguko lililozikumba taasisi
zilizotangulia.
Prof. Mkenda ameyasema hayo
jana tarehe 19 Agosti 2021 wakati akizindua Viwanda viwili cha kusaga mahindi
na kuchakata alizeti vilivyopo ofisi za CPB eneo la Kizota Jijini Dodoma.
Amesema Taasisi zilizokufa za
General Agricultural Products and Exports Board (GAPEX) na National Milling
Corporation (NMC) ilitokana na kufanya maamuzi mengi kufanyika kwa misingi
isiyokuwa ya kibiashara.
"Mwelekeo ni mzuri
umenipa matumaini kwamba hamtashindwa tena kama kwenye National Milling na
GAPEX, "alisema Prof. Mkenda.
Amefafanua zaidi ya kuwa serikali
itazidi kuwa pamoja na bodi hiyo ili kuhakikisha wanafanya vizuri katika
masuala ya usimamizi wa mazao ili kuleta matokeo chanya.
Hata hivyo, ameitaka bodi
hiyo kuhakikisha inatekeleza suala la kuingia kwenye mkataba na wakulima
wakubwa na wadogo wa kilimo cha alizeti ambao watajiunga kwenye ushirika ili
kusaidia kuongeza uzalishaji wa mafuta ya kula nchini.
Amesema kuwa wakifanya hivyo
wao, serikali itasimamia katika suala zima la Maafisa ugani na kuzalisha mbegu
bora za alizeti ambazo zitatoa mafuta kwa wingi.
Amewataka wakulima kutumia
fursa hiyo ya CPB kulima mashamba makubwa yatakayo wawezesha kuingia kilimo cha
mkataba na bodi hiyo ili kufanya Kilimo chenye tija.
Akizungumzia suala la
mahindi, amesema CPB wanapaswa kutangaza soko la mahindi nje ya nchi kwa sababu
mahindi ya Tanzania hayana Sumukuvu.
Waziri Mkenda amesema kuwa
CPB wanapaswa kusimama imara kuhakikisha wanatangaza soko kwa sababu wamekagua
mahindi na kuona yana kila aina ya sifa na ubora wa kuuzwa popote.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa
CPB, Dkt Anselm Moshi, amesema viwanda ambavyo wamezindua cha mahindi kina
uwezo wa kusaga tani 60 kwa siku huku cha Alizeti tani 40 kwa siku.
Aidha, amesema viwanda hivyo
wametumia jumla ya Tsh Bilioni 7.092 ambapo fedha nyingine wamepata mkopo
kutoka NSSF.
MWISHO
No comments:
Post a Comment